May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kapombe azigonganisha Simba, Yanga atengewa Mil 180

Shomari Kapombe

Spread the love

 

KUFUATIA taarifa za beki wa kulia wa Simba, Shomary Kapombe kutaka kutimkia Yanga, baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu uongozi wa klabu yake sasa umeanza kufanya nae mazungumzo ya kumuongeza mkataba mpya. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea). 

Simba imeanza mchakato huo wa kumuongezea mkataba Kapombe, kufuatia taarifa za kuwa klabu ya Yanga imeonesha nia ya kuhitaji huduma ya mchezaji huyo kuanzia msimu ujao wa Ligi, huku taarifa nyingine zikieleza tayari ameshasaini mkataba wa awali na Yanga.

Taarifa za Simba kuanza mazungumzo na mchezaji wao huyo zimethibitishwa na Meneja wa Kapombe, Jemedari Said ambaye amesema mazungumzo na klabu yake ya sasa yanaenda vizuri.

“Pamoja na yote ila tupo kwenye mazungumzo na klabu yake ya sasa ya Simba na mazungumzo yanaendelea na yapo kwenye hatua nzuri,” alisema Jemedari.

Ila taarifa ambazo MwanaHALISI Online imezipata kutoka kwenye chanzo cha ndani cha kuaminika zinaeleza kuwa mchezaji huyo ameshafikia makubaliano ya awali na Yanga na kumtengea kiasi cha Shilingi milioni 180 kama ada ya uhamisho.

“Ninachojua mimi Kapombe ameshakubaliana na Yanga kwa kukubali kiasi cha fedha Sh. 180 milioni, kama ada ya uhamisho na baada ya huyo kuna mwengine anafuata kutoka hapo hapo Simba,” kilisema chanzo hiko.

Katika hilo pia MwanaHALISI Online ilitaka kujua kutoka kwa meneja wa mchezaji huyo kama wameshapokea ofa kutoka kwenye klabu nyingine yoyote juu ya usajili wake.

“Sisi tumepokea ofa nyingi, kuna ofa kutoka Simba, kuna ofa kutoka Farrabati ya Morocco na kuna ofa kutoka kwenye klabu za ndani zinazoshiriki Ligi Kuu,” alisema Jemedari.

Taarifa za mchezaji huyo kutimkia Yanga zinachagizwa na kauli ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa Yanga na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM, Mhandisi Hersi Saidi ya kusema kuwa “Tutaendelea kuijenga Yanga msimu ujao ikiwemo kuvunja benki zinazowahifadhi watu.”

error: Content is protected !!