January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kaya 483 zafanikisha mradi wa mazingira

Spread the love

KAYA 483 za kijiji cha Mazengo kata ya Mvumi Makulu wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma kupitia mradi wa usafi na mazingira Tanzania (Umata) zimefanikisha uboreshaji wa mazingira katika ujenzi wa vyoo bora vya kisasa ikiwemo na vifaa vya kunawia mikono baada ya kutoka chooni. Anaandika Dany Tibason, Chamwino … (endelea).

Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya hiyo, Farida Mgomi alipokuwa anazungumza na wananchi katika sherehe ya kufikia ubora wa usafi wa mazingira.

Mgomi amesema takwimu zinaonyesha kuwa kijiji hicho kilianza kutekeleza mradi huo mwaka jana kikiwa na kaya zenye vyoo 387 na ambazo hazikuwa na vyoo kaya 96 lakini kwa sasa zote zimefanikiwa kuwa na vyoo bora vya kisasa.

Amesema mbali na vyoo kijiji hicho kimeweza kufanikisha uchimbaji wa mashimo ya taka, vichanja vya kuanikia vyombo pamoja na vifaa vya kunawia mikono baada ya kutoka chooni.

“Nyie mmekuwa wa kwanza kwenye wilaya kufikia kiwango hicho cha mafanikio, rai yangu kwenu ni kwamba msibweteke kwa mafanikio hayo kwani kiwango hicho hakitoshi, leo mmepata cheti cha daraja la pili na mnatakiwa mpate daraja la kwanza,” amesema.

Aidha aliwataka wanakijiji hao watambue kuwa Serikali wanathamini juhudi na mchango wao mkubwa kwenye usafi na kuwataka waendelee na moyo huo hasa kwenye maeneo ambayo elimu ya mazingira haijafika.

Kwa upande wake mtaalamu wa ufatiliaji na tathimini mradi wa usafi wa mazingira (Umata) Joyce Masile alipokuwa akisoma risala amesema mradi huu unaendelea kutekelezwa kwa kuhakikisha kijiji hicho kinafikia hatua ya kwanza.

Hata hivyo amesema kampeni hii pia inaendelezwa katika vijiji vingine wilaya ya Chamwino ili kufikia lengo hilo ikiwa pamoja na kuisaidia jamii kuunda vikundi vya kuweka na kukopa vitakavyosaidia kipato na kuweza kuboresha hali ya afya kwa kuweka mazingira na vyoo katika hali nzuri.

Mradi huu ulibuniwa na kundi la wadau wa sekta ya usafi wa mazingira linaloongozwa na serikali kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii na unatekelezwa na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo ni Ongawa, Codert, SAWA, CRS, PDF, Mamado na Sedit yakiongozwa na Plan International kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya ya Bahi, Chamwino na Kongwa.

error: Content is protected !!