December 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kardinali Pengo anamnadi mwanasesere!

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo

Spread the love

MWADHAMA Polycarp Kardinari Pengo, amehoji uhalali wa “matakwa” ya Maaskofu wa Tanzania, kama yalivyoelekezwa kwa Serikali na waumini wakristo, kupitia matamko yao mawili kama yaliyotolewa hivi karibuni. Anaandika Deusdedit Kahangwa … (endelea).

Kwanza, Pengo amehoji uhalali wa Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lililotolewa 17 Februari 2015. Na pili, Pengo amehoji uhalali wa Tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania lililotolewa tarehe 10 Machi 2015.

Kardinali Pengo anasema kwamba, kupitia matamko haya mawili, Maaskofu wameingilia haki za waumini wao kuhusiana na uhuru wa dhamiri walizo nazo waumini hawa. Anasema kwamba Maaskofu hawana mamlaka hayo kabisa.

Kwa heshima, napenda kuonyesha kwamba, maoni ya Kardinali Pengo, ambaye ni askofu wangu, yanayo dosari kubwa kwa kuwa, yamekiuka kanuni za kiepistemolojia na kisemantiki katika usanifu na utetezi wa hoja.  

Matamko mawili ya Maaskofu yaliyoongelewa hapo juu yanafanana kwa kuwa yanaongelea mada zile zile. Kati ya mambo mengine, matamko haya yameongelea zoezi la kuipigia kura Katiba inayopendekezwa, mada ambayo ndio kiini cha makala hii.  

Kuhusu zoezi la kupiga kura kwa Katiba Inayopendekezwa, matamko ya Maaskofu hawa yamejenga hoja rasmi ifuatayo:

Mosi, Maaskofu wamedai kwamba, Katiba Inayopendekezwa imepatikana kwa njia za kihalifu, kwani mchakato wake umeendeshwa kwa hila na ubabe. Kwa maoni yao, kupitia Bunge Maalum la Katiba, mchakato wa kupata Katiba mpya uliendeshwa bila kuzingatia uadilifu; dhamiri za wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ziliingiliwa, na wengi wao kulazimishwa kutenda kwa hofu na unafiki; uwazi ulikosekana; sheria haikuzingatiwa; na roho ya sheria yenyewe haikupewa tafakari stahiki.

Pili, Maaskofu wamedai kwamba, bado Katiba Inayopendekezwa haijajibu matakwa na malalamiko ya wananchi kwenye masuala muhimu kama vile muundo wa serikali, miiko na maadili ya viongozi wa umma, haki za binadamu, madaraka ya Rais, na uwiano wa mihimili ya dola.

Kuhusu jambo hili, wanasema, watu wengi wanaelewa wazi kwamba maoni yao waliyoyatoa na yakazingatiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba hayakuheshimiwa na Katiba Inayopendekezwa. Badala yake matakwa ya kisiasa ya watu wachache ndio yamepewa uzito mkubwa katika Katiba Inayopendekezwa.

Na tatu, Maaskofu wamedai kwamba, Katiba Inayopendekezwa haijasambazwa kwa wananchi wengi ili waisome, waichambue na kujiridhisha kama ndicho kitu wanachokitaka au hapana. Kwa maoni yao, sio jambo la busara kuendelea kuwataka watu kupigia kura kitu wasichokijua.

Katika muktadha huu, msimamo na ushauri wa Maaskofu unazo sura mbili. Kwanza wanaishauri serikali kwamba, zoezi la kupitisha Katiba Inayopendekezwa linapaswa kupewa muda zaidi, kwa maana kwamba liahirishwe na kufanyika baada ya uchaguzi mkuu, Oktoba 2015.

Na pili, Maaskofu wanawaomba waumini wao kuona na kuukubali ukweli kwamba, endapo watawala wataendelea kuwalazimisha kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa wakati hawajaisoma na kuieleewa, basi wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi na kupiga kura ya “HAPANA” kwa Katiba Inayopendekezwa.

Kuhusu mapendekezo haya, Tamko la Jukwa la Wakristo, linayo kauli ifuatayo:

“Hivyo basi, Jukwaa linawataka waumini wake wote wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, waisome Katiba Inayopendekezwa na kushiriki kikamilifu vipindi vya elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa na kisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya HAPANA kwa Katiba Inayopendekezwa kwa sababu zilizotajwa hapo juu.”

Na Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki nalo linayo maneno haya: “Tuonavyo sisi, sio jambo la busara kuendelea kuwataka watu kupigia kura kitu wasichokijua. Ikiwa watawala wataendelea kulazimisha, basi wananchi wajitokeze na kupiga kura ya kuikataa Katiba Inayopendekezwa.”  

Siku chache baada ya Maaskofu kutoa mapendekezo haya, Kardinali Pengo alijitokeza mbele ya Wanawake Wakatoliki Tanzani, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, wakati wa kufungua mafungo yao mnamo 14 Machi 2015, katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, na kuyakosoa.

Katika mahubiri yake, yaliyoripotiwa na vyombo vya habari alionyesha kukerwa sana na maneno haya: “Hivyo basi, Jukwaa linawataka waumini wake wote … wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya HAPANA kwa Katiba Inayopendekezwa kwa sababu zilizotajwa hapo juu.”

Kwa hiyo, maneno ambayo ni chimbuko la ugomvi kati ya Kardinali Pengo na Maaskofu ni “Jukwaa linawataka.” Lakini, kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, toleo la pili (Dar es Salaam: Oxford University Press, 2004), neno “taka” linamaanisha “kuwa na hamu au haja ya jambo fulani; tamani, hitaji.”

Na neno “matakwa” linamaanisha “jambo ambalo mtu analitaka; haja, mahitaji, maombi.” (uk. 226). Kwa hiyo, matamko ya maaskofu hayamlazimishi muumini yeyote kutenda kinyume na dhamiri yake. Kardinali Pengo ametenda kosa la kisemantiki hapa.

Kosa hili linaonekana wazi katika matamshi yake, kama yalivyoripotiwa na vyombo vya habari. Kardinali Pengo anasema:

“Nililetewa nakala hizi zilizopo hapa mbele yangu. Barua zote mbili zimetengenezwa kutokana na umakini wa hali ya juu.

“Lakini napenda niseme kwamba, sisi Maaskofu hatuna mamlaka ya kuwalazimisha waamini watende kitu kinyume cha dhamiri yao. Huo ni msimamo hakika kabisa na haiwezekani mtu akaja kwangu akaupinga.

“Pamoja na tafakari nzuri kabisa na mawazo makini yaliyotolewa katika barua hizi, ni kosa kufikia hatua ya kumwambia kila mkristo kwamba itakapofika siku ya kuipigia kura katiba inayopendekezwa upige kura ya hapana.

“Katika maelekezo hayo tutakuwa hatujaheshimu dhamiri za waumini wetu. Na kwa nini tuwafanye hivyo?

“Kwa nini tuwageuze watoto wadogo ambao lazima kuambiwa la kufanya? Hilo ni jambo ambalo linadhalilisha uhuru wa wana wa Mungu ndani ya waamini wetu.

“Sisi Maaskofu hatuna uwezo wala hatuna haki ya kuwaambia mwende mkapige kura ya hapana. Kama mtu anasema tunayo, tumepata wapi haki hiyo? Hilo ni swali muhimu sana.”

Kutokana na maelezo haya ya kardinali Pengo ni maoni yangu kwamba, Kardinali alitengeneza hoja yake, na  kisha akaijibu yeye, lakini akadai kwamba anaijibu hoja ya Maaskofu. Sio kweli. Katika kanuni za usanifu na utetezi wa hoja, kosa alilolifanya tunaliita “straw man’s fallacy.” Hili ni kosa la kunadi “hoja mwanasesere.” Kwa maneno mengine, Kardinali wetu alikururpuka.

Hoja ya Maaskofu ni nzito. Imezingatia kanuni zote za kimantiki na kiepistemolojia. Kwa mujibu wa kanuni hizi, kila kauli duniani husindikizwa na kauli nyingine mbili.

Kwa mfano. Ukisema “Katiba Inayopendekezwa ni mbaya.” Kauli nyingine inayoisindikiza kauli hii ni, “Katiba Inayopendekezwa ni nzuri.” Na kauli ya tatu ni “Ama katiba Inayopendekezwa ni nzuri au ni mbaya.”

Maaskofu wanasema kwamba, “Katiba Inayopendekezwa ni mbaya.” Wametoa ushahidi usio kanushika. Kwa hiyo, kauli nyingine mbili, kama nilivyo zitaja hapo juu, hazina nafasi kwao. Wanawaomba wafuasi wao “kuwaamini” kama ambavyo wanawaamini katika mambo mengine mengi.  

Kama Kardinali Pengo anataka wakristo waamini vinginevyo ajenge hoja.  Aachane na biashara ya kunadi “hoja mwanasesere.”

error: Content is protected !!