May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Karia: Mwakalebela alistahili adhabu kali zaidi

Frederick Mwakalebela, Makamu Mwenyekiti wa Yanga

Spread the love

 

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema, Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Fedrick Mwakalebela alipaswa kupewa adhabu kali kutokana na nyaraka zenye kanuni mbalimbali, alizisaini yeye akiwa katibu mkuu wa shirikisho hilo. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Karia ameyasema hayo leo Jumatatu, tarehe 3 Mei 2021, kwenye mahojiano yake na kituo cha radio cha E-Fm kwenye kipindi cha Joto la Asubuhi na kupigilia msumali kuwa adhabu za kufungia baadhi ya watu kwenye familia ya mpira zinasaidia.

Wakati akielezea sakata la kufungia miaka mitano kwa kiongozi huyo wa klabu ya Yanga, Karia amesema, Mwakalebela ndiye aliyepitisha na kusaini nyaraka zenye sheria hizo wakati akiwa katibu mkuu wa TFF chini ya utawala wa Leodger Tenga hivyo alipaswa kupewa adhabu kali zaidi hii.

Walace Karia, Rais wa TFF

“Mwakalebelea hizi nyaraka zenye kanuni mbalimbali, kazitengeneza yeye na ndio aliyesaini pamoja na Tenga na anajua, kwa hiyo mtu wa namna hii anatakiwa apate adhabu kali zaidi” amesema Karia

Makamu Mwenyekiti huyo wa Yanga, amefungiwa kujihusisha na soka katika kipindi cha miaka mitano na kamati ya maadili ya TFF mara baada ya kushindwa kuthibitisha tuhuma alizozitoa juu ya shirikisho hilo na bodi ya Ligi ya kuwa wanaihujumu klabu ya Yanga.

Taarifa ya kufungiwa kwa Mwakalebela, iliyotolewa na TFF tarehe 2 Aprili 2021, ilieleza adhabu ya kumfungia miaka mitano, kiongozi hiyo imetolewa kwa kuzingatia kifungu cha 73(4) cha kanuni za maadili toleo la 2013 mara baada ya kushindwa kuthibitisha madai hayo.

Mwakalebela alitoa tuhuma hizo tarehe 19 Februari 2021, alipofanya mkutano na waandishi wa habari makao makuu ya klabu ya Yanga na kutoa madai hayo.

Katika hatua nyingine, Karia aliendelea amesema, wataendelea kuwafungia viongozi au mtu yoyote aatakafanya kosa na kwenda kinyume na kanuni pamoja na sheria zilizopo.

“Mkitaka tufanye mnavyotaka ninyi tutarudi kule, itakuwa utawala wa kambale kila mtu ana ndefu mkiona nimewaonea nendeni mkanishtaki maadili,” amesema

error: Content is protected !!