July 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi Bavicha kuendeshwa kwa mwezi mmoja

Spread the love

HAKIMU Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, James Karayemaha amesema, kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), itamalizika ndani ya mwezi mmoja, anaandika Dany Tibason.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Patrobas Katambi, Mwenyekiti wa Taifa; Julius Mwita, Katibu na George Tito, Mwenyekiti wa Mkoa wa Mbeya.

Akizungumza mara baada ya Wakili wa Serikali, Lina Magoma kutamka kuwa, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika Karayemaha amesema, mara baada ya kusomwa kwa mashtaka ya awali na iwapo wataonekana kuwa na mashtaka ya kujibu, atapanga utaratibu utakaowezesha kesi hiyo kukamilika ndani ya mwezi
mmoja.

“Wakisoma mashtaka ya awali na kama itaonekana washtakiwa wanashtaka la kujibu, tutaiendesha kesi hii ndani ya mwezi mmoja iwe imekamilika,” amesema.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 16 Agosti mwaka huu washtakiwa hao watakaposomewa maelezo ya awali na dhamana zao bado zinaendelea.
Washtakiwa hao wanashtakiwa kwa tuhuma za kukutwa na maandishi ya uchochezi kinyume na kifungu cha 32 (2) cha Sheria ya Magazeti sura namba 229 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Washtakiwa hao wanadaiwa tarehe 8 Julai mwaka huu walikutwa katika Baa ya Captown, Dodoma wakiwa na fulana zilizoandikwa lugha ya uchochozi.

Maneno  yaliyoandikwa katika fulana hizo yanatajwa kuwa ni  Mwalimu Nyerere: Demokrasia inanyongwa na Dikteta Uchwara.

Washtakiwa hao wanatetewa na mawakili Fred Kalonga na John Chigongo.

 

error: Content is protected !!