January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kamukara azikwa kifalme Muleba

Dada mkubwa wa marehemu Kamukara, Joyce akilia kwa uchungu wakati wa kumuaga mdogo wake

Spread the love

HATIMAYE mwili wa Mhariri wa MwanaHALISI Online, Marehemu Edson Kamukara umezikwa leo nyumbani kwao katika kijiji cha Ihangiro, Muleba Kusini, mkoani Kagera. Anaandika Deusdedit Kahangwa, Muleba … (endelea).

Katika mazishi hayo kama ilivyokuwa kwenye shughuli ya kuagwa jijini Dar es Salaam, nako pia kulihudhuliwa na idadi kubwa ya watu ambao kila mmoja wao alionekana kuwa na nyuso ya majonzi ikiwa ishara ya kumlilia marehemu Edson Kamukara.

Mazishi hayo pamoja na kuhudhuliwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa lakini pia yalihudhuliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd, Saed Kubenea ambaye alikuwa mwajiri wake wa mwisho.

Mbali na wanasiasa na mwajiri wake lakini pia mazishi hayo yalihudhuliwa na waandishi wa habari 20 kutoka katika chama cha Kagera Press Club sambamba na maelfu ya waombelezaji.

Ibada ya mazishi ya marehemu Edson Kamukara iliongozwa na mapadre watatu wakiongozwa na Padre Monsinyori Gosbert Byamungu akisaidiwa na Mapadre Process Mutungi na Chrisanth Mugasha wote kutoka parokia ya Rubya katika jumbo la Bukoba, ambapo marehemu alikuwa akisali enzi za uhai wake.

Padre Mugasha katika mahubili yake aliwaambia waombolezaji kuwa marehemu Kamukara alikuwa msema ukweli siku zote bila kujali matokeo yake ukweli anaousema. Hivyo akawaomba kumuenzi kwa kuzingatia kanuni ya ukweli kila wakati, kila mahali na kwa kila mtu.

Kwa mujibu wa hati ya kifo cha marehemu Kamukara, kinaeleza kuwa chanzo cha kifo chake ni kilitokana na mfumo wa hewa kushindwa kufanya kazi vizuri.

Hata hivyo hati hiyo haikusema sababu iliyoufanya mfumo huo kukwama, kitendawili hicho hakikuweza kupata jibu hadi marehemu anazikwa.

Katika salamu zake za rambirambi, Kubenea ameahidi kufanya uchunguzi wa kina kutatua kutendewili hicho, huku akijitolea kuchangia malezi ya mtoto wa marehemu, Egdar Edson.

Marehemu Kamukara alifikwa na mauti Juni 26, 2015 saa 12:30 jioni nyumbani kwake, Mabibo jijini Dar es Salaam, akiwa na umri wa miaka 35, ameacha mtoto mmoja Edgar (miaka minne).

Wakati wa uhai wake marehemu alikuwa mpigania haki za wanyonge, wajane, na watu wasiokuwa na jukwaa lA kusemea shida zao.
Kijijini kwao Ihangiro atakumbukwa kwa kuanzisha wazo la kujenga chumba cha kisasa cha kuhifadhia maiti na kusimamia ujenzi wake hadi mwisho. Baada ya kufariki mwili wake ulihifadhiwa kwenye chumba hicho.

Wasifu wa Marehemu Edson Kamukara

Edson alizaliwa Machi 27, 1980. Alisoma katika Shule ya Msingi Muungano iliyopo Moshi, Kilimanjaro (1990-96), Shule ya Sekondari Majengo iliyopo Moshi, Kilimanjaro (1997-2000) na Kitado cha tano na sita alisoma Shule ya Sekondari ya Umbwe (2001-2003) na elimu ya juu alisoma katika Chuo Kikuu cha St. Augustino (SAUT) (2005-2008).

Amefanya kazi kama mwandishi wa habari katika magazeti ya Majira (2009), Jambo Leo (2010-2011), Tanzania Daima (2012-15), kuanzia mwezi Februari mwaka huu alijiunga na Hali Halisi Publishers akiwa kama Mhariri Mwanzilishi wa gazeti la mtandaoni la MwanaHALISI Online.

error: Content is protected !!