RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema, wafanyabiashara kutoka Tanzania wako huru kuwekeza nchini humo pasina vikwazo ikiwemo visa au vibali vya kazi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Amesema, wafanyabiashara wa Tanzania wakifika Kenya, watafuata sheria na kanuni pekee ili kufanya biashara.
Rais Kenyatta ametoa kauli hiyo leo Jumatano, tarehe 5 Mei 2021, wakati akizungumza katika Jukwaa la Wafanyabiashara wa Kenya na Tanzania, lililofanyika jijini Naironi.
Jukwaa hilo, limehudhuriwa na wafanyabishara kutoka nchi hizo mbili akiwemo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye leo Jumatano, anahitimisha ziara yake ya siku mbili aliyoianza jana Jumanne.
“Wananchi wetu wa Kenya na Tanzania, wakijiona kama ni ndugu kwa kushirikiana badala ya kushindana, tutafanikiwa na hatuna haja ya kushindana.
“Tukijiona kama nchi ambazo zinashindana, hatutaweza kupata wawekezaji wakubwa kuja kuweka viwanda katika nchi zetu na Afrika Mashariki,” amesema.
Rais Kenyatta amesema, Tanzania na Kenya zinapaswa kusaidiana ili kukuza uchumi na fursa za wananchi wa mataifa hayo mawili yaliyomo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Tukishirikiana kati ya Kenya na Tanzania, tutakuwa washindi kwa Pamoja. Tungependa kuona wawekezaji wengi wa Tanzania wanakuja kuwekeza Kenya.
“Wawekezaji wa Tanzania, mko na uhuru kuja kufanya biashara zenu hapa, bila vibali vya kazi, visa za biashara. Mfanyebiashara kama mnavyofanya Tanzania, haja tu mfuate sheria na kanuni zilizowekwa,” amesema.

Pia, amewataka mawaziri wa Kenya na Tanzania, kuweka utamaduni wa kukutana mara kwa mara kujadiliana changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
“Tunawataka mawaziri, mtoke ofisini mtatue changamoto hizo, msaidie wananchi na itasaidia kukuza uchumi na kodi,” amesema na kuongeza;
“Nakuahidi (Rais Samia) kuwa awamu yako ya uongozi wa Tanzania, utaona uhusiano wetu ukipanda juu juu zaidi na tutatembea kwa Pamoja.”
Leave a comment