December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kesi kupinga kufukuzwa Chadema: Kina Mdee kuendelea kuhojiwa mahakakani

Spread the love

 

HAWA Mwaifunga, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chama Cha Chadema (BAWACHA), Leo Alhamisi, tarehe 3 Novemba 2022, anaendelea kuhojiwa katika Mahakama Kuu,Masjala Kuu, jijini Dar es Salaam na mawakili wa chama hicho, dhidi ya malalamiko yake ya kufukuzwa kinyume cha Sheria. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ni katika kesi Na. 36/2022, iliyofunguliwa na wabunge viti maalum 19, wakiongozwa na Halima Mdee, katika mahakama hiyo, kupinga mchakato uliotumika kuwavua uanachama wa Chadema kwa tuhuma za usaliti, wakidai haukuwa halali hivyo wanaiomba mahakama ifanye mapitio dhidi yake ili kubaini ukweli.

Hawa anaendelea kuulizwa maswali ya dodoso na Wakili wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema (mjibu maombi namba moja), Peter Kibatala, mahakamani hapo mbele ya Jaji Cyprian Mkeha.

Mbunge huyo viti maalum, alianza kuhojiwa na Wakili Kibatala, tarehe 13 Oktoba 2022 na kutakiwa kuendelea kuhojiwa tena tarehe 21 Oktoba mwaka huu, lakini mahakama iliahirisha kesi hiyo baada ya kudai ana matatizo ya mgongo.

Miongoni mwa maswali ambayo Wakili Kibatala alimuuliza, ni kuhusu madai yake ya kupewa adhabu ya kuvuliwa uanachama bila kupewa nafasi ya kusikilizwa, ambapo wakili huyo alimhoji kama anafahamu aliyekuwa mwanachama wa Chadema, Zitto Kabwe (Kiongozi wa ACT-Wazalendo), kuwa alifukuzwa na Kamati Kuu ya chama hicho bila ya kushiriki kikao, ambapo alijibu anafahamu.

Wakati anahojiwa na Wakili Kibatala, Hawa alidai kikao Cha Kamati Kuu ya Chadema kilichomvua uanachama, baadhi ya wajumbe walikuwa si halali akiwemo Shaban Othumani.

Wakili wa Chadema, wakiongozwa na Peter Kibatala (katikati) wakiwa mahakamani

Pia, Hawa alidai alishirikiana na wenzake 18, kufungua kesi hiyo kupinga kufukuzwa Chadema, kwa kuwa hakusikilizwa na pia walituhumiwa kujiapisha kuwa wabunge viti maalum, Kwa kushirikiana na mfumo.

Hawa alidai, hakusikilizwa mbele ya kikao Cha Kamati Kuu ya Chadema, kilichofanyika tarehe 27 Novemba 2020, Kwa kuwa aliomba apatiwe muda wa kupitia hoja zake kwa ajili ya kuzijibu.

Hawa pamoja na wabunge wengine, walifukuzwa Chadema 2020 Kwa tuhuma za kujipeleka bungeni kinyume Cha msimamo wa chama hicho, wa kutopeleka wawakilishi katika mhimili huo kikipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu.

Hata hivyo, Grace Tendega, aliyekuwa Katibu Mkuu wa BAWACHA, wakati akihojiwa na Wakili Kibatala mahakanani hapo, alidai Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alishiriki mchakato wa uteuzi wa wabunge viti maalum na kuwasilisha majina yake 10, akitaka yasiachwe katika uteuzi.

Mara Kwa mara Viongozi wa Chadema, akiwemo Mnyika kupitia vyombo vya habari, walikanusha madai ya kuhusika na uteuzi huo, huku katibu mkuu huyo wa Chadema, akidai hakuwahi wasilisha majina Yao katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mbali na Grace na Hawa, wabunge wengine ambao mawakili wa Chadema wameomba wawahoji mahakamanj hapo Kwa ajili ya ushahidi, ni Ester Bulaya, Esther Matiko, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Cecilia Pareso na Halima Mdee.

error: Content is protected !!