January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Katiba Mpya: Wanawake mnasheherekea kilio

Wanawake wa kijijini wakihangaika na shida ya maji

Spread the love

KATIBA pendekezi, tayari imepitishwa na Bunge Maalum, lililokuwa chini ya Samwel Sitta. Miongoni mwa walioonyesha furaha, ni baadhi ya wanawake hasa kuhusu suala la usawa wa jinsia bungeni, maarufu kama asilimia 50 kwa 50.

Wanawake ambao mara baada ya Katiba hiyo kupitishwa walionyesha furaha yao hadharani, ni wale wanaojitambulisha kama Mtandao wa Wanawake na Katiba.

Hawa walionyesha furaha yao Ijumaa, 3 Oktoba, kupitia kituo kimoja cha televisheni nchini. Hii ilikuwa siku moja baada ya Bunge Maalum kupitisha Katiba Inayopendekezwa.

Wengine ni Umoja wa Wabunge Wanawake (TWPG), ambao walikuwa wajumbe wa Bunge Maalum kutoka CCM. Hawa walifanya sherehe mjini Dodoma, tarehe 4 Oktoba 2014.

Wabunge wenzao kutoka vyama vya  NCCR- Mageuzi; Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendelezo (Chadema), vinavyounda Muungano wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA), hawakushiriki katika sherehe hizo.

Wajumbe wa Bunge Maalum kutoka vyama hivyo, walisusia mchakato wa kuandika katiba mpya. Hii ni baada ya kujiridhisha kuwa Katiba inayotafutwa siyo ya wananchi bali ni ya CCM; na kwamba maoni ya wananchi yaliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yalikuwa tayari yametupwa.

Wanawake hao kutoka CCM pengine wamesheherekea wakiamini kuwa idadi ya wanawake bungeni itaongezeka na kufikia asilimia 50 iwapo Katiba Inayopendekezwa itapitishwa.

Hata hivyo, uchambuzi katika Katiba Inayopendekezwa unaonyesha kuwa suala la usawa wa jinsia bungeni, ni kiini macho; kwani ndani yake, hakuna popote ambako kumebainishwa utaratibu wa kupata asilimia 50 ya wanawake.

Katika Katiba Inayopendekezwa, Sura ya 10, Sehemu ya kwanza  kifungu 129 (5), kinaishia kueleza kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano, litakuwa na wabunge wasiozidi 360. Wabunge hao watakuwa wa aina tano.

Aina ya kwanza, ni wabunge watakaopatikana kwa kuchaguliwa na wananchi majimboni kwa kupigiwa kura. Hawa wametajwa kwenye kifungu 129(4); “…kutazingatiwa uwakilishi ulio sawa kati ya wabunge wanawake na wanaume.”

Lakini tofauti na Rasimu ya wananchi – Rasimu ya Jaji Joseph Warioba – iliyotamka bayana kuwa kila jimbo litawakilishwa na watu wawili, mwanamke na mwanaume, Katiba pendekezi haikueleza usawa huo utapatikanaje katika majimbo.

Hivyo basi, kile kinachoitwa, “Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaweka utaratibu ambao utawezesha kupatikana usawa,” hakitaweza kutekelezeka kwa kuwa Katiba haijabainisha utaratibu utakaotumika kupata idadi sawa.

Kulingana na idadi ya majimbo 239 ya Bunge la Jamhuri yaliyopo sasa, kila jimbo likiwakilishwa na mwanamke na mwanaume, Bunge litakuwa na wabunge 478 . Idadi hii inazidi idadi  iliyowekwa katika Rasimu ya Warioba ilikopendekezwa kwamba wabunge wasizidi 360.

Wabunge wengine watano, kwa mujibu wa Katiba iliyopendekezwa, ni watu wenye ulemavu. Hawa kwa mujibu wa Katiba inayopendekezwa, kifungu 129 (2) (b), ”Watateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kuchaguliwa kuwa wabunge.”

Hata hivyo, Katiba inayopendekezwa haikueleza kati ya wabunge wenye ulemavu, wanawake watakuwa wangapi. Hata kwa idadi iliyopendekezwa – wabunge watano – tayari hakuwezi kupatikana asilimia 50 kwa 50. Asilimia 50 ya wabunge watano, ni wabunge wawili na nusu.

Hii inaashiria kuwa kinachohubiriwa, hakiwezi kutekelezeka. Katiba inayopendekezwa haijaweka utaratibu ulio wazi kuhakikisha kunakuwa na idadi sawa ya wanawake na wanaume kutoka kwa watu wenye ulemavu.

Lakini kibaya zaidi, wenye ulemavu watateuliwa na rais. Hawatajiteua wenyewe. Hapa anayeweza kuteuliwa anaweza kuwa siyo mwakilishi wa wenye ulemavu; anaweza kuwa ndugu, jamaa au watu walio karibu na rais; au kutoka chama anachotoka rais.

Swali la msingi hapa ni kwamba, ni kwa nini  wabunge wenye ulemavu wasichaguliwe moja kwa moja na wenye ulemavu wenyewe  ili wawajibike kwa waliowachagua?

Aidha, kifungu 129 (2) (c) kinasema, rais atakuwa na mamlaka ya kuteua wabunge wasiozidi 10. Lakini haikuelezwa wanawake watakuwa ni wangapi. Hivyo rais habanwi kuteua, kwa mfano,  wanaume wanane na wanawake wawili. Katiba haikuweka nguvu kwa rais kumlazimisha kuteua kwa usawa wa jinsia.

Wabunge wengine watakaoweza kuteuliwa na rais ni Spika endapo atakuwa hakuchaguliwa kutokana na wabunge na  Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye naye moja kwa moja, ni mbunge.

Hivyo, kati ya wabunge wasiozidi 360, ukiondoa wabunge 17 (10 wa kuteuliwa na rais, wabunge watano wenye ulemavu, spika na mwanasheria mkuu wa serikali), watabaki wabunge 343 ambao wanapaswa kuchaguliwa kutoka majimboni.

Ni utaratibu gani utatumika kuwezesha kupatikana idadi sawa ya wanawake na wanaume kutoka wabunge hawa (343) wa majimbo?

Je, kwa hesabu hizi, Katiba inayopendekezwa itaweza kuleta  usawa  wa 50 kwa 50 katika uwakilishi bungeni?

Zaidi ya hayo, Katiba inayopendekezwa haikueleza katika ngazi za madiwani na uenyekiti wa serikali za mitaa na vijiji asilimia 50 ya wanawake itapatikana vipi.

Ndiyo sababu tunasema kuwa hatua ya wanawake kusheherekea Katiba Inayopendekezwa katika suala la uwakilishi wa wanawake, ni kutojitambua. Ni sheherehe za maumivu.

Hivyo basi – tusishangae kwa papara hizi za kupitisha katiba bila maridhiano – tukakuta idadi ya wawakilishi wanawake bungeni, kwenye halmashauri na serikali za mitaa/vijiji, wakapungua kuliko ilivyo sasa.

Hivi  sasa, kwa mujibu wa orodha ya wabunge  Mei 2014,  kati  ya wabunge wote 357  wa Bunge la Jamhuri, wanawake ni 127. Ni sawa na asilimia 36 ambapo 106 wanatokana na viti maalum na 21 wamechaguliwa moja kwa moja na wananchi.

Lakini cha kujifunza hapa ni kwamba asilimia 30 imeweza kufikiwa kutokana na ukweli kwamba Katiba ya  sasa (1977) inaeleza kuwa kutakuwa na asilimia isiyopungua 30 ya wanawake  bungeni na watapatikana kwa kupitia viti maalum na kupigiwa kura majimboni.

Madiwani nao hawazidi asilimia 35 ya wanawake; wenyeviti wa  mitaa  hawafiki hata asilimia moja. Wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji nchini wako zaidi ya 12,000. Lakini wanawake wenyeviti hawafiki 800.

Kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2009 wanawake wenyeviti wa mitaa na vijiji hawakuzidi 200 nchi nzima.

Jambo la kusikitisha ni kwamba Katiba inayopendekezwa imeshindwa kuweka vipengele vitakavyoleta mageuzi ya kweli katika uwakilishi wa wanawake.

Hivyo tunaweza kusema kwa kujiamini kwamba Katiba inayopendekezwa ikipitishwa na wananchi katika kura ya maoni, Tanzania itashuhudia wanawake wakiwa na uwakilishi mdogo na dhaifu bungeni kuliko sasa.

Lakini kibaya zaidi, Bunge la Jamhuri litaendelea kuwa na idadi kubwa ya wabunge isiyo ya lazima na hivyo kulifanya taifa kupoteza  fedha nyingi za walipa kodi bila sababu kutokana na  kuwahudumia wabunge hao.

Rasimu ya Jaji Joseph Warioba ilipendekeza wabunge 75 tu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.  Idadi hii ndogo ya wabunge ingeokoa fedha nyingi zitakazotumika, kulinganisha na kuhudumia wabunge 360 wanaopendekezwa katika Katiba  ya Sitta.

Fedha hizo zingeweza kutumika kuwapatia wananchi huduma za maji, shule, barabara, umeme na afya; ikiwepo afya ya uzazi.

Kwa mujibu wa Katiba inayopendekezwa, siyo tu bungeni, halmashauri na mitaa /vijiji kutakuwa na uwakilishi usio sawa kati ya wanawake na wanaume; bali pia na kwenye baraza la mawaziri.

Ibara ya 115 (1) ya Katiba Inayopendekezwa inasema,  “Kutakuwa na Mawaziri na Manaibu mawaziri wasiozidi 40.”

Lakini Katiba hiyo haikutamka kuwa mawaziri hao watateuliwa  kwa utaratibu upi ili kuwepo usawa wa jinsia.

Kwa msingi huo, kitendo cha wanawake kufurahia Katiba inayopendekezwa, ni kusheherekea anguko kubwa la wanawake katika nafasi za uwakilishi na uongozi serikalini.

Katiba inayopendekezwa ikipitishwa, itakwamisha taifa hili kutekeleza kwa vitendo, itifaki ya  Jumuiya ya  Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ambayo inaweka mkazo wa suala la 50 kwa 50 katika uwakilishi kuwa liwe limetekelezwa mwaka 2015.

Je, katika hali hiyo, Katiba Inayopendekezwa inastahili kura ya NDIYO kwa wanawake au HAPANA, wakati suala la asimilia 50 kwa 50 kuhusu uwakilishi katika vyombo vya maamuzi bado lina utata? Tafakari.

Mwandishi wa makala haya ni mwanaharakati wa haki za wanawake. Anapatikana  kwa simu  0754 464368  na barua pepe: ananilea_nkya@yahoo.com

error: Content is protected !!