KESI ya kupinga mkataba wa kiserikali wa ushirikiano juu ya uendeshaji bandari nchini, ulioingiwa kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai, inaanza kusikilizwa leo Jumatatu, tarehe 3 Julai 2023, kwenye Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya…(endelea).
Kesi hiyo Na. 5/2023, imepangwa kusikilizwa mahakamani hapo mbele ya majaji, Mustafa Ismaili Kambona, Dunstun Ndunguru na Abdi Kagomba.
Tayari wafungua kesi hiyo, akiwemo Alphonce Lusako wameshawasili katika viwanja vya mahakama kwa ajili ya usikilizaji. Wanawakilishwa na mawakili, Boniface Mwabukusi na Phillip Mwakilima.
Mbali na Lusako, wengine waliofungua kesi hiyo ni, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalus. Wamefungua kesi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Bunge.
Waleta maombi hao wakipinga mkataba huo unaotarajiwa kutekelezwa na Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Serikali ya Dubai kwa kutumia Kampuni ya DP World, kwa madai kwamba kuna baadhi ya vipengele vyake vinakiuka katiba ya nchi.
Katika madai mengine, wanadai mkataba huo wa kimataifa umepelekwa bungeni kwa ajili ya kupitishwa bila kushirikisha umma na kutoa nafasi ya kutosha kwa wananchi kutoa maoni yao kinyjme cha Sheria ya Rasilimali za Taifa No. 5 ya 2017, kifungu cha 11 (1) na (2).
Kesi hiyo imefunguliwa katika kipindi ambacho kuna mjadala kuhusu suala hilo, ambapo baadhi ya wananchi wameiomba Serikali iuboreshe mkataba huo ili ulinde maslahi ya taifa, huku wengine wakishauri hatua za kisheria zichukuliwe kwa ajili ya kuusitisha.
Hivi karibuni, mwanasheria maarufu nchini, Prof. Issa Shviji, alidai njia pekee ya kuzuia mkataba huo ni kwenda mahakani kuupinga, au kulishinikiza Bunge kufuta azimio la kuuridhia utekelezwaji wake.
Leave a comment