August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kasi ya kipindupindu yaongezeka

Spread the love

KASI ya ugonjwa wa kipindupindu katika wiki iliyopita imeongezeka kutoka wagonjwa 138 walioripotiwa kuanzia tarehe 1 Mei mwaka huu hadi 9 na kufikia 212, anaandika Regina Mkonde.

Akizungumza na MwanaHALISI Online Nsachris Mwamwaja, Ofisa Habari wa Wizara ya Afya kwa niaba ya Dk. Ummy Mwalimu ambaye ni waziri wa wizara hiyo leo jijini Dar es Salaam amesema, idadi ya vifo pia imeongezeka.

“Takwimu za wiki iliyopita kuanzia tarehe 9 hadi 15 Mei 2016 zinaonesha kuwa kasi ya ugonjwa imeongezeka kidogo ambapo idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa wiki hiyo ni 212 ikilinganishwa na 138 walioripotiwa wiki iliyotangulia (Mei, 2 hadi 8, 2016),” amesema Mwamwaja.

Aidha, idadi ya vifo vitokanavyo na kipindupindu pia imeongezeka katika wiki hiyo ambapo viliripotiwa vifo vitano ikilinganishwa na vifo viwili vya wiki iliyotangulia.

“Wiki iliyoanzia tarehe 9 hadi 15 Mei 2016, jumla ya mikoa minane imeripoti ugonjwa wa kipindupindu. Mikoa hiyo ni Morogoro (78), Lindi (51), Manyara (42), Dar es salaam (16), Mara (8), Pwani (8), Kilimanjaro (6) na Kagera (3),” amesema.

Amesema Mikoa minne kati ya hiyo iliripoti vifo vilivyotokana na ugonjwa wa kipindupindu; Lindi (2), Morogoro (1), Mara (1) na Kagera (1).

“Halmashauri zilizoongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi katika wiki hiyo iliyopita ni Kilwa (51), Kilosa (47), Babati Vijijini (33), Mvomero (23), Kinondoni (10), Mbulu (9), Kibaha Mjini (8), Morogoro Mjini (8), Tarime Mjini (8), Same (6), Temeke (6) na Bukoba Mjini (3),” amesema Mwamwaja.

Halmashauri nne ziliripoti vifo vilivyotokana na ugonjwa huu; Kilwa (2), Mvomero (1), Tarime Mjini (1) na Bukoba Mjini (1).

“Kwa bahati nzuri, ugonjwa wa Kipindupindu hadi sasa haujaripotiwa kutoka mikoa ya Njombe na Ruvuma,” amesema.

Wizara imesema kuwa, hadi kufikia tarehe 15 Mei 2016, jumla ya wagonjwa 21,477 wametolewa taarifa, na kati ya hao 338 wamepoteza maisha.

Aidha, wizara imeendelea kuisistiza jamii Kujenga na kutumia vyoo bora ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huu,Kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutumia choo na baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia.

Pamoja na Mamlaka za maji zilizopo nchini zihakikishe upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi,Kufikisha wagonjwa wa Kipindupindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu.

Watumishi wa afya kutoa takwimu sahihi na kamili za ugonjwa kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Wizara

error: Content is protected !!