Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Katiba mpya, Tume huru zavigawa vyama vya siasa
Habari za SiasaTangulizi

Katiba mpya, Tume huru zavigawa vyama vya siasa

Rais Samia Suluhu Hassan
Spread the love

 

MJADALA wa nini kianze kupatikana kati ya katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, umevigawa vyama vya siasa, baada ‘ya kutofautiana misimamo juu ya suala hilo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hadi sasa kumeibuka makundi mawili ya vyama hivyo, ambapo moja linaunga mkono upatikanaji wa katiba mpya kwanza, huku lingine likiunga mkono kuanza na tume huru ya uchaguzi.

Chama cha Wananchi (CUF), kimeungana na ACT-Wazalendo, katika kuunga mkono upatikanaji wa tume huru ya uchaguzi kabla ya katiba mpya.

Huku hoja yao ikidai kuwa mchakato wa kupata katiba hiyo, ni mrefu hauwezi kukamilika katika kipindi cha chaguzi zijazo, Uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa wa 2024 na Mkuu wa 2025.

Jana Jumapili, ACT-Wazalendo, kupitia Mwenyekiti wake, Juma Duni Hajji, jijini Dar es Salaam, kilizindua operesheni ya tume huru ya uchaguzi, kuelekea katiba mpya yenye maoni ya wananchi.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, kwa simu leo Jumatatu, tarehe 21 Machi 2022, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma CUF, Mhandisi Mohamed Ngulangwa, amesema kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi kabla ya chaguzi zijazo kutasaidia kupatikanaji wa katiba.

“Msimamo wa CUF ni kupata katiba mpya, lakini kupata mapema iwezekanvyo tume huru ya uchaguzi ili ifanye kazi tunapoenda 2025 tuwe nayo na sisi tunawaza zaidi ya 2025 sababu kuna uwezekano katiba mpya ikachelewa na tukashindwa kupata tume huru,” amesema Mhandisi Ngulangwa na kuongeza:

“Sisi vyote viende pamoja, tunaamini kama ikitokea kuna shida ya kupata katiba tume huru ya uchaguzi itaenda kubadilisha sura ya Serikali, maana yake tume itafanikisha uchaguzi huru na wa haki kama ambavyo ingepatikana katiba.”

Msimamo huo wa ACT-Wazalendo na CUF, umepingwa na NCCR-Mageuzi na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), ambavyo vimesema katiba mpya inatakiwa ipatikane kabla ya tume huru ya uchaguzi.

Mwenyekiti wa Kikosi kazi, Profesa Rwekaza Mukandara

Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano na Umma, NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye, amesema wanaotaka tume huru ya uchaguzi kwanza wanapigania mabadiliko kwenye uchaguzi na siyo ya nchi nzima.

“Ukisema unataka tume huru kabla ya katiba, unakwenda kwenye matokeo kabla ya mfumo mzima, ambao tunaoupigania. Unapowaza tume unawaza uchaguzi lakini unapowaza katiba unataka mifumo ya nchi ibadilike,” amesema Simbeye.

Simbeye amesema “ukiwaza tume hauwazi mifumo ya uendeshaji, asilimia kubwa chaguzi zetu haziharibiwi na tume peke yake, hata Jeshi la Polisi wanaharibu, wakiharibu hakuna mahali wanawajibika. Ukiwa na tume bado jeshi linaweza kuharibu na hakuna sheria inayowagusa, ndiyo maana tunataka katiba sababu ndani yake kuna tume na taratibu nzuri za uchaguzi.”

Alipoulizwa kama katiba mpya haitapatikana wakati wa chaguzi zijazo NCCR-Mageuzi kitachukua hatua gani, Simbeye amesema ni vyema chaguzi hizo zikasogezwa mbele hadi mchakato wa upatikanaji katiba hiyo ubadilike.

“Ukiniuliza mimi naangalia nchi sio matukio ya uchaguzi, kwa maoni yangu niko radhi uchaguzi upelekwe mbele hata kama kwa miaka miwili ili katiba yenye tume huru ya uchaguzi ipatikane na kila mfumo wa nchi uwe imara kwa mujibu wa katiba, tuondokane na matukio ya onyo kwenye uchaguzi,” amesema Simbeye.

Eugine Kabendera, Katibu Mkuu wa Chaumma Bara

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CHAUMMA, Eugine Kabendera amesema “mjadala wa katiba moja ni kama wa kuku na yai nani alianza. Wanasayansi watakimbilia kwenye yai, lakini aliyeanza ni kuku, mama kwanza anakuja mtoto. Watu wanataka kuingizwa mkenge lakini katiba kwanza kisha tume.”

Kabendera amesema, katiba mpya inahitajika kabla ya tume huru ya uchaguzi kwa kuwa ni sheria mama ya nchi na ndiyo inayosimamia vyombo vyote vinavyoendesha mchakato wa uchaguzi, ikiwemo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Tukienda kwenye tume hapa wanasiasa tutakuwa wabinafsi na tutakuwa tumesahau Watanzania. Tukumbuke kuna mambo ya msingi wengi watayapata kupitia katiba, tusijisahau kukimbilia tume ingawa ni matakwa ya wanasiasa japokuwa nao ni Watanzania,” amesema Kabendera.

Kabendera ameshauri ni bora Serikali iliyoko madarakani iongezewe muda ili uchaguzi usogezwe mbele hadi pale katiba mpya itakapopatikana.

“Ukweli tume huru ni ubinafsi wa wanasiasa, tunarudisha uhuru wa wanasiasa kuchaguliwa, lakini sisi tunasema suala ni nia njema, watu wakiwa tayari kubadili katiba hata mwaka huu tunapata katiba,” amesema Kabendera na kuongeza:

“Tuko tayari kumuongezea muda Rais aliyepo madarakani, badala amalize 2025, tumuongezee kipindi cha mpito ili katiba ipatikane.”

Chama cha NCCR-Mageuzi na CHAUMMA, vinaungana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutaka katiba mpya kabla ya tume huru ya uchaguzi.

1 Comment

  • Tamaa ya madaraka ndiyo inayotaka Tume Huru. Je, Tume Huru italindwaje kama haipo kwenye Katiba?
    Katiba Mpya ikitoa uraratibu wa wa mfumo wa Tume, basi uundwaji wa Tume Huru utakuwepo.
    Hii itasaidia wakati wowote, Tume yeyote ikiundwa itakuwa huru…siyo Tume ya siasa peke yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!