January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kampeni za Odinga zaingia shubiri

Elgeyo Marakwet Micah Kigen

Spread the love

 

Mwenyekiti wa Chama cha ODM nchini Kenya, Elgeyo Marakwet Micah Kigen amemkosoa kiongozi wake na mgombea urais wa chama hicho Raila Odinga kwa kushindwa kuwajumuisha watu kutoka kabila la Wakalenjin kwenye timu yake ya kampeni za urais. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumza na vyombo vya habari nchini humo, jana tarehe 8 Januari,2022 Kigen amesema alichunguza na kuona kuwa ili kuwepo na sura ya Kenya, ni sharti mwanachama wa jamii ya Kalenjin ajumuishwe.

“Licha ya kwamba Raila alijaribu kuwajumuisha viongozi mbalimbali wa siasa, alishindwa kuwajumuisha Wakalenjin kwenye kikosi chake. Tunamuomba afanye haraka ili kuwe na usawa wa kimaeneo,’ amesema Kigen.

Aidha, aliwataja walioteuliwa kwenye kamati hiyo kuwa ni wapangaji mikakati na wahamasishaji.

“Nimeshawishika kuwa kikosi hicho kitatekeleza majukumu yao ipasavyo ila yeye (Raila) anapaswa kuunda kikosi kingine kitakachomsaidia kuhamasisha watu zaidi kwenye mashina,” Kigen alisema.

Kauli hiyo ya Kigen imekuja baada ya vyombo vya habari nchini humo kuripoti kuwa Raila aliongeza nguvu katika timu yake kwa kuwateua magwiji 11 wa siasa, wakati akijiandaa kuwania urais kwa mara ya tano.

Tarehe 6 Januari, 2022 Raila alizindua timu hiyo yenye wanachama wengine 11 wakiwemo magavana Anyang’ Nyong’o (Kisumu) na Charity Ngilu (Kitui).

Raila ambaye anatokeo kabila la Luo, pia aliwateua maprofesa Peter Wanyande, Makau Mutua na Karuti Kanyinga kuwa washauri wa kampeni zake za urais.

error: Content is protected !!