Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Katiba Mpya: Tuanzie pale alipoishia Jaji Warioba
Makala & UchambuziTangulizi

Katiba Mpya: Tuanzie pale alipoishia Jaji Warioba

Prof. Ibrahim Lipumba
Spread the love

 

PROFESA Ibrahim Haruma Lipumba, mwenyekiti wa taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), ametonesha kidonda kilichoanza kusahauliwa na pengine kutotaka kuguswa. Anaandika Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza juzi Jumatatu kwenye maadhimisho ya miaka 100 ya Mahakama, jijini Dodoma, Prof. Lipumba alisema, Rais wa Jamhuri, Dk. John Magufuli, aliahidi Novemba mwaka 2015, kuhuisha mchakato wa Katiba Mpya.

Akamtaka kutekeleza ahadi yake kama ambavyo aliahidi na wananchi wanavyotaka.

Alisema, “…mheshimiwa Rais, wakati ulipokuwa ukizindua Bunge, Novemba mwaka 2015, ulieleza Watanzania kuwa serikali yako imepokea kiporo cha mchakato wa Katiba Mpya.”

Akaongeza, “mchakato wa Katiba Mpya ambao watu wengi waliotoa maoni, haukuweza kukamilika katika awamu iliyopita, kutokana na kutokamilika kwa wakati, zoezi la uandikishaji wapiga kura.”

Rais Magufuli alitoa ahadi ya kushunghulikia mchakato wa Katiba Mpya, wakati akifungua Bunge jipya, Novemba mwaka 2015.

Katika hotuba yake hiyo, Profesa Lipumba alisema, Rais Maguli alieleza kuwa anatambua na kuthamini kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge la Katiba lililotupatia Katiba Pendekezwa.

Akaongeza: “Tutatekeleza wajibu wetu kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba.”

Ahadi hiyo ya Rais Magufuli, ilipewa nguvu na Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015/20 inayoeleza kuwa itakamilisha mchakato huo.

Kutokana na kauli hiyo, Prof. Lipumba akaenda mbali zaidi. Akasema, Rais Magufuli alirejea ahadi yake ya kutekeleza hilo, alipokuwa akipokea ripoti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mwanasiasa huyo amemuomba Rais Magufuli katika kipindi chake cha mwisho cha uongozi wake, ahakikishe Katiba Mpya inapatikana ili iwe alama yake kwa Watanzania.

Alisema, “viporo ulivyovitoa ambavyo hujavitekeleza, 2015 ulivisema utavitekeleza, natoa wito hivyo viporo vyote katika kipindi hiki uweze kutekeleza.

“Utakapomaliza kipindi chako, watu watakaoweza kuyalinda mafanikio uliyoyaleta katika nchi yetu ni kuwa na Katiba inayotokana na mapendekezo ya Watanzania.”

Jaji,Joseph Warioba Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba

Rais Magufuli aliingia madarakani tarehe 5 Novemba 2015, baada ya kuapishwa kumrithi Jakaya Kikwete. Kwa sasa, Rais Magufuli yuko katika kipindi cha mwisho cha uongozi wake, ambapo anategemewa kumaliza ngwe yake ya urais, Novemba 2025.

“Nina uhakika kwa sababu hili jambo ni la kwako, si la kwetu. Liko katika uwezo wako, naamini utashughulikia. Utatuachia urithi wa Katiba inayotokana na wananchi,” alieleza Prof. Lipumba.

Akamtaka kuwatumia waliokuwa wajumbe wa Bunge la Katiba ambao baadhi yao ni wateule wake, kufufua mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya kwa kutumia Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Waliokuwamo kwenye Tume ya Jaji Warioba, ni Prof. Palamagamba Kabudi na Humphrey Polepole. Makamu wa Rais, Samia Hassani Suluhu, alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba; huku Naibu Spika wa sasa, Dk. Tulia Ackson, alikuwa mjumbe wa Bunge Maalum kutokea Kamati ya vyuo vikuu, iliyochambua na kutoa mapendekezo kuhusu rasimu ya Jaji Warioba.

“Kwa bahati ulikuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba na Mama Samia alikuwa Makamu Mwenyekiti, kuna wazee wazito Prof. Kabudi walikuwa Wajumbe wa Tume ya Jaji Warioba, kuna vijana wako ndio alikuwa mjumbe,” ameeleza Prof. Lipumba.

Hata hivyo, tarehe 1 Novemba 2018, akizungumza katika kongamano kuhusu hali ya uchumi na siasa Tanzania, lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema, hategemei kutenga fedha kwa ajili ya mchakato huo kwa sasa.

Rais Jakaya Kikwete (kushoto) na Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein (katikati) wakionesha katiba Mpya

Alisema, kuliko fedha kutumika katika mchakato huo, ni bora zielekezwe katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge-SDG).

Aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva, tarehe 2 Aprili 2015, alinukuliwa akisema, kura ya maoni iliyokuwa ifanyike 30 Aprili 2015, imeghairishwa kutokana na kutokukamilika kwa uandikishaji wa dafatari la wapiga kura.

Lakini pamoja na kughairishwa kwa mchakato wa kura ya maoni, wengi wanaona kuwa ni busara mchakato wa Katiba Mpya ukaanzia pale ambapo Tume ya Jaji Warioba ilipoishia.

Hii ni kwa sababu, kura za kupitisha Katiba Inayopendekezwa, zilipigwa na wafu waliokuwa wametangulia mbele ya haki, mahujaji waliokuwa wanampiga shetani mawe katika Mlima Ararat, Makka nchini Saudi Arabia, wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini India na wajumbe wengine wasiojulikana kwa majina wala walikokuwa wakati wa kura hiyo!

Aidha, matakwa ya Sheria ya Kura ya Maoni ya mwaka 2013, yameweka utaratibu mgumu wa uendeshaji wa kura ya maoni, ambapo kila hatua inayotakiwa kuchukuliwa haiwezekani kuahirishwa wala kuongezewa muda.

Kwa mfano, ndani ya siku kumi na nne tangu tarehe ya kupokea Katiba Inayopendekezwa, rais alitakiwa – kwa amri iliyotangazwa katika gazeti la serikali na baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar – kuielekeza Tume kuendesha kura ya maoni.

Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Katiba, Humphrey Polepole
Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Katiba, Humphrey Polepole akitoa ufafanuzi juu ya muundo wa Serikali katika Rasimu ya Katiba Mpya

Amri ya kura ya maoni inatakiwa kufafanua kipindi cha kampeni na kipindi ambacho kura hiyo inatakiwa kufanyika. Rais Kikwete alikwishatoa amri kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha sheria.

Kwa mujibu wa sheria hii, Rais hana mamlaka yoyote, kutengua amri yake au kutoa amri mpya ili kuwezesha kura ya maoni kufanyika kwa tarehe nyingine, tofauti na tarehe iliyotangazwa kwenye amri ya kwanza.

Ndani ya siku saba baada ya kuchapishwa kwa Katiba Inayopendekezwa, Tume inatakiwa kuandaa swali la kura ya maoni na kulichapisha katika gazeti la serikali.

Ndani ya siku kumi na nne baada ya kuchapisha swali hilo, Tume inatakiwa kutoa taarifa ya kufanyika kwa kura ya maoni. Inatakiwa kueleza kipindi cha kuhamasisha na kuelimisha umma juu ya kura hiyo na siku ya kura yenyewe.

Naye msimamizi wa kura ya maoni anatakiwa, ndani ya siku 21 baada ya kuchapishwa kwa taarifa ya Tume, kuwajulisha wananchi katika jimbo lake la uchaguzi kuhusu utaratibu wa kufanyika kwa kura ya maoni.

Aidha, Tume inatakiwa kutoa elimu kwa umma juu ya Katiba Inayopendekezwa kwa muda wa siku sitini tangu katiba hiyo ilipochapishwa.

Tume ilikwishaandaa na kuchapisha swali la kura ya maoni na ilikwishatoa taarifa ya kura ya maoni na ratiba yake. Tume haina mamlaka yoyote, kwa mujibu wa sheria hiyo, kutengua taarifa yake na kutoa taarifa nyingine, au kuweka ratiba nyingine badala ya ratiba iliyokwishatolewa.

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samwel Sitta

Haiwezi kujiongezea muda wa kutoa elimu kwa umma juu ya Katiba Inayopendekezwa; au kujipa muda mwingine kwa vile muda uliowekwa na sheria haukutumika ipasavyo.

Nao, wasimamizi wa kura ya maoni hawana mamlaka yoyote kisheria ya kuongeza au kuongezewa muda wa kutoa taarifa kwa umma chini ya kifungu cha 5(2) cha sheria hiyo.

Kwa kifupi, hakuna uwezekano kisheria wa kurudi nyuma. Hakuna uwezekano kisheria wa kuongeza muda kwa hatua zozote ambazo muda wake ulikwishapita.

Kwa sababu hizi, hakuna uwezekano wa kufanyika kura ya maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni kama ilivyo kwa sasa.

Tume ya uchaguzi yenyewe imeshatangaza kwa maandishi katika Randama ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2015/16, kwamba, “Sheria ya Kura ya Maoni ina maeneo ambayo hayawezi kutekelezeka na baadhi yake kuwa na tafsiri zaidi ya moja. Eneo ambalo linaweza kuleta utata ni uhesabuji wa kura na utangazaji matokeo.”

Inasema, “suluhisho la changamoto” hiyo ni “sheria hii kufanyiwa marekebisho kwenye maeneo ambayo hayatekelezeki au kuwa na tafsiri zaidi ya moja.”

Rais anapaswa kuanzia pale alipoishia Jaji Warioba kwa kuwa Katiba Pendekezwa, inaligawa taifa katika nyanja nyingi – Tanganyika na Zanzibar na kati ya wanachama wa CCM na wale wa upinzani.

Katiba Pendekezwa inawagawa watawala na watawaliwa; wazalendo na mamluki; walio chini ya sheria na walio juu ya sheria; wazee kwa vijana; wanawake matajiri na wanawake maskini; waliozaliwa kabla ya uhuru na baada ya uhuru.

Migawanyiko hii haiwezi kuliacha taifa letu likawa salama huko tuendako. Hata ndani ya vyombo vya ulinzi, tayari kuna mgawanyiko kati ya watakaoruhusiwa kupiga kura na watakaopigiwa kura kwa niaba. Kwa mtu yeyote anayelitakia mema taifa letu, hawezi kuunga mkono kitu kinacholigawa taifa lake katika mapande mawili yanayolingana.

Kura mbili zilizopitisha Rasimu zina Utata

Kwamba, kura za upande wa Bara zilitosha na hata ungeondoa zenye utata, kupitisha Katiba Inayopendekezwa. Lakini hali ni tofauti na upande wa Zanzibar. Rasimu ilipitishwa kwa kura mbili tu. Hizi nazo baada ya kutangazwa uliibuka utata wa kisheria na kimaadili.

Mzanzibari mmoja alidai hakupiga kura kabisa, tena kwa kiapo. Lakini jina lake lilionekana kuwa limepiga kura. Mtanganyika mmoja, kwa jina la Zakhia Meghji, alipiga kura lakini ikahesabika kupigia kura upande wa Zanzibar.

Hata kama ana nasaba na Zanzibar, lakini uteuzi wake ulimtaja kama Mtanganyika. Kwa utata huo, kura zote mbili zilizodaiwa kupitisha rasimu, hazipo tena. Yeyote aliyebaki na chembe ya uadilifu katika nafsi yake, hawezi kuunga mkono rasimu iliyopitishwa katika kiwingu cha mashaka ya namna hii.

Hata bila kusoma maudhui yake, inatosha kuikataa. Rais ameonekana kama vile anasema, kuunga mkono wizi ni dhambi kuliko kuiba kwenyewe.

Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wakiwa katika moja ya vikao vyake

Ndani na nje ya Bunge Maalum; ndani na nje ya chama tawala; na ndani na nje ya kundi la upinzani; hakuna maridhiano kuhusu rasimu hii.

Naye aliyekuwa mkuu wa nchi alikuwa anampiga vijembe mwenyekiti wa Bunge Maalum kuwa anakurupuka. Akafika mahali akakutana na viongozi wenzake kutoka vyama vya upinzani kama ishara ya kutokubaliana na mambo yanavyokwenda bungeni.

Lakini punde tu, akapokea rasimu hiyo kwa mbwembwe! Wabunge wa Bunge Maalum walikuwa wanaunga mkono rasimu hiyo ndani ya Bunge, lakini wakiwa nje wanadai hiyo siyo rasimu yao; mwenyewe anajua alikoitoa na atakakoipeleka!

Katiba haipaswi kuwa na chembechembe za kimakundi wala kimaslahi. Katiba ni matokeo ya mchakato (process). Si maudhui tu. Kama katiba ni maudhui, tungefungia chumbani wanasheria wawili au hata mmoja wakaandika kisha sisi tukapiga kura ikawa katiba yetu.

Hata bila kuisoma lakini ukiangalia haya, inatosha kuikataa. Mchakato ulioileta hii rasimu mahali ilipo sasa, ulikuwa na makona mengi, tena yaliyolazimishwa na kundi dogo kwa makusudi maalum. Mathalani, kwa nini iliamriwa ghafla kuwa badala ya kupigia kifungu kwa kifungu ili kukipitisha, ikaamriwa zipigiwe ibara zote kwa pamoja?

Inawezekana vipi ibara inayohusu kondoo, nyingine inahusu wazee, na nyingine inahusu miamba zipigiwe kura moja mara moja? Kisingizo hapa ni eti muda ulikuwa hautoshi? Walikuwa wanakimbilia nini?

Ukweli walikuwa hawakimbii ili kuokoa fedha, bali kuwahi kabla ya muda waliopewa na rais haujaisha maana kulikuwa na tishio kuwa muda ukiisha hautaongezwa! Kwa hiyo mchakato ukaingia kasoro kwa shinikizo fulani.

Kwa kuwa mchakato uligeuka mchanyato, hata bila kuisoma rasimu hii, inatosha kuikataa hata kama maudhui yake yanaweza kuwa yanaahidi paradiso hapa duniani!

Rais mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete

Tuliamua kuandika katiba mpya kwa sababu nyingi, lakini moja kubwa, ni kwa sababu katiba tuliyo nayo, iliandikwa na chama kimoja wakati wa chama kimoja. Hivi sasa tuna vyama vingi.

Rasimu inayopendekezwa imeandikwa na vyama vingapi? Jibu rahisi. Imeandikwa na kundi moja au hata chama kimoja. Haijalishi chama hicho ni UKAWA, CCM au kingine chochote.

Kwa nyakati tulizonazo, hata kama chama kingekuwa kizuri sana na kina asilimia 99 ndani ya bunge na serikali za mitaa; hakiwezi na hakipaswi kutuandikia katiba ya nchi. Huu ni msingi mama wa uandishi wa katiba yoyote.

Kwa maana hiyo, walioondoka bungeni na waliobaki bungeni, hawapaswi kutuandikia katiba. Hawawezi kutuhakikishia kuwa hawatajipendelea katika uandishi wa katiba. Kundi lililobaki ndani ya bunge; liwe ni kutoka chama kimoja au vinginevyo, linageuka kuwa chama kimoja dhidi ya kingine kilichotoka nje.

Tunaikataa katiba iliyopo kwa sababu iliandikwa na chama kimoja; hatuwezi kukubali rasimu nyingine iliyoandikwa na chama kimoja au kundi moja lenye malengo yanayofanana.

Hata bila kusoma rasimu, sababu hii inatosha kutufanya tukatae rasimu ya katiba mpya, hata kama Ikulu ya Rais Kikwete, itatumia bilioni tano kutushawishi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the love  TUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

error: Content is protected !!