
KATA tano katika Jimbo la Segerea jijini Dar es Salaam, zinakabiliwa na changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara za mitaa, hali inayosabisha wananchi wake kukosa huduma za kijamii. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Hayo yameelezwa jana tarehe 19 Juni 2021 na Mbunge wa Segerea (CCM), Bonnah Kamoli, katika ziara ya kikazi ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, David Silinde, alipotembelea kwenye jimbo hilo kukagua miundombinu ya barabara.
Kamoli alizitaja kata hizo ni, Bonyokwa, Kisukuru, Tabata, Kimanga na Kipawa.
Mbunge huyo wa Segerea alisema, barabara za kata hizo hazipitiki katika majira yote ya mwaka, iwe wakati wa mvua au wa jua. Na kuiomba Serikali ifanye hima kuzikarabati ili kuwaondolewa changanoto ya usafiri wananchi wake.

Naye Diwani wa Kata ya Tabata, Omary Matulanga, alimuomba Silinde afikishe kilio hicho Serikalini, ili barabara hizo zifanyiwe marekebisho, hasa ya Tabata Mwananchi, inayounganisha maeneo mengi ya jimbo hilo.
Matulanga aliiomba Serikali iijenge barabara hiyo kwa kiwango cha lami, ili isaidie kuondoa foleni katika Barabara ya Ally hassan Mwinyi.
Akijibu maombi hayo, Silinde alisema Barabara ya Tabata Mwananchi kwenda Tabata Kimanga na maeneo mengine, ipo katika Mradi wa Uendelezaji wa Mkoa wa Dar es Salaam (DMDP), awamu ya tatu, hivyo kupitia mradi huo itawekewa lami.

Aidha, Silinde aliuagiza Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA), kufanya upembuzi katika barabara hiyo, ili kubaini sehemu inayohitajika kwa ajili ya ujenzi wake.
Silinde aliagiza tathimini hiyo ifanyike ili wananchi wanaomiliki ardhi karibu na barabara hiyo, wapatiwe taarifa mapema kwa ajili ua kujiandaa na kuondoa usumbufu, pindi watakapohitajika kuachia maeneo yao.
More Stories
ACT-Wazalendo yasema bei ya vyakula imepaa, yatoa mapendekezo
CCM yataka viingilio Sabasaba vipunguzwe
Mahakama yasema uamuzi kesi ya kina Mdee haujakamilika