July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Katiba Mpya batili

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta akitafakari jambo

Spread the love

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali Visiwani Zanzibar, Othuman Masoud Othuman, amejiuzulu ujumbe katika Kamati ya Uandishi wa Katiba Mpya.

Taarifa kutoka Dodoma ambako Bunge Maalum la Katiba linaendelea na shughuli zake zinasema, kigogo huyo muhimu katika upatikanaji wa katiba, tayari amemjulisha mwenyekiti wa bunge hilo, Samwel Sitta, kujiuzulu nafasi hiyo.

Sitta alimteua Othuman kuwa mjumbe wa kamati ya uandishi – kamati ambayo ndiyo moyo wa bunge hilo katika kuandika vifungu, ibara na sura za rasimu.

Kamati ambayo Othuman aliteuliwa kuwa mjumbe, ndiyo yenye jukumu la kuandika katiba itakayokwenda kwa wananchi kupigiwa kura.

Othuman amejiondoa katika kamati hii kwa sababu amekataa kuwa msaliti. Amegoma kusaliti wananchi wake; taifa lake na watu wa Visiwani.

Kujiondoa kwake katika kamati hii, kutakuwa pigo kubwa kwa Sitta na chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – pamoja na wale wanaomuunga mkono katika harakati zake za kuingia Ikulu mwaka kesho. Upande mwingine utakuwa ushindi kwa Muungano wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Muungano wa UKAWA unaoundwa na vyama vya NCCR- Mageuzi; Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema); Chama cha Wananchi (CUF), National League for Democracy (NLD) na Democratic Party (DP), ulijiondoa bungeni 16 Aprili 2014, kwa kile walichodai, “Bunge la Katiba kugeuzwa mkutano mkuu wa CCM.”

Wengine waliondoka na UKAWA, ni wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka kundi la 201.

Walimtuhumu Sitta kulitumia bunge hilo kulinda maslahi ya chama chake. Hii ni kwa sababu, badala ya bunge kujikita katika kujadili na kuboresha Rasimu ya Katiba, linafanya kazi ya kukusanya maoni; kubandua ibara na kuingiza ibara mpya.

Msimamo wa Othuman Masoud katika utafutaji wa katiba mpya unafahamika. Yeye ni mtetezi mkuu wa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na Jaji Joseph Sinde Warioba, mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Rasimu ambayo Jaji Warioba aliwasilisha bungeni inazungumzia Jamhuri ya Muungano kuwa nchi ya Shirikisho la Serikali tatu – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Muungano.

Sitta anahaha kubadilisha maoni ya wananchi na kujaza maoni ya chama chake. Tayari amefumua karibu mapendekezo yote ambayo Jaji Warioba aliyaingiza kwenye rasimu.

Amebadili mapendekezo ya wananchi ya kutaka kuwa na muundo wa Muungano wa Serikali tatu zilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuunda muundo mpya wa serikali mbili na nusu.

Aidha, Sitta amebariki unyofoaji wa mamlaka ya mahakama ya rufaa; ameiacha mahakama kuu ya Tanzania Bara, kuendelea kuelea na ameingiza mambo ya Tanganyika katika katiba ya Muungano.

Kwa mfano, Sitta ameanzisha muundo mpya wa Bunge. Ametaka kuwapo na mabunge matatu – Bunge la Jamhuri; Bunge la Tanzania Bara (Tanganyika) na Bunge la Zanzibar.

Lakini papo hapo amezuia kuwapo serikali ya Tanganyika. Wadadisi wa masuala ya siasa wanahoji kama kazi moja kuu ya Bunge ni kusimamia serikali, bunge la Tanganyika lisilokuwa na serikali litamsimamia nani?

Kwa mujibu wa Sitta, bunge la Tanganyika litaundwa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoka Tanzania Bara (Tanganyika). Wabunge hawa watakutana wakati Bunge la Jamhuri linaendelea na vikao vyake; wabunge kutoka Zanzibar watazuiwa kushiriki vikao vya Bunge la Tanganyika.

Huu ndio ubaguzi ambao Othuman amegoma kushiriki. Ndani na nje ya vikao Othuman ameasa wenzake kuacha kuchana rasimu ya wananchi. Hakusikilizwa!

Alitahadharisha juu ya kubadili maudhui yenye msingi wa muundo wa serikali tatu; kuhariri; kunyofoa; kukusanya upya maoni na kuchomeka mapendekezo mapya.

Hatua ya Othuman kujiondoa katika kamati, kunatoa ujumbe ufuatao: Mosi, amethibitisha kuwa hayuko tayari kuwapelekea wananchi kile ambacho hawakukipendekeza. Pili, Katiba inayotungwa bungeni, imekosa uhalali kisheria na kisiasa.

error: Content is protected !!