October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Katibu Mkuu wa Chadema’ ajiunga CCM

Vicent Mashini, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema (kushoto) akiwa na Humphrey Polepole, Katibu wa Itibaki na Uenezi wa CCM muda mchache baada ya kumpokea mwanachama huyo mpya

Spread the love

ALIYEKUWA swahiba mkuu wa Freeman Mbowe, mwenyekiti wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vicenti Mashinji, ameondoka ndani ya chama hicho cha upinzani nchini Tanzania na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Dk. Mashinji alikuwa katibu mkuu wa Chadema, kuanzia Aprili mwaka 2016 hadi Desemba mwaka jana. Ametangaza kukihama chama hicho, leo Jumanne, tarehe 18 Februari 2020, jijini Dar es Salaam. Alipokelewa  na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi, Humprey Polepole.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dk. Mashinji alisema, ameamua kuondoka Chadema, kutokana na chama hicho, kuwa mali ya mtu binafsi.

“Chadema siyo taasisi ya umma, kama ambavyo baadhi ya watu wanavyofikiri,” ameeleza Dk. Mashinji na kuongeza, “ile ni kampuni binafsi ya Freeman Mbowe.”

Amesema, “nimeona tuache malumbano ya asubuhi na jioni. Nije Lumumba kuongea na wenzangu, ili nione ninawezaje kupata  fursa ya kujiunga na CCM kwa madhumuni ya kunilea na kunikuza. Ninahitaji kuendelea kutoa mchango wangu kwa maendeleo ya taifa langu.”

Amekituhumu chama chake hicho cha zamani, kwa kile alichoita, “kutoendana na itikadi yake.”

“Ukiangalia Chadema, utaona jinsi kinavyojitambulisha kuwa ni chama cha wahafidhina. Lakini ukweli ni kwamba hakiendani na dhana hiyo,” amesisitiza Dk. Mashinji na kuongeza,  “siyo tu Chadema hakina Itikadi, bali kina vitu vya hovyo sana.”

Amesema, “ndani ya Chadema, hakuna uwazi wa mapato na matumizi; hakuna uwazi kwenye madeni ya chama, hakuna uwazi kwenye ruzuku na mapato mengine yanayotoka serikalini; na ama wafadhili.”

Hata hivyo, Dk. Mashinji amekiri kuwa hakuna chama kisichokuwa na mapungufu kwa kuwa vinaongozwa na wanadamu, na kudai kwamba uamuzi wake wa kujiunga na CCM umetokana na chama hicho kuwa na uthubutu wa kusikiliza.

“Katika kukaa na kutafakari, nikaona Tanzania haiumbwi na malaika. Inaumbwa na binadamu. Nikaona wenzetu hawa CCM, angalau  wanasikiliza, wana utu na  ubidamu,” ameeleza Dk. Mashinji.

Akiwa hajulikani kabisa kwenye siasa za ndani ya Chadema, Dk. Mashinji aliibuka kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la taifa (BKT), uliofanyika jijini Mwanza, Aprili 2016, kufuatia Mbowe “kung’ang’aniza” wajumbe wa baraza, kuwa ndiye pendekezo lake katika nafasi ya katibu mkuu.

Taarifa zinasema, kabla ya jina la Mashinji kuletwa kwenye Baraza Kuu, baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu (CC), wakiongozwa na Tundu Lissu, walipinga pendekezo hilo la mwenyekiti.

Alikuwa ni Edward Lowassa, aliyekuwa mjumbe wa CC wakati huo, aliyemnusuru Mbowe kuaibika, baada ya kuwashawishi wakubaliane na matakwa ya Mbowe ili kukinusuru chama na mgawanyiko uliotokana na nafasi hiyo.

Aidha, nje ya Kamati Kuu, baadhi ya wabunge, wakiongozwa na mbunge mmoja wa Dar es Salaam (jina tunalihifadhi), walisimama kidete kupinga uteuzi wa Dk. Mashinji kwa maelezo kuwa hana rekodi ya harakati za Chadema na mtu ambaye historia yake haijulikani.

“Katika hili, muache Mbowe avune aibu. Huyu bwana hatukumfahamu. Jina lake alilichomoa mwenyewe mfukoni na kulileta baraza kuu,” ameeleza mjumbe mmoja wa CC ambaye kwa sasa ameomba jina lisitajwe.

Dk. Mashinji anakuwa kiongozi wa tatu mkubwa kuondoka Chadema katika kipindi cha wiki mbili. Wengine waliondoka, ni pamoja na aliyekuwa waziri mkuu mstaafu na Mjumbe wa CC, Fredrick Sumaye na aliyekuwa mbunge wa Ndanda, Cecil David Mwambe.

error: Content is protected !!