Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kampuni 7 zamuangukia Rais Samia madeni Uchaguzi Mkuu 2020
Habari za Siasa

Kampuni 7 zamuangukia Rais Samia madeni Uchaguzi Mkuu 2020

Spread the love

 

KAMPUNI saba za uchapishaji kutoka Kariakoo, jijini Dar es Salaam, zimekiomba Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilipe kiasi cha Sh. bilioni moja fedha zinazodaiwa kutokana na huduma za sare, mabango kwenye mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumanne, tarehe 26 Aprili 2022 na wawakilishi wa kampuni hizo wakati wakizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam kuhusu madai yao.

Kampuni hizo ni, FRT Printers, Master Samon Digital Print, Total Graphics Solution, Swab Trading Co, Mas General Supply, Mwamakula Production na Print Plus Limited.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Total Graphics, Salum Mussa amemuomba Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati suala hilo, ili walipwe fedha zao na kwamba kama maombi yao hayatafanyiwa kazi, watachukua hatua ya kwenda mahakamani.

“Haki haibembelezwi, sisi tunachotaka ni hela zetu tulipwe, ni hela nyingi kwetu zimetuingiza katika madeni kiasi kwamba huko mitaani tumeonekana matapeli. Kwa hali tuliyo nayo sisi hatuwezi kurejesha fedha tulizokopa hasa ikizingatiwa riba imeongezeka,” amedai Mussa na kuongeza:

“Kampuni zote saba tunadai zaidi ya Sh. bilioni moja, tungeomba CCM waingilie kati tumechoka kwenda Uhuru Media kupeleka malalamiko yetu. Kesho tutapeleka barua ya mwisho kama haitachukuliwa hatua yoyote tutakwenda mahakamani.”

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo

Naye Elifadhar Mdassa, kutoka Kampuni ya Master Samon Digital Print, amedai wamechukua hatua ya kutoka hadharani kudai malipo hayo, baada ya jitihada zao za kutafuta suluhu na Kampuni ya Uhuru Media Group pamoja na uongozi wa CCM, kugonga mwamba.

Amedai, waliwahi kuzungumza na aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Uhuru Media Group, Ernest Sungura, lakini hakutatua suala hilo.

Mdassa amedai kuwa, kila walipowasilisha malalamiko yao walikuwa wanaambiwa hayajafanyiwa kazi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo mabadiliko ya uongozi wa CCM na Uhuru Media Group, yaliyotokana na kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli.

“Tumefanya jitihada kubwa, mbali na kuonana nao ana kwa ana na kuandika barua kuhitaji malipo yetu, lakini hazijazaa matunda kwa sababu mbalimbali ikiwemo tukiambiwa kuna mabadiliko ya hapa na pale,” amedai Mdassa na kuongeza:

“Mara tukaambiwa kuna msiba wa Rais Magufuli… ngoja mtalipwa, muda unazidi kwenda ahadi tunazopewa hazikidhi matakwa yetu. Kimsingi wavae viatu vyetu waone hali tunayopitia ni ngumu.”

Akizungumza katika mkutano huo, Eliatosha Muganyizi, Mkurugenzi wa Kampuni ya FRT Printers, amesema kampuni hizo ziliingia mkataba na Kampuni ya Uhuru Media Group, June 2020, kwa ajili ya kutoa huduma za sare za CCM katika uchaguzi huo.

Muganyizi amedai kuwa, kwa mujibu wa mkataba kati ya kampuni hizo na Uhuru Media Group inayomilikiwa na CCM, walipaswa kulipwa fedha zao ndani ya siku 30 baada ya kutoa huduma, lakini hadi leo baadhi ya kampuni zimelipwa nusu huku nyingine zikikosa kabisa.

“Kuanzia June 2020 tulianza kusambaza sare kama fulana, nembo za chama, key holders. Tulisambaza kwa muda wa miezi mitatu hadi uchaguzi ulipoisha. Mimi kampuni yangu inadai Sh milioni 38 ambapo ukijumlisha na ongezeko la riba ni Sh. milioni 150, hadi sasa sijalipwa naomba nilipwe,” amedai Muganyizi.

Kwa upande wake Elia Susuye Mwangayo, amedai “hadi leo tumefanya kazi ya chama chetu pendwa lakini hatujalipwa. Sisi hatuna ugomvi na chama chetu ila tumeamua kuongea baada ya kuona malalamiko yetu hayafanywi kazi.

Mwangayo amedai kuwa, kutolipwa kwa fedha hizo kumewaletea athari kubwa, ikiwemo baadhi yao kuuza mali ili kulipa madeni huku mwingine aliyemtaja kwa jina la Fredy Mwamakula, akifariki dunia kutokana na msongo wa mawazo wa kudai.

Mtandao huu ulimtafuta Sungura kwa simu, ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, ambaye alijibu akidai hafahamu hilo suala na wala hayuko kazini kwa sasa.

“Hicho kitu sikijui na unajua pia mimi siko kazini, sikijui hicho kitu,” amedai Sungura.

Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa sasa wa Uhuru Media Group, Shabani Kisu na kuulizwa juu ya suala hilo, aliwataka walalamikaji kufika ofisini kwake kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi.

“Waje ofisini, hatuwezi kuongea kwenye simu sababu hivyo vitu ni vya kurithi… waje ofisini tumalize. Mimi niko Dodoma kwenye pilika pilika za siku kuu za Mei Mosi, zikiisha nitakuwepo ofisini waje,” amesema Kisu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

error: Content is protected !!