September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kaya 3,800 kushiriki utafiti utalii wa ndani

Spread the love

 

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro amezindua rasmi utafiti wa utalii wa ndani na mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19. Anaripoti Danson Kaijage – Dodoma … (endelea)

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) jana tarehe 15 Januari, 2022 Dk. Ndumbaro amesema kaya zaidi ya 3,800 zinaenda kufikiwa katika utafiti huo.

“Mpango tunaozindua ni mpango muhimu kuhusiana na utalii wa ndani, jambo hili halijawahi kufanyika toka tumepata uhuru, hakika ugonjwa wa UVIKO 19 umetoa darasa kwetu.

Aidha, Dk. Ndumbaro amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mgawo wa zaidi ya bilioni 90 ilikusaidia wizara hiyo katika sekta ya utalii na maliasili kukabiliana na UVIKO – 19.

“Mimi binafsi, Naibu waziri na katibu mkuuu na Naibu Katibu tumemfurahisha hivyo, ameona tuendelee kuiongoza wizara hii ili kumalizia jambo lililobakia  tunamuahidi hatutamuangusha, tutafanya kazi kwa bidii zaidi,’’ amesema.

Aidha, amekipongeza OUT kwa kukubali kufanya kazi hiyo ya utafiti hasa ikizingatiwa wana uwezo na ubobezi wa kutosha katika idara ya utalii.

“Chuo hiki ni cha watanzania waliobobea utaalaam, kitatoa wakusanya data zaidi ya 600 na watalaam wengine jumla watafika 700 ambao wataenda kuguswa na uwezeshwaji wa utafiti huu, haya yote ni jitihada za Mama Samia,” amesema.

Hata hivyo, Dk. Ndumbaro alibainisha kuwa, mwaka 2020-2021 Wizara hiyo imefanikiwa kuongeza kiwango cha watalii nchini.

“Mwaka 2021 tulipata watalii wa ndani 700,000 na watalii wa nje ni  900,000, hili ni ongezeko kubwa na hata Shirika la Utalii Duniani limetupongeza kwa hatua hii kubwa licha ya changamoto ya UVIKO,” amesema.

 Aidha, ametoa wito kwa OUT kuzingatia fursa hiyo kwani ni utafiti ambao unaenda kutoa takwimu sahihi na ushauri wa kitaalaam katika kukuza sekta ya utalii nchini.

Pia ameziomba taasisi zote zitakazoshiriki  katika utafiti huo, kuhakikisha asilimia kubwa ya washiriki wawe ni vijana kwani ndio watakaodumu kwa muda mrefu katika masuala ya utalii.

Ameongeza kuwa utafiti huo utasaidia kutengeneza dira nyingine ya miaka mitano ya wizara na kitaifa kupitia utalii.

Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema utafiti huo utatoa dira ya mwenendo wa utalii wa ndani

.“Utalii wa ndani ni eneo pana sana ambalo tuliliacha nyuma kwa hivyo leo tunaenda kuzindua utafiti huu kwa lengo la kujua tulipotoka, tulipo na tunapoenda ili utalii wa ndani ukue”

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma Mkomi amesema utafiti huo utawezesha sio tu kupatikana kwa takwimu sahihi bali utatoa fursa ya kujua pengo lililopo kati ya utalii wa ndani na wa nje

“Serikali imefikia uamuzi wa kufanya utafiti huo kwa sababu sekta ya utalii imekuwa ikichangia katika uchumi wa nchi zaidi ya Shilingi trilioni 6.06 na kuzalisha ajira takriban milioni 1.5 (za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja).

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Profesa Deus Ndaruko  amesema mradi huo unaotarajia kuanza hivi karibuni na utakuwa wa miezi minne.

“Tunashukuru Wizara ya Maliasili kwa ushirikiano huu na tunaahidi kuzitumia vizuri fedha na watanzania wataiona wizara wakitembea katika maeneo yao mbalimbali,” amesema Prof. Ndaruko.

error: Content is protected !!