July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Katibu mkuu Bakwata Taifa amkana Kitundu

Spread the love

KATIBU  mkuu wa Bakwata Taifa, Seleman Lolila amemkana Meneja wa shule za El-Hijra, Mashaka Kitundu, kwamba hausiki kwa jambo lolote la kumkingia kifua pale anapolalamikiwa na wafanyakazi. Anaandika Dany Tibasom, Dodoma … (endelea).

Lolila alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza kwa njia ya simu kwa lengo la kutoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya watumishi na walimu wa shule za sekondari za El-Hijra na Jamhuri kwa kutolipwa mishahara na stahiki zao kwa ujumla.

Lolila amesema hawezi kumkingia kifua Kitundu na wala hahusiki kwa jambo lolote.

“Mimi nipo Dar es Salaam, Kitundu ndiye anayelipa mishahara sasa mimi nitamkingiaje kifua mimi,” amesema Lolila.

Watumishi kwa nyakati tofauti wakizungumza kwa masharti ya kutokutajwa majina yao walisema Kitundu amekuwa akiwanyanyasa watumishi huku akitumia jina la katibu mkuu Bakwata Taifa.

Kutokana na hali hiyo watumishi na walimu wa shule ya sekondari ya El- Hijra  pamoja na sekondari ya Jamhuri  ambazo zinamilikiwa na Baraza Kuu la Waislam (BAKWATA) wamemuomba Mufti wa Tanzania, Shekhe Abubakari Zuberi kumsimamisha kazi Meneja wa shule hizo, Mashaka Kitundu na ikishindikana  wametishia kugoma.

Watumishi hao wamefikia hatua hiyo kwa madai kwamba hawana imani na mkuu wa shule ya sekondari ya Hijra na meneja wa shule ya Hijra na Jamhuri ambaye pia ni Kaimu katibu wa Bakwata mkoa, Mashaka Kitundu kutokana na manyanyaso wanayoyapata ikiwa ni pamoja na kutolipwa mishahara yao na stahiki nyingine.

Wakizungumzia adha yanayopata watumishi hao wamesema ni kutolipwa mishahara yao huku Meneja huyo akiendelea kujineemesha, kujenga nyumba ya kifahari na kununua magari.

Watumishi hao pamoja na walimu walisema kwamba kwa sasa wana hali mbaya kwani hawajalipwa mishahara yao na pale wanapodai wanapigwa kalenda.

“Tangu mwezi wa saba hadi mwezi huu hatujalipwa mishahara, mara tunalipwa sh.10,000 na wengine wanapewa sh.50,000 na hatujui ni za nini.

“Mbaya zaidi Meneja Kitundu ametugawa watumishi kuwa wale ambao amewafanya watu wake wa karibu huku wengine akiwa hataki hata kuwasikiliza,” amesema mmoja wa watumishi.

Wamesema tangu Kitundu awe meneja katika shule hizo  hali ya watumishi imekuwa mbaya lakini jambo la ajabu ni matumizi kuwa makubwa tofauti na kipindi cha nyuma.

“Hivi karibuni alitumia kiasi cha sh. 800,000 kwa wiki kulisha wanafunzi wa Bweni ambao ni kati ya 150 ambapo kawaida wanafunzi hao wa bweni utumia Sh. 450,000 kwa wiki,” walieleza.

Katika msisitizo  watumishi walimuomba Mufti wa Taifa, Abbakari Zuberi kumwondoa au kumsimamisha kazi ili uchunguzi ufanyike kubaini ubadhilifu alioufanya kwa muda mfupi tangu afike shuleni hapo.

Katika hatua nyingine watumishi hao wamesema Kitundu amekuwa akiwabeza watumishi kwa maelezo kuwa hakuna mtu wa kumfanya lolote kwani yeye anamahusiano makubwa na Katibu mkuu wa Bakwata Taifa, Seleman Lolila.

Hata hivyo watumishi na walimu wamesema baada ya kumbana meneja aliwapatia kiwango sawa wote laki moja kama sehemu ya kupunguza ukali wa maisha.

Kwa upande wake Meneja wa shule hizo alipoulizwa juu ya tuhuma hizo alisema suala la mishahara ni tatizo lakini amelazimika kukopa benki na kulipa mishahara.

“Watumishi na walimu walikuwa hawajalipwa mshahara kwa miezi mitatu lakini ni kutokana na ada kuchelewa hivyo nimelazimika kukopa fedha kwa ajili ya kulipa mishahara ya miezi mitatu”alisema Kitundu.

error: Content is protected !!