April 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Katibu Chadema auawa

Sweetbert Njewike, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida

Spread the love

ALEX Jonas, Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Manyoni Mashariki mkoani Singida, ameuawa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Singida … (endelea).

Taarifa zaidi zinaeleza, Jonas ameuawa usiku wa kuamkia jana tarehe 25 Februari 2020, na mpaka sasa watu waliofanya tukio hilo, hawajajulikana.

Sweetbert Njewike, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida akizungumza na MwanaHalisi Online kwa njia ya simu kuhusu mauaji hayo, amesema Jeshi la Polisi linayo taarifa hiyo na kwamba linafuatilia.

Kamanda Njewike amesema, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Manyoni (OCD), anafuatilia tukio hilo, na kwamba atatoa taarifa rasmi pindi ufuatiliaji huo utakapokamilika.

“Nimesikia kuna mtu ameuawa lakini sijajua kama ni katibu wa chadema, OCD Manyoni anafuatilia tutajua kama ni huyo. Taarifa rasmi tutatoa baadaye, nasubiri kwanza taarifa kutoka kwa OCD wa wilaya hiyo,” amesema Kamanda Njewike.

Kwa mujibu wa Chadema leo tarehe 26 Februari 2020, mwili wa Jonas ulikutwa eneo la Mwembeni Manyoni Mjini, ukiwa umekatwa na mapanga maeneo mbalimbali ya mwili hasa kichwani na mikononi.

Chama hicho kimesema, kinafuatilia kwa undani kuhusu tukio hilo, huku kikilaani mauaji hayo.

“Tumepata taarifa za kushtua na kusikitisha sana za mauaji ya katibu wa Chadema Manyoni Mashariki ndugu Alex Jonas yaliyotokea usiku wa kuamkia jana, Mwembeni Manyoni Mjini. Chama kinafuatilia kujua kilichotokea kisha tutatoa taarifa juu ya tukio hilo,” imeeleza taarifa ya Chadema.

error: Content is protected !!