KAMPUNI inayojihusisha na uandaaji wa mapambano ya ngumi za kulipwa, Hall of Fame Boxing and Promotion, imeiburuza mahakamani Kampuni ya Azam Media, ikitaka ilipwe fidia ya Sh. mbili bilioni kwa madai imerusha maudhui yake katika runinga kinyume na makubaliano. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Kampuni hiyo imefungua kesi ya madai Na. 100/2023 katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, ikidai Azam Media ilikiuka makubaliano ya kimkataba kwa kurusha maudhui kwenye kipindi, yaliyohusu mapambano mawili.

Mapambano hayo ni kati ya bondia Hassan Mwakinyo na rais wa Ufilipino, Arnel Tinampay na la Twaha Kiduku dhidi ya Dulla Mbabe, ambapo Azam Media inadaiwa kuyarusha bila ya kuwa na haki miliki ya maudhui hayo.
Inadaiwa kuwa makubaliano ya kimkataba yaliyokuwepo baina ya wadai hao na Azam Media ni kurusha mapambano hayo mubashara (live) tu, lakini iliendelea kurusha marudio mapambano hayo kwa nyakati tofauti, kinyume na makubaliano.
Kampuni hiyo inadai kurudiwa kwa maudhui hayo kuliendelea kuinufaisha Azam Media jambo ambalo linawasukuma kudai fidia hiyo. Pia, inadai Azam Media imerusha mapambano hayo bila kuweka nembo “logo” yake.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni hiyo ya ndondi, imefikia uamuzi wa kufungua kesi baada ya jitihada za kutafuta suluhu katika mamlaka mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Haki Miliki Tanzania (COSOTA), kutozaa matunda.
Kesi hiyo ya madai inatarajiwa kuanza kusikilizwa mahakamani hapo tarehe 18 Septemba 2023, mbele ya Jaji Mussa Pomo.
Leave a comment