April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kauli ya Membe baada ya kuhojiwa

Bernard Membe, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Tanzania

Spread the love

BERNARD Membe, waziri wa zamani wa Mambo ya Nje amesema, mahojiano yake na Kamati ya Kamati ya Maadili na Usalama ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), yamempa furaha ya ajabu. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma…(endelea).

Amesema, safari yake ya kwenda Dodoma na kukutana na kamati hiyo iliyomuhoji kwa saa tano, ina manufaa makubwa kwake, kwa chama chake na taifa.

“…nimekuwa mtu wa furaha kubwa ajabu,” amesema Membe huku akitoa tabasabu “…lakini niwaambie tu, safari hii ya kuja Dodoma ilikuwa ni ya manufaa makubwa sana sana sana, kwangu kwa chama na kwa taifa letu.”

Waandishi wa habari walimtaka kueleza mwenendo wa mahojiano na hatima yake, hata hivyo hakuwa tayari kueleza kilichojiri na badala yake amesema “mambo mengine yatakuja kidogo kidogo.”

Akizungumzia mazungumzo yalivyokuwa, Membe amesifia namna mijadala ilivyoendeshwa na kamati hiyo iliyoongozwa na Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM wakati akihojiwa.

“Mijadala ilikuwa mizuri, mikubwa na ya kitaifa inayohusu chama chetu cha mapinduzi, inayohusu nchi yetu. Nimepata nafasi nzuri ya kujadili masuala ya kitaifa na ya kimataifa, nimepata nafasi nzuri ya kufafanua mambo kadhaa ambayo chama changu walitaka kuyajua,” amesema.

Membe alifika kwenye ofisi ya chama hicho ambapo ndio Makao Makuu ya CCM, jijini Dodoma maarufu kama ‘White House’ SAA 3:20.

Tarehe 13 Desemba 2019, Halmashauri Kuu ya chama hicho iliiagiza kamati ya maadili ya chama hicho, kuwahoji Membe na makatibu wakuu wastaafu – Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba –  kwa kile kilichoelezwa, utovu wa maadili.

error: Content is protected !!