Wednesday , 8 February 2023
Home Kitengo Habari Kimataifa Kenyatta ajipanga kujitetea kashfa bilioni 70
Kimataifa

Kenyatta ajipanga kujitetea kashfa bilioni 70

Rais Uhuru Kenyata
Spread the love

 

BAADA ya Panama Papers mwaka 2016, Paradise Papers mwaka 2017, Mauritius Leaks mwaka 2019 na Luanda Leaks mwaka 2020, hatimaye Jumuiya ya Kimataifa ya Wanahabari wa Upelelezi (ICIJ) imebainisha kuwa viongozi 43 wa Afrika akiwamo Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta wanamiliki kampuni au akaunti za benki za nje kukwepa kulipa kodi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hatua hiyo imekuja baada ya Nyaraka za Pandora au Pandora Papers zilizofanyiwa uchunguzi na timu hiyo ya waandishi wa habari 600 kutoka vituo 150 vya habari duniani kugundua kuwa watu mashuhuri wapatao 336 duniani wanamiliki akaunti kama hizo za siri za nje ya nchi zao.

Aidha, Rais Kenyatta ambaye alichaguliwa mwaka 2013, pamoja na mambo mengine ametajwa katika uchunguzi huo licha ya kuahidi kupambana na ufisadi nchini humo

Nyaraka za siri kwenye bandari kuhusu ushuru zilizopatikana na kukaguliwa na ICIJ, zinaonyesha jinsi yeye na familia yake hutumia kwa siri kampuni za nje kwa kuficha kiwango cha utajiri wao na kukwepa mamlaka ya ushuru.

Uwekezaji wa pwani wa familia hiyo pamoja na kampuni iliyo na hisa na dhamana zenye thamani ya dola za Marekani milioni 30 sawa na Sh bilioni 70, ziligunduliwa kati ya mamia ya maelfu ya kurasa za makaratasi ya kiutawala kutoka kwenye kumbukumbu za kampuni 14 za sheria na watoa huduma huko Panama na Visiwa vya Virgin vya Uingereza ( BVI) na sehemu nyingine zinazotoza kiasi cha chini cha ushuru au zisizotoza ushuru kabisa.

Mali hizo za siri zilifichuliwa na uchunguzi, uliochapishwa mapema Jumapili tarehe 3 Oktoba mwaka huu na ICIJ, Finance Uncovered, Africa Uncensored na mashirika mengine ya habari.

Nyaraka zinaonyesha kwamba wakfu ulioitwa ‘Varies’ ulianzishwa mwaka 2003 huko Panama, ukimtaja mama yake Kenyatta, Ngina (88), kama mnufaika wa kwanza – na kiongozi huyo wa Kenya kama mnufaika wa pili ambaye angeurithi baada ya kifo chake. Madhumuni ya wakfu huo na thamani ya mali yake haijulikani.

Hata hivyo, Rais Kenyatta amesema kwamba ufichuzi wa nakala za ‘Pandora papers’ utaimarisha uwazi wa umiliki wa fedha unaohitajika nchini Kenya na duniani kwa jumla.

Kwa mujibu wa BBC, Kenyatta amesema kwamba usafirishaji wa fedha, mapato yaliyopatikana kwa njia za uhalifu na ufisadi, ulifanyika katika mazingira ya siri na giza.

Ameongezea kwamba kitakachofuatia baada ya ufichuzi wa nakala hizo za Pandora na ukaguzi, utaondoa usiri na giza kwa wale ambao hawawezi kuelezea mali na utajiri wao.

Pamoja na mambo mengine Rais Kenyatta ambaye yuko nje ya nchi ameahidi kutoa taarifa kamili atakaporejea nchini humo.

Katika uchunguzi huo ni kwamba jumla ya wanasiasa 43 kati ya 336 wanatoka Afrika. 10 kati yao wanatoka Nigeria, tisa wanatoka Angola, watano wanatoka Ivory Coast. Wengine wanatoka nchi za Chad, Gabon, Congo-Brazzaville.

Viongozi wa nchi nyingi zilizotajwa katika uchunguzi huo zina rasilimali kubwa ya mafuta.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Kimataifa

Raia Pakistan walilia haki siku ya Mshikamano Kashimir

Spread the loveRAIA wa Pakistani waishio nchini Tanzania wameadhimisha siku ya Mshikamano...

Kimataifa

Ramaphosa akiri tatizo la umeme Afrika Kusini kuathiri sekta ya madini

Spread the love  RAIS wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema tatizo la...

Kimataifa

Idadi ya vifo tetemeko la ardhi yafikia 9000

Spread the love  IDADI ya vifo vilivyotokana na tetemeko la ardhi lililotokea...

Kimataifa

Tetemeko la ardhi Uturuki: Vifo vyaongezeka hadi 4,800

Spread the love  Idadi ya vifo vilivyotokana na tetemeko lililotokea jana Jumatatu...

error: Content is protected !!