November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi ndogo ya Mbowe yaanza, Jamhuri kutumia mashahidi sita na vielelezo 4

Spread the love

 

KESI ndogo ndani ya kesi ya msingi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, imeanza kusikilizwa, Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu, Mawasiliano jijini Dar es Salaam. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kesi hiyo  ndogo imeanza kusikilizwa mahakamani hapo mbele ya Jaji Joackim Tiganga, leo Jumatano, tarehe 10 Novemba 2021.

Kesi hiyo inatokana na mapingamizi ya upande wa utetezi dhidi ya maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Mohammed Abdillah Ling’wenya, wakiiomba mahakama hiyo isiyapokee kwa madai kuwa si halali kisheria.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, ameieleza mahakama hiyo kuwa wanapanga kuita mashahidi  sita na vielelezo vinne.

Wakili Kidando ameileza mahakama hiyo kuwa, leo wana shahidi mmoja ambaye ameanza kutoa ushahidi wake, mahakamani hapo.

Shahidi huyo ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wilayani Arumeru, SP Jumanne Malangahe, ameanza kutoa ushahidi wake akiongozwa na Wakili Kidando.

Mapingamizi hayo yaliibuka baada ya shahidi wa nane wa jamhuri, Jumanne Malangahe, kuiomba mahakama hiyo iipokee nyaraka ya maelezo hayo, kama sehemu ya ushahidi wa upande wa mashtaka.

Katika hoja za upande wa utetezi, walidai  Ling’wenya hakuwahi kuchukuliwa maelezo hayo, kama ilivyodaiwa na SP Jumanne, kwamba aliyachukua baada ya kumhoji tarehe 7 Agosti 2020, Katika Kituo cha Polisi cha Kati Dar es Salaam.

Mawakili wa utetezi walidai kuwa, Ling’wenya alilalizimishwa kusaini nyaraka ya maelezo hayo kwa kupewa mateso ya kisaikolojia. Na kwamba hakuisoma kujua kilichomo ndani yake.

Sehemu ya mahojiano ya ushahidi anaoendelea kuutoa yapo hivi;

Jaji: Shahidi jina lako?

Shahidi: Superitendent Jumanne Malangahe.

Jaji: Umri?

Shahidi: Miaka 46.

Jaji: Dini.

Jaji: (Kiapo)

Shahidi: Muislamu. Shahidi Wallah wabillah watallah. Nathibitisha ushahidi nitaotoa utakuwa ni kweli na ukweli mtupu, Eeeh Mwenyezi Mungu nisaidie.

Wakili wa Serikali: Umesema wewe ni askari Polisi. Je, shughuli zako unazifanyia wapi kwa sasa?

Shahidi: Wilayani Arumeru Mkoani Arusha.

Wakili wa Serikali: Una nafasi gani hapo Wilayani Arumeru?

Shahidi: Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru.

Wakili wa Serikali: Majukumu yako ni yapi?

Shahidi: Kuzuia uhalifu. Kukamata watuhumiwa, kuwapekua watuhumiwa, kuwaongoza askari walio chini yangu kasika shughuli ya upelelezi.

Wakili wa Serikali: Kuna mtu mmoja anaitwa Mohammed Abdilah Ling’wenya. Elezea Mahakamani kama unamfahamu mtu huyu.

Shahidi: Namfahamu.

Wakili wa Serikali: Tangu lini?

Shahidi: Tarehe 5 Agosti 2020.

Wakili wa Serikali: Ilikuwaje mpaka ukamfahamu?

Shahidi: Baada ya kumkamata pale Rau Madukani.

Wakili wa Serikali: Ilikuwaje ukamakamata?

Shahidi: Baada ya kuwapo kwa taarifa kwamba anajihusisha kula njama za kutenda vitendo vya kigaidi.

Wakili wa Serikali: Vitendo gani vya kigaidi alivyokuwa anajihusisha navyo?

Shahidi: Kulipua vituo vya mafuta, kuchoma moto maeneo yenye mkusanyiko kama vile masoko , kukata miti na kuweka barabarani, ikwemo na kuwadhuru viongozi wa Serikali, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Ole Sabaya.

Wakili wa Serikali: Elezea hapa Mahakamani vitendo hivi vilikusudiwa kufanyikaje au kukusudiwa kufanyika wapi?

Shahidi: vilikusudiwa Kufanyika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Mbeya na Mwanza.

Wakili wa Serikali: Dhumuni lilikuwa ni nini?

Shahidi: Kuleta hofu au kuwaogofya wananchi na kuonyesha kwamba nchi haitawaliki.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taari mbalimbali

error: Content is protected !!