July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kampuni za simu ziisaidie serikali – Waziri Majaliwa

Spread the love

KASSIM Majaliwa, Waziri Mkuu ametaka kampuni zinazotoa huduma za mawasiliano nchini, kuisaidia serikali kubaini wanaotumia simu vibaya. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Majaliwa amesema hayo leo tarehe 30 Aprili 2019 wakati wa kufunga Maadhimisho ya Miaka 10 ya Mfuko wa Mawasiliano kwa wote yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

Amesema, Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuimarisha sekta ya mawasiliano hususani ya simu, data, redio na televisheni kwa kuwa, ni hitaji la msingi na la lazima kwa wananchi na Taifa kwa ujumla, hasa katika kufungua fursa za kiuchumi na kujiletea maendeleo hivyo vitumike katika matumizi sahihi.

“Katika umuhimu huo serikali imeendelea kutekeleza maelekezo ya ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa kuhakikisha, ifikapo mwaka 2020 wananchi wote nchini wawe wamepata mawasiliano ya simu kwani hadi sasa asilimia 94 ya Watanzania wote wanawasiliana kwa njia ya simu nchini kote,” amesema Waziri Majaliwa.

Aidha, ametoa maagizo kwa mfuko wa mawasiliano kwa wote uendelee kubaini maeneo ambayo bado yanachangamoto za mawasiliano nchini, ili serikali iweze kupeleka huduma hiyo mapema iwezekanavyo.

Amesema, mfuko uendelee kufuatilia kwa karibu sehemu zilizojengwa minara ya mawasiliano kwa kutumia ruzuku ya serikali, ili kuhakikisha wananchi katika maeneo hayo wananufaika na upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano.

Amesema, kampuni zinazotoa huduma za mawasiliano ziendelee kushirikiana na mfuko wa mawasiliano kwa wote ili mfuko huo uweze kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

Mhandisi Peter Ulanga, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote amesema, tangu kuanzishwa kwa mfuko huo, umekuwa ukitambua mahitaji ya mawasiliano nchi nzima, kushirikisha wadau mbalimbali wa mawasiliano pamoja na wananchi katika kutatua kero za mawasiliano.

“Wakati Mfuko unaanza takribani asilimia 45 tu ya Watanzania walikuwa wanaishi katika maeneo yanayofikiwa na mawasiliano ya simu, lakini mpaka sasa takribani asilimia 94 ya Watanzania wanaishi kwenye maeneo yanayofikiwa na mawasiliano simu,” amesema Ulanga.

error: Content is protected !!