January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Katiba mpya imeota mbawa

Spread the love
· Kinachotafutwa sasa, ni Katiba ya CCM

JOHN Shibuda, mbunge wa Maswa (Chadema) na Leticia Nyerere, mbunge wa Viti Maalum kupitia chama hicho, hawako Dodoma kwenye mkutano wa Bunge Maalum la Katiba.

Aliyeko Dodoma mpaka sasa na ambaye anahudhuria mkutano wa Bunge Maalum la Katiba, ni Said Arfi, mbunge wa chama hicho katika jimbo la Mpanda Kati.

“Hawa watu hawako hapa. Nakuambia hawako. Kinachoandikwa na vyombo vya habari, siyo kilichopo Dodoma. Hapa kuna mkakati wa kuonyesha UKAWA umesambaratika,” ameeleza mbunge mmoja wa CCM ambaye hakupenda kutajwa jina lake.

Amesema, “Ninachokuambia ndugu, chama chetu kimekwama. Sitta (Samwel Sitta, mwenyekiti wa Bunge la Katiba) amekwama. Kama ni ushindi, UKAWA tayari watakuwa wameshinda.”

Amesema, Shibuda na Alfi hajaonekana Dodoma na hakuna ushahidi unaoweza kuthibitika mpaka sasa kuwa walikuwapo.

Naye Chiku Abwao alikuwapo Dodoma kwa shughuli zake binafsi na jana alikutana na waandishi wa habari kueleza msimamo wake kuhusu jambo hilo.

Alfi alikuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho. Alijiuzulu mwanzoni mwa mwaka huu kwa kile kilichoitwa, “Mkakati wa kutaka kumrejesha Zitto Kabwe kwenye nafasi yake.”

Muungano wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA), unaoundwa na vyama vitano vya siasa – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR- Mageuzi, DP na NLD – wamesusia mkutano wa Bunge Maalum la Katiba kwa kile walichodai, “Sitta amegeuza Bunge la Katiba kuwa mkutano mkuu wa chama chake.”

Vyanzo vya taarifa kutoka Dodoma vinasema, tayari maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya yametupwa rasmi, baada ya baadhi ya Kamati za Bunge hilo kuanza kifuta rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyopendekeza muundo wa serikali tatu.

“Rasimu inayojadiliwa bungeni, ni rasimu ya serikali mbili. “Kitu ambacho tulikuwa wazi jana kabla hatujaanza mjadala, Katika ngazi ya Kamati tulipigia kura na maoni ambako wengi wanataka tuendelee na muundo wa muungano wa serikali mbili,” ameeleza Ummy Mwalimu, mwenyekiti wa kamati namba moja.

Kauli ya Mwalimu, inathibitisha kile ambacho UKAWA wamekuwa wakieleza, kwamba Sitta ameibua mambo mapya na kutaka kuyaingiza katika mjadala wa Rasimu ya Pili ya Katiba.

Mambo yote ya Muungano yametajwa katika Sura ya Kwanza na Sura ya Sita ya Rasimu ya Katiba. Sura hizo mbili ndiyo “moyo wa Katiba.”

Miongoni mwa ambayo Sitta amesema yataingizwa ndani ya Rasimu ya Katiba na ambayo hayahusu masuala ya Muungano, ni masuala yote yanayohusu serikali za mitaa, kilimo, mifugo, uvuvi, wakulima na aridhi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa hati ya makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, masuala yote ambayo Sitta ametaka yaingizwe bungeni, hayana uhusiano wowote na muundo wa Muungano uliopendekezwa na rasimu.

Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba, imependekeza muundo wa Muungano wa serikali tatu – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Muungano.

error: Content is protected !!