Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kasoro sheria za uchaguzi Tanzania zabainishwa 
Habari za Siasa

Kasoro sheria za uchaguzi Tanzania zabainishwa 

Mwenyekiti wa WFT, Profesa Ruth Meena
Spread the love

WAKATI  michakato ya kuwapata wagombea ndani ya vyama vya siasa watakaoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2020 nchini Tanzania ukiendelea, wito umetolewa kwa vyama hivyo kuzingatia usawa wa kijinsia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumatatu tarehe 18 Mei, 2020 na Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi chini ya uratibu wa Mfuko wa Udhamini wa  Wanawake Tanzania (WFT) wakati ukitoa mrejesho wa uchambuzi wa sheria tano za uchaguzi kwa mrengo wa jinsia.

Vyama mbalimbali vya siasa nchini Tanzania vimekwisha kuanza kuwataka wanachama wao kujitokeza kutangaza nia ya kugombea udiwani, ubunge na uwakilishi upande wa Zanzibar.

Akitoa mrejesho huo, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwa njia ya mtandao ‘video conference,’ Mwenyekiti wa WFT, Profesa Ruth Meena amesema malengo mahususi ya uchambuzi huo ni kutoa muhtasari wa mambo yaliyojitokeza kwenye baadhi ya sheria za uchaguzi ili kubainisha mapengo yanayoweza kuwa kikwazo katika kutekeleza azma ya ujenzi wa demokrasia shirikishi kwa mlengo wa jinsia.

Profesa Ruth alisema uchambuzi huo uliwawezesha kutoa mapendekezo mahususi yatakayoongoza wadau mbalimbali katika kuchukua hatua stahiki zenye kukabiliana na sheria za ubaguzi wa aina zote hususani ubaguzi wa jinsia kwenye mchakato wa uchaguzi.

Seria zilizochambuliwa ni pamoja na:

  • Sheria ya  Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 ya 2015.
  • Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar namba 4  (2018).
  • Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa namba 4 ya mwaka 1979 namba 292 kama ilivofanyiwa marekebisho mwaka 2010 na mwaka 2015.
  • Sheria ya  Serikali Za Mitaa ( Mamlaka za Wilaya Sura 287 kama ilivyorekebishwa 2002).
  • Sheria za Serikali za Mitaa za mmlaka za miji sura ya 288 na mamlaka za wilaya sura ya 287.

Profesa Ruth amesema, mfumo wa uchaguzi unaongozwa na dhana ya “mshindi anapata yote” yaani “the winner gets all” hauko rafiki kwenye uwakilishi wa makundi yote na demokrasia shirikishi.

“Takwimu toka nchi nyingi zinazotumia mfumo huu zinaonyesha kwamba ufikiaji wa azma ya usawa wa jinsia ni mgumu sana,” amesema.

Katika eneo la uwazi kwenye uteuzi, Profesa Ruth amesema, taratibu za uteuzi ndani ya vyama haziko wazi, kwenye mfumo wa uteuzi, hasa kwenye kuzingatia msingi wa usawa wa kijinsia.

Amesema sheria ziko kimya kwenye kuwajibisha vyama vinavyokiuka sharti la usawa wa jinsia katika uteuzi wa wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uchaguzi.

“Sheria haijatoa meno kwa Tume ya Uchaguzi (NEC) kuwajibisha vyama vya siasa, ambavyo kwenye uteuzi, hawazingatii usawa wa jinsia kwenye uteuzi wao,” amesema Profesa Ruth.

Amesema, uteuzi wa wagombea ni msingi wa kupata wagombea wenye sifa na hatimaye viongozi bora.

“Mapungufu yaliyopo ni wagombea wote, kwenye mchakato wa uchaguzi, lazima wawe ni wanachama wa vyama vya siasa, na wawe wamependekezwa na vyama husika,” amesema.

Amevitaja vifungu hivyo ni; kifungu cha 26 (2) (d) cha Katiba ya Zanzibar – 2018 na kifungu cha 36 cha Katiba ya Jamhuri (1977).

“Kwenye muktadha unaoongozwa na mfumo dume ndani ya vyama vya siasa, na uongozi usio na utashi wa kuzingatia usawa wa jinsia, sharti hili huwaumiza wanawake zaidi,” amesema Profesa Ruth

Amesema, takwimu za chaguzi zote zinaonesha jinsi vyama vinavyobagua wanawake kwenye uteuzi.

Ametolea, mfano ni mwaka 2015 asili mia ya  wagombea viti vya ubunge (wanawake) ilikua kama ifuatavyo: ACT- Wazalendo (15%); CUF (11%); CCM (9%) na CHADEMA (6%). Hali hii inaonesha kutokuwepo na utashi wa siasa wa kutekeleza azma ya ujenzi wa demokrasia shirikishi kwa mlengo wa jinsia.

Amesema azma ya kuwepo kwa viti Maalum imetumiwa kwa njia iliyoingiza ubaguzi kati ya wajumbe wa kuchaguliwa majimboni na wale wanaoingia bungeni kwa kuteuliwa viti Maalum.

“Mbunge wa viti maalum hawezi kuchaguliwa kuwa waziri mkuu, hapewi fedha za jimbo (kwa ajili hawakilishi jimbo) na hubaguliwa kuingia kwenye kamati mbalimbali za Bunge. Kuna haja ya kuboresha Sheria za Viti Maalum ambavyo kimsingi hupewa wanawake,” amesema.

Akigusia gharama za uchaguzi, Profesa Ruth amesema, sheria zinatoa sharti la kuweka dhamana ya kiwango fulani cha pesa kwa wagombea, kwa mfano kiwango cha shilingi million moja kwa rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania na million mbili kwa mgombea kiti cha Urais Zanzibar.

“Viwango hivi ni kikwazo cha wanawake wenye uwezo wa uongozi, lakini hawana uwezo wa kifedha,” amesema.

Akijibu swali la waandishi waliotaka kujua, baada ya uchambuzi huo kipi kitafuata, Profesa Ruth amesema, hatua hiyo imewasaidia kuwapatia nyezo za kutetea na kubadili sheria na vile vile kubadilisha taratibu.

“Tumewapa mrejesho makundi mbalimbali ikiwamo wabunge ili kuona hayo mapengo na jinsi ya kuyafanyia marekebisho,” amesema Profesa Ruth.

Naye Bernadetha Fuko, Mratibu WFT amesema, tayari wametoa mrejesho wa kile walichokibaini kwa wabunge, chama cha wanawake wa serikali za mitaa na Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), asasi za kirai na watafanya hivyo kwa NEC.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!