Monday , 26 February 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Katiba murua Zbar yaikwamisha CCM
Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Katiba murua Zbar yaikwamisha CCM

Spread the love

BARAZA la Wawakilishi la Zanzibar limwepitisha muswada wa sheria wa kurekebisha vifungu vya Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar pasina mabadiliko ya msingi yanayohusu Katiba ya Zanzibar, anaandika Jabir Idrissa.

Jana jioni Baraza hilo linaloundwa na wajumbe waliotangazwa washindi wa uchaguzi wa marudio wa 20 Machi 2016 uliopingwa na chama kikuu cha upinzani Chama cha Wananchi  (CUF), lilikaa kama kamati na kupitisha kifungu kwa kifungu cha mapendekezo yaliyotokana na majadiliano.

Hata hivyo, wakati vifungu vya sheria ya uchaguzi vingi viliridhiwa kubadilishwa, serikali ilikataa mabadiliko yanayohusu masuala ambayo msingi wake umeshomwa kwenye Katiba ya Zanzibar.
Zanzibar inatumia Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985.

Miongoni mwa maeneo yaliyozuilika kubadilishwa ni muda au kipindi cha urais, umri wa mtu anayefaa kugombea wadhifa huo na kutaka kazi ya kuhesabu kura na kutangaza matokeo ifanywe kwa siri huku watendaji wa serikali tu ndio wakisimamiaKatika suala la muda au kipindi cha urais, wajumbe ambao wote kasoro watatu wanatoka Chama Cha Mapinduzi  (CCM), walitaka rais atumikie wadhifa huo kwa miaka saba badala ya mitano kabla ya kuitishwa kwa uchaguzi mwingine.

Kwa mujibu wa Katiba ya sasa, Rais wa Zanzibar kama ilivyo kwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye mamlaka yake yanatajwa na Katiba ya Muungano, anaweza kuongoza kwa miaka kumi iwapo atachaguliwa tena baada ya miaka mitano ya mwanzo.

Hamza Hassan Juma, mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura, Unguja, na waziri wa zamani wa nchi ofisi ya Waziri Kiongozi, alipendekeza kwamba Rais aongoze kwa miaka saba mfululizo kwa kuwa “itapunguza gharama na kumpa muda wa kutosha rais kutekeleza malengo yake ya kuwaletea maendeleo wananchi.”

Pia alichangia pendekezo la kuweka muda mahsusi wa umri wa mtu anayefaa kugombea urais. Kwa sasa katiba inatambua umri wa miaka 40 kuendelea kuwa mtu anastahiki kugombea. Wawakilishi walitaka umri unaoanzia 35 na mwisho iwe miaka 75.

Akichangia eneo hilo, mwakilishi huyo anayeonekana fundi wa kujenga hoja zake, alisema inafaa mgombea apimwe afya yake ili kuepuka kuchaguliwa mtu ambaye afya yake ina mgogoro kiasi kwamba kila mwaka analazimika kugharamiwa matibabu nje ya nchi.

Naye mwakilishi wa Jimbo la Chumbuni, Unguja, Khamis Mahmoud Hafidh alitaka na kushikilia hoja kwamba kazi ya uandikishaji wapigakura ifanywe pasina kushirikishwa mawakala wa vyama vya siasa.

Alitaka Sheha, kiongozi wa ngazibya mtaa kwa mujibu wa sheria za Zanzibar ndio awe pekee kama wakala kwa kuwa “huyu kiongozi anawafahamu watu wa eneo lake kuliko mtu mwingine yeyote.”

Wajumbe hao wawili walishikilia hoja yao hata baada ya kupata maelezo ya kutosha upande wa serikali ukiwemo ufafanuzi uliotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Said Hassan Said Mzee.

Mohamed Aboud Mohamed, Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, aliliambia Baraza kuwa mabadiliko yaliyotakiwa na wajumbe wengi hayawezekani kwa kuwa yanavunja msingi wa Katiba ambayo ndio sheria mama.

Alisema maeneo mengine kama la kutaka kura zihesabiwe na matokeo kutangazwa bila chini ya usimamizi wa serikali, yanalazimika kubaki yalivyo katika sheria kwa kuwa ndio msisitizo wa kidunia wa kuendesha uchaguzi kwa misingi ya kidemokrasia.

Hata pale Hamza na Hafidh walipotaka Katiba ibadilishwe ili kuruhusu mapendekezo yao kufanyiwa kazi, Waziri Aboud alisisitiza kuwa lazima hilo lifanyike kwa kufuata masharti yaliyowekwa na Katiba yenyewe.

Walitaka pia kuwepo ruhusa ya wapiganaji katika vyombo vya ulinzi na usalama ya kupiga kura mapema ili baadaye watekeleze jukumu la kusimamia ulinzi siku ya uchaguzi na baada ya matokeo kitangazwa.

Wawakilishi walitaka serikali iandae mazingira ya kuwezesha Baraza la Wawakilishi au wawakilishi wenyewe kufanya mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ambayo ilifanyiwa mabadiliko makubwa mwaka 2010 na kuwezesha kuundwa kwa Serikali ya Umoja.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Hamahama Ngorongoro kutikisa maandamano ya Chadema Arusha

Spread the loveMAELFU ya wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na...

Habari za SiasaTangulizi

Waliofariki ajalini Arusha kuagwa siku ya maandamano Chadema

Spread the loveMIILI ya watu 25 waliofariki dunia katika ajali iliyohusisha lori...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali kuiburuzwa mahakamani ajali iliyoua 25 Arusha

Spread the loveMTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), imeitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Samia atoa pole ajali iliyoua 25, kujeruhi 21 Arusha

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu...

error: Content is protected !!