December 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kesi 107 za ukatili wa kijinsia zapokelewa TAMWA

Spread the love

MRATIBU wa Kituo cha Usuluhishi (CRC) kilichoko ndani ya Chama  cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Gladness Munuo, amesema kwa mwaka 2014, kituo kimepokea kesi 107 za vitendo vya ukatili wa kijinsia vilivyosababishwa na ulevi wa pombe kupindukia. Anaandika Mwandishi Wetu … (endele).

Amesema kati ya kesi hizo, wanawake walikuwa 80, wanaume 22 na watoto walikuwa ni watano. 

Munuo ametoa takwimu hizo leo katika mkutano wa TAMWA na wahariri wa vyombo vya habari mbalimbali, kujadili mikakati kwa kutumia vyombo hivyo ili kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyosababishwa na unywaji pombe kupindukia. 

Mkutano huo umejadili njia zitakazotumika kwa jamii ili kuweka uelewa wa madhara ya unywaji pombe kupindukia kwani unachangia ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto na kurudisha maendeleo nyuma.

Katika mkutano huo; wahariri walijadili mbinu jinsi ya kukuza uelewa wa jamii juu ya madhara ya unywaji pombe kutokana na kuwa baadhi ya wanaume wamekuwa wakitelekeza familia zao na kuacha wanawake wakihangaika na watoto.

Munuo amesema vyombo vya habari vikitumika katika kutoa elimu ya madhara ya unywaji pombe hasa kwa ukatili ambao umekuwa ukifanywa kimya kimya vinaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo ndani ya jamii.

Ameutaja ukatili unaofanywa kimya kimya kuwa ni wa kingono, ubakaji na vipigo ambao unafanyika ndani ya familia huku idadi ya wanawake na watoto kutelekezwa ikiendelea kuongezeka.

Kwa mujibu wa Munuo, baadhi ya wanandoa wamekuwa wakitumia kilevi kupindukia na kusababisha wengine kushindwa kuwahudumia watoto wao ki – afya, kukosa chakula na mahitaji mengine kama ada za shule hali ambayo husababisha taifa kupoteza nguvu kazi.

error: Content is protected !!