October 21, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kardinali Pengo umekosea, wengi wape

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo

Spread the love

NANAMSHUKURU Mungu kwa kuniamsha salama, mwenye afya njema na akili timamu. Mnamo tarehe 10 Machi 2015, Jukwaa la Wakristo nchini lilitoa tamko kuhusu Katiba inayopendekezwa na kufikia kuwahamasisha waumini wa dini ya kikristo wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na muda ukifika wapige kura ya hapana kwa katiba pendekezwa bila ya kusita. Anaandika Benedict Kambona … (endelea).

Hapa sijaona ubaya wa maaskofu kuuhamasisha umma wa waumini wao kwa kuwa ziko sababu za msingi walizozitaja, sababu hizi ni zenye ukweli mwingi na ulio wazi.

Hivi ni nani ambaye hakushuhudia matusi, kashfa, lugha za dharau wakati wa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba? Likawa ni Bunge liloshuhudiwa kuwabagua watu na maeneo yao, wako watanzania waishio visiwani Zanzibar walionyanyapaliwa kwa zodo, mipasho na matusi yasiyomithilika?

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, hukumshuhudia Samuel Sitta alivyoushambulia waraka wa maaskofu na kufikia kuuita usio na utukufu?

Hivi ni yepi ya utukufu aliyoyafanya Sitta na Bunge lile ambayo wewe unaweza kuyabariki? Au kwa kauli za Sitta wakati ule hukujisikia lolote kuanzia mwenendo mzima wa Bunge na kauli zake kuhusu maaskofu na waraka wao? Tuambie tuelewe!

Hivi unataka kuuaminisha umma kuwa unaitetea Katiba pendekezwa na Mahakama ya Kadhi? Bwana Yesu ametufundisha tuwe na kauli moja tu kati ya ndiyo na hapana!

Sasa kwa hili jibu ni hapana kama walivyosema maaskofu kwani sababu walizozitaja ni za msingi zisizo mawaa!

Askofu Pengo umesahau kwamba Waislam walihamasishwa wasijitokeze kuhesabiwa wakati wa sensa iliyopita kufikia kuvurugika kwa mchakato ule hadi leo kukosekana kujulikana vyema kwa idadi ya Watanzania? Sidhani kama umelisahau na hilo!

Au pia hujui ya kwamba kuna baadhi ya Waislam wana chuki na ukristo na wanawaza na kutamani nchi ingetawaliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za imani yao? Hebu nitajie ndani ya miaka kumi ni misikiti mingapi imehujumiwa na kuchomwa moto? Na ni masheikh wangapi wameuawa kwa risasi?

Ninakushauri kiongozi wangu wa dini kwa kukuambia kuwa mimi ni mkatoliki toka kuzaliwa, tena ujitambue kuwa wewe ni askofu kama wao waliokaa na kujadili kwa mapana na marefu yake kufikia kutoa majibu ndani ya tamko lile.

Niende mbali kwa kusema hayo uliyotueleza baada ya safari kutoka nchini Italia ni maoni yako binafsi kama Askofu Pengo na niseme hatutoyasikiliza kwani ili katiba iwe nzuri na bora ni lazima yaingizwe yale yaliyoondolewa!

Maaskofu walichokifanya ni kilekile walichokifanya masheikh kwani wao walitamka ya kwamba bila ya uwepo wa kipengele cha sheria ndani ya katiba kitambuacho mahakama ya kadhi basi watawahamasisha waumini wasipige kura ya maoni ya hii katiba pendekezwa!

Baada ya hapo maaskofu wakabaini kuwa kumbe kiu yao kubwa wenzetu Waislam ni mahakama ya kadhi tu na mambo mengine ni bora liende (maoni yangu mimi), je, sasa kuna ubaya gani kwa upande wa maaskofu?

Nadhani waache Wakristo waikatae na wengine wanaoona kuwa maoni ya wananchi yameachwa nje yakabaki ya kuwalinda mafisadi nao waikatae tu mbona Profesa Ibrahim Lipumba amewaunga mkono maaskofu?

Yote hayo ni kwa sababu yeye ni mwananchi anayeguswa na anayetaka mabadiliko na mabadiliko ni lazima! Kwani mabadiliko haya yataletwa na wananchi na miongoni mwao ni sisi.

Tafadhali usituchanganye askofu wangu kama wewe upo upande wa pili endelea tu waache maaskofu wetu wengine waipiganie haki, mbona askofu Desmond Tutu wa Afrika kusini anapigania haki na bado anaendelea kuheshimika kama askofu pia raia na si mwanasiasa!

Maaskofu wetu tupo pamoja nao wasikatishwe tamaa na yoyote kwani maoni ya Askofu Pengo ni yake na ana haki kama Mtanzania! Mwenyezi Mungu awabariki maaskofu wote Tanzania.

Nimalizie kwa kusema kuwa sijatumwa na situmwi na shetani yoyote maana haya niyaandikayo ni kwa akili yangu timamu nikiongozwa na roho mtakatifu.

 

0773-402133

error: Content is protected !!