May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Karia atoa onyo mabilioni ya Azam TV

Walace Karia, Rais wa TFF

Spread the love

 

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ametoa onyo kwa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara juu ya matumizi mabaya ya fedha za udhamini wa haki za matangazo kutoka kwa kampuni ya Azam TV na kuahidi kuwachukulia hatua kwa wale wote watakaotumia kinyume fedha hizo. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Karia ameyasema hayo wakati wa hafla ya kuingia mkataba na kampuni ya Azam Media Limited, ambao wanadhamini haki za matangazo kwenye michezo ya Ligi Kuu na kutoa kiasi cha Sh. 225.6 bilioni katika kipindi cha miaka 10.

Hafla hiyo ilifanyika hii leo kwenye Hoteli ya Hayat Regency na kuhudhuliwa na wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Karia alisema kuwa kitendo walichofanya kampuni ya Azam TV kitasababisha wawekezaji wengine kuwekeza fedha nyingi kwenye sekta ya mpira wa miguu nchini na kuwataadharisha viongozi watakaotumia vibaya fedha hizo kuwachukulia hatua ikiwemo kuwafungia.

“Mimi nasema anayependa mpira hili ni tukio la kushangilia walichokifanya Azam, kitasababisha wengine kuweka mzigo mkubwa na hizi hela, sio za kuchezea na zitapoteza watu na wale wanaosema tunafungia watu na tutawafungia sana kwa sababu hizi hela tunataka kuzilinda kuhakikisha zinautumikia mpira,” alisema Karia.

Katika fedha hizo Azam Media itatoa kiasi cha shilingi 22 bilioni, kwa msimu mmoja huku kila klabu ikitarajiwa kupata shilingi 1.4 bilioni kwa msimu mmoja.

Licha ya kutoa fedha hizo kwenye udhamini wa haki za matangazo, Azam Media kupitia kwa Mkurugenzi wake, Tido Mhando alisema kuwa wataenda mbali kwa kutoa nyongeza ya fedha kwa bingwa wa Ligi Kuu kuanzia msimu ujao.

“Ili Ligi Kuu iwe na mvuto zaidi kampuni ya Azam Media imeweka ziada ya fedha kwa kila nafasi kwenye msimamo wa Ligi kila inapofika tamati mathalani kwa msimu mitatu ijayo yaani 2021/22 mpaka 2023/24 bingwa wa Ligi Kuu atapata shilingi 500 milioni kwa msimu.” alisema Tido.

Mgawanyo mwengine wa fedha hizo kwa kuzingatia msimamo wa Ligi itakuwa shilingi 250 milioni kwa aliyeshika nafasi ya pili, shilingi 225 milioni kwa aliyeshika nafasi ya tatu na shilingi 200 milioni kwa timu iliyoshika nafasi ya nne.

error: Content is protected !!