Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kashfa ya ufisadi yamng’oa Lugola
Habari za SiasaTangulizi

Kashfa ya ufisadi yamng’oa Lugola

Spread the love

KASHFA inayohusu mkataba wa ununuzi wa vifaa vya kutumika ndani ya Jeshi la Magereza nchini imechochea kujiuzulu kwa Waziri Kangi Lugola. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa mujibu wa Rais Dk. John Magufuli, aliyekuwa kwenye hafla ya makabidhiano ya nyumba za askari wa jeshi hilo, Ukonga, jijini Dar es Salaam leo, watendaji kadhaa wa wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, wamefanikisha kusainiwa kwa “mkataba wa kifisadi” na hivyo waziri Lugola kulazimika kujiuzulu.

Rais Magufuli amesema anampenda Lugola na kwamba ni mwanafunzi wake, licha ya mwili wake ulivyo (mkubwa), lakini kwa hilo “nimeridhia ajiuzulu.”

“Sina urafiki kwenye kazi,” alisema Rais Magufuli kuhusu Lugola, mbunge wa Mwibara, mkoani Mara ambaye alimteua kushika wadhifa huo Julai mosi 2018 kuchukua nafasi ya Mwigulu Nchemba, mbunge mkoani Singida.

Mkataba huo, amesema Rais Magufuli, ni wa thamani ya zaidi ya Sh. 1 trilioni; zikihusisha na kuchukua mkopo, ambao anasema, “hakuna ruhusa ya Wizara ya Fedha na Mipango.”

“Ninajua leo hapa Waziri wa Mambo ya Ndani haonekani (alikuwepo), ameshaleta barua ya kujiuzulu na nimemkubalia, na nimempongeza kwa kutambua hilo.

“Lakini kitu kikubwa ni nini? Ni watu kukosa uadilifu. Hivi karibuni kulikuwa na mkataba wa ajabu unatengenezwa Wizara ya Mambo ya Ndani, wenye thamani ya EURO milioni 408,” amesema.

Amesema wizara hiyo imekosa uadilifu kwa kuwa (watendaji) walidiriki kuingia mkataba wenye thamani ya Euro milioni 408, “bila ya kupangwa katika bajeti na kupitishwa na Bunge.”

“Umetayarishwa na kusainiwa na kamishna jenerali wa Fire (Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji), haujapangwa kwenye bajeti, (wala) haujapitishwa na Bunge.

“Wakati wa vikao, kuna kampuni moja nafikiri kutoka Romania, wahusika wanaokwenda kwenye majadiliano, wanalipwa allowance (posho), bado ya kulipiwa kwenye tiketi za ndege. Mradi wa ovyo wameusaini,” amesema.

Akifafanua dosari za mkataba huo, Rais Magufuli amesema, masharti yake yanaibana serikali, pamoja na vifaa vilivyoorodheshwa katika mkataba huo ambavyo vinatarajiwa kununuliwa, havikidhi mahitaji ya nchi.

“Lakini (uwajibikaji kimkataba) ndani unaeleza, ukitaka kuvunja yale yaliyoanza kutekelezwa, lazima yaendelee kutekelezwa. Mimi Lugola nampenda sana, ni mwanafunzi wangu pamoja na mwili wake… lakini katika hili hapana, nilitegemea hata hapa nitakuta hayupo, nasema kwa dhati,” amesisitiza Rais Magufuli.

“Hatuwezi kuendesha nchi kwa misingi ya ajabu namna hii, yanayokwenda kununuliwa mule kwenye mkataba ni ya ovyo, mara drones (ndege isiyo rubani) mara nini.”

Licha ya Lugola kujiuzulu, vigogo wengine wa wizara hiyo waliong’oka kufuatia kashfa hiyo, ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Jacob Kingu na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Tanzania, Thobias Andengenye.

“Kamishna Jenerali Andengenye nampenda sana, ni mchapakazi lakini kwenye hili hapana, nilitegemea hapa awe hayupo. Na ndiyo maana nampongeza Meja Jenerali Kingu aliyekuwa Katibu Wizara Mambo ya Ndani kwa kuwajibika.

“… na hii imempa heshima kwamba angalau ametambua kwamba inawezekana haya hakuyafanya yeye, lakini yeye ni katibu mkuu angewajibika kwa haya,” amesema Rais Magufuli.

Pia Rais Magufuli amesema, Wizara ya Mambo ya Ndani inaongoza kwa kumtesa, kwani inaongoza kwa kuwa na miradi pamoja na mikataba ya ovyo.

“Nimesema kazi ya uongozi saa nyingine ni ngumu, na tuna changamoto nyingi na hasa hii Wizara….  Kama kuna wizara inanitesa, ni hii Wizara ya Mambo ya Ndani. nataka muelewe hivyo Watanzania, inatesa sana,” amesema.

Rais Magufuli amesema katika miaka minne ya utawala wake, tayari tume nne zimeundwa kuchunguza baadhi ya mambo yaliyotendwa kwenye wizara hiyo.

“Tangu tumeingia madarakani katika miaka minne, kuna tume nyingi zimeundwa kwa ajili ya kuchunguza mambo ya ndani, kwa mamiradi ya ovyo ambayo imefanyika, na mimi nilitegemea watu watakuwa wanajifunza,” amesema.

Kwa upande wake Lugola amesema: “Alichokisema Rais Magufuli ni maelekezo, kwa hiyo nitayafuata na kutekeleza maagizo hayo.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!