January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Katiba inaandikwa kwa mtutu wa bunduki

Viongozi wa Umoja wa wadai Katiya ya Wananchi (UKAWA), (kutoka kushoto) Freeman Mbowe, Prof. Ibrahim Lipumba na James Mbatia

Spread the love

KATIBA Mpya ya Jamhuri ya Muungano, sasa inaandikwa kwa nguvu ya mtutu wa bunduki, MwanaHALISI Online linaweza kuripoti.

Taarifa kutoka mjini Dodoma zinasema, maeneo yote yanazonguuka jengo la Bunge yamezingirwa na vikosi vya jeshi la polisi vilivyobeba mtutu wa bunduki, ili kukabiliana na wananchi wanaopinga bunge hilo kuendelea na shughuli zake.

Aidha, jeshi la polisi lilobeba mbwa; farasi; maji washawasha na virungu, wamekuwa wakiendesha operesheni mitaani kukamata mamia ya wanachama na wafuasi wa upinzani wanaopinga kuendelea kwa mchakato wa katiba.

Upinzani dhidi ya Bunge Maalum la Katiba umeibuka muda mfupi baada ya Samwel Sitta, mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, kunyofoa maoni ya wananchi yaliyowasilishwa katika bunge hilo na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Tayari mwenyekiti huyo wa Bunge Maalum amejiapiza kuwa Katiba Mpya ya Jamhuri, itatengenezwa ndani ya Bunge na siyo nje ya ukumbi huo.

Maapizo ya Sitta yameibuka kufuatia upinzani mkali kutoka vyama vinavyounda Muungano wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA); madhehebu ya kidini ya Kikristo (CCT); Tume ya Mabadiliko ya Katiba na asasi za kiraia, zilizoapa kutetea rasimu ya wananchi kufa au kupona.

Waraka wa CCT umesema, Bunge Maalum la Katiba, haliwezi kuleta Katiba Mpya; badala yake litaishia kukwamisha matarajio ya wananchi ya kupata katiba bora.

Tamko la madhehebu hayo limetolewa na fungamano la majukwaa manne ambayo ni: Christian Council of Tanzania (CCT); Tanzania Episcopal Conference (TEC); The Council of Pentecostal Churches of Tanzania (CPCT); na The Seventh Day Adventists (SDA).

Limesema, Bunge Maalum la Katiba “…halijadili rasimu ya Katiba kama ilivyowasilishwa bungeni na Jaji Warioba.”

Linajadili Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM); ambayo sasa inaitwa, “Rasimu ya Katiba.”

MwanaHALISI Online limeelezwa chochote kitakachotokana na mchakato huu wa kimabavu hakikubariki na hakiwezi kupata uhalali wowote wa kisiasa.

Akizungumza na MwanaHALISI mwishoni mwa wiki, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendelezo (CHADEMA), Tundu Lissu amesema, katiba huandikwa kwa njia ya maridhiano; katiba haindikwi kwa ubabe au mabavu ya vyombo vya dola.

“Tulipenda kuwa na katiba mpya, lakini ambayo ingepatikana kwa mchakato huru. Kupata katiba kwa ubabe na vitisho vya vyombo vya dola, kutaifanya kukosa uhalali,” ameeleza.

Amesema jeshi la polisi limetanda kila mahali, wakiwa na silaha kali kwa lengo la kuzuia maandamano na mikutano ya wananchi wanaopinga mchakato huo, jambo ambalo kwa maoni yake, ni kinyume cha sheria.

Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na wakili wa Mahakama Kuu amesema, “Watanzania wote ni mateka na Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vyote vya dola vyenye mabavu, hii ni wazi kuwa katiba mpya inatengenezwa kwa mtutu wa bunduki.”

Lissu amewataka wananchi wote wenye nia njema na taifa lao, kupinga nchi yao kuwa chini ya utawala wa kijeshi usio rasmi.

Amemtuhumu rais Jakaya Kikwete kuwa wakati nchi iko katika hali tete kama hii, “…rais amekimbia nchi na kwenda Marekani kwa ziara ya wiki mbili ili kukwepa majukumu yake.”

Akizungumzia upigaji kura kwa njia ya mtandao, Lissu amesema, “Huo ni uchakachuaji wa Rasimu ya Katiba; kitendo ambacho hakikubariki kwa mujibu wa sheria.”

Amesema, “Kwa njia ya upigaji kura wa namna hii, chochote kitakachotolewa na Bunge Maalum kwa sura ya Katiba inayopendekezwa, kitakuwa batili kisheria.”

“ Tunawaomba wanachama na viongozi wote wa vyama vinavyoundwa muungano wa UKAWA kufanya maandalizi ya kupinga vitendo hivi kwa njia mbali mbali za kidemokrasia. Kuruhusu katiba ya nchi kuandikwa kwa mabavu, ni kutaka kuhalalisha matumizi ya nguvu katika nchi ambayo inajiita ya kidemokrasia,” ameeleza Lissu.

Aliwaomba viongozi wanaounda UKAWA kufanya maandalizi ya kutosha ya uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu, ili kurahisisha kazi ya kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika utawala wa nchi mwaka 2015.

Tangu Bunge Maalum la Katiba lianze kujadili katiba mpya, kumeibuka upinzani mkubwa miongoni mwa jamii kuhusu mchakato huo.

Makala hii imeandikwa na Sarafina Lindwino

error: Content is protected !!