July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Katiba ya Sitta mgogoro mtupu

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Ali Mohamed Shein akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya KIbanda Maiti, Zanzibar

Spread the love

KATIBA Mpya Inayopendekezwa haiwezi kupenya kura ya maoni Visiwani Zanzibar, MAWIO limeelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM); Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano zinasema, hofu ya kutopita katiba iliyopendekezwa, tayari imewakumba baadhi ya viongozi wakuu katika chama na serikali.

“Katiba hii haiwezi kupita Zanzibar. Kule hakuna anayelitaka andishi hili. Itakwama kwenye kura ya maoni Visiwani kwa kuwa imepora mamlaka muhimu ya Zanzibar,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya chama tawala.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, hofu ya kushindwa kupita kwa Katiba inayopendekezwa Visiwani, ilianza kuonekana wazi wakati wa sherehe za kupokea rasimu zilizofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, wiki iliyopita.

Katika sherehe hizo, mtoa taarifa anasema, viongozi mbalimbali wa chama tawala, hawakuhudhuria kwa kuwa hawakiamini kinachopendekezwa.

Mabadiliko ya mwaka 2010 katika katiba ya Zanzibar yanataka kuwapo “Kura ya Maoni kwa mabadiliko ya baadhi ya vifungu vya Katiba” kwa jambo lolote ambalo litahusu mamlaka ya Katiba ya Zanzibar.

Kwa kuwa Katiba pendekezi imegusa maeneo mengi ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 pamoja na marekebisho ya mwaka 2010, sharti yafanyike marekebisho makubwa katika katiba hiyo ili kukidhi matakwa ya kile kinachopendekezwa; jambo ambalo wachunguzi wanasema haliwezi kukubaliwa na Zanzibar.

Haya yanatokea wakati vuguvugu la upinzani dhidi ya katiba inayopendekezwa likizidi kushika kasi kutokana kinachoitwa “udanganyifu katika upatikanaji wa theluthi mbili ya kura za kupitisha katiba.”

Tayari kura mbili ambazo mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samwel Sitta alikuwa akitambia kuwa zimekamilisha theluthi mbili za kura kutoka Zanzibar, zimeanza kuleta mzozo.

Haji Khamis Ambari, ambaye awali aliorodheshwa kuwa alipiga kura ya ndio kutoka Zanzibar, amejitokeza na kukana kupiga kura; madai ambayo tayari yamekubaliwa na aliyekuwa Naibu Katibu wa Bunge Maalum, Dk. Thomas Kashilila.

Kura nyingine ambayo itapotea ni ile ya Zakia Hamdani Meghji, mjumbe wa Tanzania Bara ambaye ameorodheshwa kuwa anatoka Zanzibar.

Meghji ambaye kwa miaka zaidi 20 amekuwa mbunge wa Bunge la Muungano kupitia mkoa wa Kilimanjaro; na ambaye ameingia bungeni kupitia uteuzi wa rais kutoka Tanzania Bara, alifanywa kuwa mjumbe kutoka Zanzibar.

Aidha, kuna taarifa kwamba wajumbe waliokuwa katika ibada ya Hijja Makka, nchini Saudi Arabia, hawakuweza kupiga kura kama ilivyotarajiwa.

Taarifa zinasema tayari kulikuwa na ujumbe kutoka ubalozi wa Tanzania nchini humo uliowataarifu kuwa wasingeweza kupiga kura kutokana na mazingira ya Hijja.

Eneo jingine linaloendelea kumomonyoa kura zinazodaiwa kuwa za “ndiyo” na kuondoa kabisa uwezekano wa kupata theluthi mbili kutoka Zanzibar, ni msululu wa waliokataa vipengele vya Katiba; wakitaka virekebishwe au viondolewe ndipo watapiga kura ya “ndiyo.”

Wajumbe hao pia wamechukuliwa kuwa walikubali Katiba pendekezi kwa shauku ya kupata theluthi mbili za kura kutoka Zanzibar.

Hata hivyo, Katiba ya Zanzibar inaelekeza kuwa jambo au sheria yoyote ambayo inapaswa kutumika Zanzibar, sharti iridhiwe na Baraza la Wawakilishi.

Iwapo jambo hilo linahitaji kufanyika marekebisho ya Katiba ya Zanzibar, sharti wananchi waulizwe kupitia Kura ya Maoni.

Vyanzo vya taarifa vinataja mambo ambayo yanaingilia Katiba ya Zanzibar, ambayo yamo katika Katiba inayopendekezwa kuwa ni pamoja na kuruhusu Mahakama ya Juu ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Rufaa, kusikiliza mashauri yaliyofanyiwa uamuzi na mahakama kuu ya Zanzibar, yakiwamo mashauri ya ndoa za kiislamu na talaka.

Mgongano katika Katiba ya Zanzibar na Katiba inayopendekezwa umeanzia katika Sura ya Kwanza, sehemu ya Kwanza, ambako kumetamkwa kuwa  Zanzibar ni Nchi, ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba.

Eneo la Nchi ya Zanzibar, yanasema marekebisho ya mwaka 2010 ya Katiba, ni Visiwa vidogo vilivyoizunguka; na bahari yake, ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ilikuwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Katika Ibara ya 2 ya Katiba ya Zanzibar inatamkwa, “Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Nako kwenye Ibara ya 26 ya Katiba ya Zanzibar kunatamkwa, “Rais wa Zanzibar ni Mkuu wa Nchi ya Zanzibar.”

Lakini Katiba Inayopendekezwa inatamka kuwa “Tanzania ni nchi moja yenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.”

Ibara ya 77 (2), ndani ya Katiba Inayopendekezwa kumetajwa kuwa “Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa Mkuu wa nchi, Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Amiri Jeshi Mkuu….”

Bali katika Katiba ya Zanzibar, katika Ibara ya 2A inatamkwa kwamba, “Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za serikali, rais aweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.”

Hilo linakinzana na Katiba pendekezi, Ibara ya 2(2) ambayo inatamka kinyume chake. Inasema rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa na mamlaka ya kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo; “na kwa upande wa Zanzibar, rais aweza kukasimu mamlaka hayo kwa rais wa Zanzibar.”

Katiba ya Zanzibar katika Ibara yake ya 132 inatamka kwamba hakuna sheria yoyote itakayopitishwa na Bunge la Muungano ambayo itatumika Zanzibar, mpaka sheria hiyo iwe ni kwa ajili ya mambo ya Muungano tu na ipitishwe kulingana na maelekezo yaliyo chini ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Sheria kama hiyo lazima ipelekwe mbele ya waziri anayehusika na hatimaye Baraza la Wawakilishi kabla ya kutumika. Masharti haya ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Katiba ya Zanzibar katika Sura ya 3 juu ya Kinga ya Haki za Lazima, Wajibu na Uhuru wa Mtu Binafsi, inatamka katika Ibara ya 24(3) kwamba, rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar katika shauri lililofunguliwa chini ya masharti ya Sura hii ya Katiba, yatasikilizwa na Mahakama Kuu mbele ya Majaji watatu bila ya kumjumuisha Jaji aliyeamua shauri hilo mara ya kwanza.

Majaji hao watatu watateuliwa na Jaji Mkuu na uamuzi wao utakuwa ni wa mwisho; na hautokatiwa rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Masharti haya ni kinyume cha Katiba Inayopendekezwa; Ibara ya 117(1) na (4) ambayo inatambua Mahakama ya Juu ya Jamhuri ya Muungano.

Akizungumzia mgongano uliopo katika Katiba ya Zanzibar na Katiba inayopendekezwa; na uhai wa Muungano kwa ujumla, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema, “Katiba hii, ni hatari kwa uhai wa Jamhuri ya Muungano.”

Amesema, “Katiba inayopendekezwa, inagongana na Katiba ya Zanzibar. Mgongano huu ni mkubwa sana. Unachochea mifarakano kwenye Muungano; unapora mamlaka ya Zanzibar na unaifanya Tanganyika kuwa ndiyo Muungano.”

Amesema yote haya yanatokea kwa sababu ya ukaidi ya CCM kung’ang’aniza kuweka maoni yao katika Katiba inayopendekezwa, badala ya maoni ya wananchi.

Katika hatua nyingine, Katiba inayopendekezwa imetupilia mbali pendekezo la wananchi lililowasilishwa bungeni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba, likitaka mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na makamu wake wathibitishwe na Bunge.

Kwa mujibu wa kifungu cha 190 (2) cha Rasimu ya Jaji Warioba,  “Mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi, watashika madaraka hayo baada ya kuthibitishwa na Bunge.”

Lakini Katiba ya Sitta inapinga, katika kifungu cha 211 (3). Inasema “Mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi, watashika madaraka hayo baada ya kuapishwa na rais.”

error: Content is protected !!