KOCHA Mkuu wa Mbeya City FC, Kinnah Phiri amesibitisha kuwa mlinda mlango mahiri wa kikosi chake, Juma Kaseja hatakuwepo katika mchezo dhidi ya Simba utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, anaandika Regina Mkonde.
Kaseja hatakuwepo katika mchezo huo kutokana na kuwa nje ya kikosi hicho kutokana na kulazimika kuwa karibu na familia yake baada ya kupata watoto mapacha hivi karibuni, japokuwa alitarajiwa kuripoti leo kambini Morogoro.
Kocha Phiri amethibitisha kutomtumia Kaseja katika mchezo huo, kutokana na Kaseja kuomba kuongezewa muda wa kukaa karibu na familia yake ili kushughulikia masuala kadhaa ya kifamilia aliyonayo hivi sasa.
“Wakati anaondoka Mbeya siku tano zilizopita tulikubaliana kuwa ataungana nasi hapa siku ya leo, nimezungumza nae leo asubuhi kuna mambo muhimu ya kifamilia amenieleza hivyo basi nimeamua kumuongezea siku kadhaa za kubaki nyumbani kushughulikia yale yote yaliyopo kwenye familia yake na imani yangu kuwa ataungana na kikosi hivi karibuni,” amesema Phiri.
Juma Kaseja aliondoka jijini Mbeya mara baada ya mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Prisons uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine kufuatia taarifa njema ya mkewe kujifungua watoto mapacha.
Wachezaji wanzeke na uongozi wa Mbeya City kwa ujumla unampongeza Juma Kaseja na kumtakia kila la kheri kwenye malezi ya watoto wake.
More Stories
Injinia Hersi kuanza na uwanja Yanga
Sopu aibuka kinara wa mabao ASFC
Mgunda atoa tahadhari kwa Mayele kesho