December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kauli ya JPM ilivyobadili upepo Coco Beach

Rais John Magufuli

Spread the love

KAULI ya Rais John Magufuli kwamba mradi wa kuendeleza ufukwe wa Coco Beach, jijini Dar es Salaam hauna tija, imewafariji wafanyabiashara wa eneo hilo. Anaripoti Martin Kamote… (endelea).

Wafanyabiashara hao walikuwa wakihesabu siku za kufungasha virago. Ni baada ya kupewa notisi ya siku 45 kuhakikisha wanaondoka kwenye eneo hilo kupisha ulioitwa ‘mradi wa kimkakati’ wa kuendeleza ufukwe huo.

Wanasema, ni kweli kuwa eneo hilo linatosha kubaki kama lilivyo na kwamba, kauli ya Rais Magufuli imezingatia uhalisia na kuzuia ujanja ujanja uliokuwa umepangwa kufanywa na waliopewa mamlaka.

 Tarehe 22 Septemba 2019, Rais Magufuli wakati akizungumza na watendaji mbalimbali wa serikali mara baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua,  alisema kuwa ujenzi huo, unazua maswali mengi.

“Huu mradi una maswali mengi sana, mkandarasi mwenyewe ndiye aliyejenga soko la Mwanjelwa akashindwa, ana mradi mwingine tena hajakamilisha, anakwenda kupelekwa Coco Beach.

“… lakini kwa mujibu wa sheria ya mazingira, hauwezi ukajenga structure kubwa kwa mita 60 kutoka kwenye bahari au ziwa,” alisema Rais Magufuli.

Kiongozi huyo wa nchi alionesha kupingana na ujenzi huo kwa maana, eneo hilo lina wafanyabiashara wa muda mrefu ambao endapo wataondolewa, hakuna maelezo ya wapi waende kuendelea na biashara zao.

“…mradi wowote ambao una matokeo chanya kwa watu, ni lazima uwatafutie njia mbadala, kama unatengeneza barabara pia  unatengeneza mchepuko, hauwezi ukaifunga barabara lazima uwapeleke mahali ili ukimaliza, uwapeleke sehemu nyingine.

“Sasa mnakwenda mnawaaambia ondokeni hapa, wataishi vipi?, inaumiza tutapopewa madaraka na kuwasahau masikini, hauwezi ukajenga pale kwa bilioni 14 wakati kinachotakiwa ni kutengeneza vinjia, unaweka na vitu vya kukalia ili watu wawe wanakwenda pale kustarehe, unajenga li-structure la nini?” amehoji.

Akizungumza leo tarehe 25 septemba 2019 na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Uokoaji, Utunzaji wa Mazingira na Usalama katika eneo la Coco Beach, Ahmed Abdallah amesema, wote wanapenda maendeleo.

“Sisi wote ni wadau wa maendeleo na tunapenda maendeleo, lakini kwa taarifa ile ya rais eneo hili halifai kupita huo mradi, hapa ni white sands tunataka ufukwe ubaki kuwa ufukwe na sio kuweka zege kama wanavyotaka wao,” amesema.

Salum Mogi, Makamu Mwenyekiti wa Kikundi cha Uokoaji, Utunzaji Mazingira na Usalama katika fukwe hiyo amesema, Tanzania inajua fukwe hiyo imefungwa, hivyo ujumbe uwafikie kuwa ipo wazi na watu waendelee kwenda kuogelea kama zamani.

“Tumepata pigo kubwa sana tangu ilipotangazwa Coco Beach kuwa imefungwa, vijana wanaishi bila kufanya kazi na wanaondoka patupu, wanakaa tu hawapigi picha kwakuwa hakuna mtu anayeingia hapa, biashara karibu zote zimesimama,” amesema.

Mfanyabiashara wa Coco Beach, Alphonce Buhatwa ambaye tarehe 22 Septemba 2019 majengo yake aliyokuwa akiyatumia kwa biashara yaliungua moto, amesema kauli ya rais imempa faraja.

Hata hivyo, ameeleza kusikitishwa na tuhuma kwamba alichoma majengo yake ili alipwe bima ya moto kutokana na mgogoro wake na Manispaa ya Kinondoni.

“Nasikitika sana na mambo yanayoendelea mtandaoni kwamba tulichoma moto ili tulipwe bima, hapa hakuna bima na sijawahi kukata bima,” amesema.

error: Content is protected !!