Tuesday , 3 October 2023
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Kesi ya Abdul Nondo: Mahakama yathibitisha uongo wa Polisi
Makala & UchambuziTangulizi

Kesi ya Abdul Nondo: Mahakama yathibitisha uongo wa Polisi

Spread the love

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Iringa imetoa hukumu yake katika kesi iliyokuwa inamkabili kiongozi wa Programu ya Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Mahmoud Nondo. Anaandika Tundu Lissu, Tienen, Belgium … (endelea).

Mahakama hiyo imemkuta Abdul Nondo hana hatia kwa makosa yote mawili aliyoshtakiwa nayo, yaani, kutoa taarifa ya uongo kwamba alitekwa nyara akiwa Ubungo, Dar Es Salaam, na kusafirishwa usiku na watu wasiojulikana hadi Mafinga mkoani Iringa walikomtupa; na kusambaza taarifa zisizokuwa na ukweli kwa njia ya mtandao.

Kwa maoni yangu, kilicho muhimu katika hukumu ya kesi hii sio uamuzi wenyewe peke yake. Kwa yeyote anayefuatilia kesi za jinai katika Mahakama zetu kwa umakini, angejua Abdul Nondo hatapatikana na hatia, kwa jinsi wapelelezi wa Jeshi la Polisi la nchi hii wanavyojua kukoroga ushahidi mahakamani, hasa pale ambapo watuhumiwa wanatetewa na mawakili.

Kilicho muhimu zaidi ni sababu zilizotolewa na Mahakama katika kumwachia huru Abdul Nondo. Sababu hizo zinathibitisha jinsi ambavyo Jeshi la Polisi la Tanzania limekuwa sasa ni tatizo, badala ya kuwa suluhisho, la matukio ya utekaji nyara ambayo yameshamiri sana katika Tanzania ya Magufuli.

Katika hukumu yake ya leo, Mahakama ya Hakimu Mkazi imesema kwamba, “tangu mwanzoni (Abdul Nondo) alichukuliwa kama mtuhumiwa na sio mlalamikaji.” Kwa mfano, “polisi walimnyang’anya vitu vyake kabla hata ya kuchukua maelezo yake, ikiwa ni uthibitisho kwamba walimwona sio mtu mwaminifu kuanzia aliporipoti tukio la kutekwa nyara mpaka aliposhtakiwa (mahakamani).”

Aidha, Mahakama ililishutumu Jeshi la Polisi kwa “… kutelekeza wajibu wake wa kisheria wa kuchunguza kama kweli mtuhumiwa alitekwa nyara, lakini haraka haraka lilikimbilia kumtuhumu mshtakiwa kuwa alijiteka mwenyewe, bila hata kuonyesha alifikaje Mafinga.”

Mahakama pia ilikataa kukubali kwamba maelezo aliyodaiwa kuyatoa Abdul Nondo polisi, na ambayo yaliwasilishwa kortini kama kielelezo, yalikuwa ni ya kwake kweli.

Kwa mujibu wa Mahakama, wakati sehemu ya kiapo cha mtuhumiwa inaonyesha maelezo yalikuwa kwenye ukurasa mmoja tu, kilichowasilishwa mahakamani kama maelezo ya mtuhumiwa kilikuwa kwenye kurasa nne. Kwa hiyo, “Mahakama inakataa kuamini kwamba hayo ni maelezo ya mtuhumiwa.”

Hukumu ya Abdul Nondo vile vile inatoa mwanga mkubwa kuhusu wahusika wa utekaji nyara huo.

Katika ushahidi wake, Abdul Nondo alielezea alivyotekwa nyara na kilichomtokea wakati akiwa mateka, na baadae akiwa mikononi mwa Jeshi la Polisi.

Kama ilivyotokea kwa Mo Dewji, Abdul Nondo na yeye alidakwa na watu wasiojulikana na kuingizwa kwa nguvu kwenye gari iliyokuwa na vioo vyeusi.

Baada ya kutekwa nyara na akiwa ndani ya gari hilo, alianza kupigwa na watekaji huku akiulizwa awataje watu waliokuwa nyuma ya mpango wa maandamano ya kupinga kuuawa kwa mwanafunzi Aquilina Aquiline wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Vile vile, na cha kushangaza, watekaji nyara hao walimhoji Abdul Nondo kwa nini alikuwa anatumiwa na ‘wanasiasa’ na CHADEMA.

Kama ilivyokuwa kwa Mo Dewji, watekaji nyara hao walimtupa Abdul Nondo machakani usiku mpaka alipookotwa na wapita njia.

Ushahidi huu haukupingwa wala kutikiswa kwa namna yoyote ile na upande wa mashtaka.

Kwa mujibu wa ushahidi wake, baada ya kugeuziwa kibao na polisi na kusafirishwa na hadi Dar Es Salaam, Abdul Nondo alihojiwa na wapelelezi wa Polisi Makao Makuu.

Cha ajabu ni kwamba maswali aliyoulizwa na wapelelezi wa polisi ni yale yale aliyoulizwa na watu wasiojulikana waliomteka nyara, i.e. nani walikuwa nyuma yake; kwamba kwa nini alikuwa anatumiwa na ‘wanasiasa’; na kwamba alikuwa na uhusiano na Mwenyekiti wa CHADEMA na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mh. Freeman Mbowe na Kiongozi Mkuu wa ACT, Mh. Zitto Kabwe.

Aidha, Abdul Nondo aliiambia Mahakama kwamba alielekezwa na wapelelezi wa polisi “kukiri mbele ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwamba alijiteka mwenyewe; na kwamba aitishe mkutano wa waandishi habari na kuutangazia umma kwamba alikuwa anatumiwa na wanasiasa.”

Alipokataa kufanya hivyo, Abdul Nondo aliendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa siku 21, kabla ya kusafirishwa tena hadi Iringa ambako alishtakiwa mahakamani.

Ushahidi huu pia haukupingwa wala kuhojiwa kwa namna yoyote na upande wa mashtaka.

Kwa ushahidi wa hukumu hii ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Iringa, mtuhumiwa wa kwanza wa kutekwa kwa Abdul Nondo ni Jeshi la Polisi na au vyombo vingine vya usalama vya Serikali ya Magufuli.

Hii ni kwa sababu, kulingana kwa maswali ya watekaji nyara na wapelelezi wa polisi waliokuwa wanamhoji Abdul Nondo haiwezi kuwa ni kitu cha bahati mbaya tu.

Hii pia ni kwa sababu Jeshi la Polisi limejenga tabia mbaya ya kuisingizia CHADEMA kwa matukio ya kihalifu yanayofanywa na baadhi ya askari polisi.

Mifano ni mingi. Shambulio la mabomu ya kurushwa kwa mkono kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi wa marudio Soweto, Arusha, mwaka 2012, lililoua watu wanne na kujeruhi wengi wengine, lililaumiwa kwa CHADEMA.

Hadi leo hakuna uchunguzi wowote uliofanywa na Jeshi la Polisi kuhusu uhalifu huo, na wauaji wa Watanzania wale hawajulikani mpaka sasa.

Mwaka huo huo, Jeshi la Polisi mkoani Iringa lilimuua mpiga picha wa Channel Ten, Daudi Mwangosi, kwa kumlipua kwa bomu la kishindo.

Mara moja Jeshi la Polisi lilitoa taarifa hadharani likiituhumu CHADEMA kwamba wafuasi wake ndio waliorusha ‘kitu kigumu’ kilicholipuka na kumuua marehemu Mwangosi.

Baadae, uchunguzi rasmi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Baraza la Habari Tanzania (MCT) ulithibitisha kwamba Daudi Mwangosi aliuawa na askari polisi, kwa amri ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Michael Kamuhanda.

Na katika tukio la kushambuliwa kwangu la September 7 mwaka jana, Jeshi la Polisi limeshindwa kufanya uchunguzi wowote, huku likiwaachia wapambe wa CCM na Rais Magufuli wakieneza propaganda chafu hadharani kwamba Mwenyekiti Mbowe ndiye anayehusika na kushambuliwa kwangu.

Sasa, kwa hukumu hii, njama hizi za Jeshi la Polisi za kuipakazia CHADEMA zimeumbuka mahakamani. Sasa Jeshi la Polisi na Serikali ya Magufuli iliyodai kwamba Abdul Nondo alijiteka mwenyewe watuambie ukweli: nani waliomteka Abdul Nondo na kwa nini hawajakamatwa wala kuchukuliwa hatua za kisheria hadi sasa???

Jeshi la Polisi na Serikali ya Magufuli watuambie kwa nini maswali ya watekaji nyara na ya wapelelezi wa polisi kwa Abdul Nondo yanalingana, kama huu haukuwa mpango wa pamoja kati ya Polisi na watekaji nyara hao???

Jeshi la Polisi na Serikali ya Magufuli watuambie hizi njama za kuipakazia CHADEMA na matukio haya zina lengo gani hasa???

Haya yote ni maswali muhimu. Majibu yake sahihi yanaweza kutoa mwanga wa matukio mengine ya kihalifu kama ya mauaji ya raia na ya kisiasa, utekaji nyara na kupotezwa kwa wanaharakati wa kisiasa, waandishi habari na wasanii, pamoja na mashambulio ambayo Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi wameyanyamazia kimya hadi sasa.

Hukumu ya Abdul Nondo inatupa fursa ya sio tu kujua kilichomtokea yeye binafsi, bali pia kudai na kupatiwa majibu sahihi ya matukio mengine ya aina hii ambayo hayajapewa majibu sahihi na ya kuridhisha na Jeshi la Polisi na Serikali ya Magufuli.

Tusikubali yaishe kirahisi kwa sababu tu Abdul Nondo ameshinda mtihani huu wa shetani. Tukikubali yaishe tujue kwamba yatarudiwa tena, pengine yakiwa na matokeo mabaya zaidi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Serikali kupokea ndege ya 14 ya ATCL, safari kuongezeka

Spread the love  SERIKALI ya Tanzania, kesho tarehe 3 Oktoba 2023, inatarajia...

Habari MchanganyikoTangulizi

Mobhare Matinyi Msemaji mpya wa Serikali

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua aliyekuwa Mkuu wa...

Habari MchanganyikoTangulizi

Basi la Magereza lagonga treni yenye abiria 650 Dar

Spread the loveBasi  Jeshi la Magereza lenye namba MT 0040 limegonga treni...

Habari MchanganyikoTangulizi

Afya ya akili yatajwa chanzo kuvunjika ndoa

Spread the loveCHANGAMOTO ya afya ya akili, imetajwa kuwa chanzo cha migogoro...

error: Content is protected !!