May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Katiba mpya: Askofu Shoo, Dk. Lwaitama wamkingia kifua Rais Samia

Dk. Azaveli Lwaitama

Spread the love

 

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo na Dk. Azaveli Lwaitama, wamewaomba Watanzania wampe muda Rais Samia Suluhu Hassan, ajipange juu ya namna ya kuufufua mchakato wa upatikanaji katiba mpya. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Askofu Shoo na Dk. Lwaitama wametoa ombi hilo leo Jumatano tarehe 21 Aprili 2021, katika mdahalo wa kukuza uelewa kwa Watanzania kuhusu mchango wa Katiba, katika kukuza na kustawisha uhuru wa maendeleo ya nchi.

Dk. Lwaitama ambaye aliwahi kuwa Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na Askofu Shoo, wametoa wito huo wakati wanazungumzia kauli ya Rais Samia kuhusu maombi la wanasiasa, wanaharakati na Watanzania, juu ya ufufuaji wa mchakato huo, ambapo aliwataka wasubiri kidogo.

Akizungumzia kauli hiyo, Askofu Shoo amesema Rais Samia anahitaji muda wa kujipanga kwa kuwa hana muda mrefu tangu alipoingia madarakani kuiongoza awamu ya sita. Aliapishwa, tarehe 19 Machi 2021.

Askofu Frederick Shoo, Mkuu wa Kanisa la KKKT

Rais Samia alichukua nafasi ya Hayati, John Pombe Magufuli, aliyefariki akiwa madarakani tarehe 17 Machi 2021, na kuzikwa nyumbani kwao Chato tarehe 26 Machi 2021.

“Lakini namuelewa rais kwa sasa anaposema tusubiri kidogo, ni kweli hata kama anayo nia hiyo ni mapema mno kusema kwamba tuanze sasa hivi. Katika upya huu, kuna mambo anahitaji kuyaweka sawa kama kiongozi wa nchi,” amesema Askofu Shoo.

Hata hivyo, Askofu Shoo amesema subira hiyo isichukue muda mrefu, kwani Taifa linahitaji Katiba mpya.

“Wakati umefika au tuseme tumuombe sana rais, hii subiri kidogo isije ikawa muda mrefu. Mapema ikiwezekana turejee kwenye mazungumzo, pale ambapo tumeishia katika Rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba,” amesema Askofu Shoo.

Kwa upande wake Dk. Lwaitama, amewaomba Watanzania wasimkwaze Rais Samia kuhusu suala hilo, bali wamuunge mkono akisema kwamba, huenda anakabiliwa na wakati mgumu ndani ya chama chake cha CCM.

“Bahati nzuri, awamu ya sita imesema tusubirie, ile awamu ya tano ilisema hili suala halipo kwangu alitumia hako kaupenyo. Nasi tusubiri sababu kuna mnyukano mkali kwenye chama chake. Tusimkwaze, tumsaidie na yeye,” amesema Dk. Lwaitama.

error: Content is protected !!