January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Katibu Mkuu AFP asimamishwa

Mkurugenzi-Habari na Uenezi Taifa, Mwaram Hazali (kushoto)

Spread the love

CHAMA cha Alliance for Tanzania Farmers (AFP), kimemsimamisha kwa muda usiojulikana Katibu Mkuu wake, Rashid Rai, kutokana na mapungufu makubwa ya kiutendaji yaliyosababisha chama kuzorota na kupoteza mvuto kwa wananchi wake. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi-Habari na Uenezi Taifa, Mwaram Hazali, amesema, kutokana na kikao cha Machi 13, 2015, chini ya Mwenyekiti wao, Said Soud, kilimsimamisha uongozi katibu huyo  kutokana na utendaji wake kuwa mbovu.

Amefafanua kuwa, kwa kipindi chote alichokuwa madarakani katibu huyo, amekuwa akikiuka maagizo yote anayopewa na mwenyekiti badala yake anafanya vitu ambavyo ni kinyume cha katika ya chama.

Hazali amesema, katibu huyo amesababisha vikao vingi kutofanyika kama inavyotakiwa, hivyo kuwakosesha wajumbe haki yao ya msingi ya kutoa mawazo yao juu ya maendeleo ya chama, haswa kwa kipindi hiki cha uchaguzi.

“Kisheria inabidi katibu huyo aitishe kikao kila baada ya miezi mitatu, ili kujadili mambo mbalimbali ya chama, lakini yeye tangu aingie madarakani ni mwaka sasa hajawahi kufanya hivyo, badala yake anajichukulia maamuzi yake na kuitisha vikao vyake ambavyo havijulikani na chama,” amesema Hazali.

Ameeleza kuwa kwa mujibu wa katiba ya chama ibara ya 19, kifungu cha 8 (d) na (f), hawawezi kumfukuza moja kwa moja ndani bali kamati kuu itaandaa tuhuma zake na kuzipeleka kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kwa uchunguzi zaidi ili kukinusuru chama.

Aidha, Hazali amesema nafasi ya ukatibu itashikwa na makamu mwenyekiti msaidizi, na hivyo shughuli za chama kuendelea kama kawaida, bila mapungufu yoyote.

Hata hivyo, Hazali amesema, chama bado kina nguvu ya kuendeleza mapambano ndani ya siasa wakiwa na lengo kuu la kukiondoa Chama Cha Mapinduzi madarakani.

“Niwape moyo wanachama wa AFP, kutokata tamaa, tunaweza kufika mbali tukiamua, kama mwaka 2010 tulishika nafasi ya 4 kati ya vyama 12, basi tunaweza,” amesema Hazali.

error: Content is protected !!