MARA baada ya kocha Cedric Kaze kutimuliwa Yanga uongozi wa klabu hiyo umemrejesha aliyekuwa kocha wao msaidizi, Juma Mwambusi kuifundisha timu hiyo kwa muda, wakati wakitafuta kocha mkuu. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea) .
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Dk. Mshindo Msolla amesema Mwambusi aliyekuwa mgonjwa kwa sasa amepona, hivyo ataifundisha timu hiyo wakati uongozi ukiwa kwenye mchakato wa kumpata kocha mkuu.
Dk. Msolla amesema klabu ya Yanga ilimsaidia kupata matibabu wakati anaumwa na kwa sasa atakuwa na timu, hawana wasiwasi kwani alikuwa na wachezaji wakati tunaanza ligi, hivyo sio mgeni.
“Kurudi kwake siyo jambo geni, sababu tulikuwa nae wakati Ligi inaanza na hata mapinduzi tulikuwa nae na kwa sasa ataichukua timu hiyo kwa muda wakati tunatafuta mwalimu mkuu kwa kuwa aliondoka vizuri,” alisema Mwenyekiti huyo.

Aidha Msolla ameendelea kusema kuwa suala la kocha mpya lipo kwenye mchakato na wasifu wa kila kocha utaenda kwenye kamati ya ufundi na kuona yupi anafaa kwa sasa.
“Tunaendelea na taratibu za kawaida, na wasifu wa kila kocha utaenda kwenye kamati ya ufundi na wataweka kila kitu ubaoni kujua ni yupi anafaa kwa sasa,” alisema Dk. Msolla
MwanaHALISI Online ilimtafuta kocha huyo ili kusikia neno kutoka kwake, baada ya kurejea tena kwenye viunga vya jangwani lakini simu yake iliita bila majibu.
Mwambusi aliachia ngazi ndani ya klabu hiyo tarehe 21 Januri 2021, baada ya kutoka michuano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar akiwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Cedric Kaze waliotwaa taji hilo.
Hii ni mara ya tatu kwa kocha huyo kurejea Yanga toka alipojiunga kwa timu hiyo mara ya kwanza chini ya Hans van Plujim aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hiko na kisha kurejea tena wakati msimu wa huu wa 2020/21 unaanza na kisha kujiweka pembeni kwa matatizo ya kiafya.
Leave a comment