July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kampeni ya mchango wa mwanamke yazinduliwa

Profesa Saida Yahya Othman (aliyesimama) akichangia mada wakati wa uzindunzi wa kampeni

Spread the love

KAMPENI ya kutambua na kuenzi mchango wa wanawake katika historia ya Tanzania imezinduliwa leo. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa sanaa za jukwaani, Makumbusho ya Taifa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Adelaide Sellema- Kaimu mkurugenzi mkuu wa Makumbusho ya Taifa, amesema “katika historia ya taifa, ni mara ya kwanza kufanya kazi maalum ya kutambua historia ya wanawake katika jamii kwa malengo ya kuweka kumbukumbu sahihi kwa maendeleo ya historia ya Tanzania”.

Amesema, kwenye siasa na harakati za ukombozi wa Tanzania, yanatajwa majina ya Mwani Theresa Ntare- aliyekuwa chifu wa Kasulu aliyesimamia vyema msimamo wa Baraza la Machifu mwaka 1958 na kuunga mkono juhudi za TANU katika kudai uhuru.

“Bibi Titi Mohamedi ambaye alikuwa kiongozi wa TANU- Women Wing aliweza kutengeneza historia ambayo sio rahisi kufikiwa au kuvujwa na kiongozi wa vyama vya siasa katika mazingira ya sasa,” amesema Sellema.

Ameongeza kuwa yupo pia Sophia Mustapha (mwenye asili ya Ki- asia) ambaye pamoja na sera za kibaguzi, zilizokuwa zimewekwa na wakoloni za kuwabagua raia kwa misingi ya rangi, aliamua kuunga mkono juhudi za TANU na alishiriki siasa na hatimaye kuingia katika baraza la kutunga sheria.

“Wapo wanawake wengi ambao hawakuwa katika mrengo wa siasa lakini wameweza kuandika historia katika nyanja mbalimbali. Lakini zimeandikwa kwa ufupi,” ameongeza Sellema.

Aidha, Lilian Liundi – Mkurugenzi mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania, amesema dhima ya kampeni hiyo ni “Uthubutu wa mwanamke na miaka 54 ya maendeleo ya Tanzania” huku kaulimbiu ikiwa “Mwanamke, Historia yetu, fahari Yetu”.

“Taarifa zitakazokusanywa zitatumika kuwaenzi wanawake kama sehemu ya kuhamasisha vizazi vya sasa na vijanvyo umuhimu wa ushiriki wa wanawake katika maendeleo endelevu.

“Kuendeleza mijadala kuhusu michango na ushiriki wa wanawake na kudai uelekezaji wa rasilimali kutoka kwa wadau mbalimbali katika kuendeleza ushiriki wanawake na kuwaenzi,” amesema Liundi.

Kampeni hiyo itachukua muda wa miaka mitatu. Inatarajiwa kuhusisha wadau mbalimbali wakiwemo TGNP Mtandao, Makumbusho ya Taifa, Women Research Development Project, Women Fund Tanzania (WFT), Soma na shule ya uandishi wa habari ya RAIDA.

error: Content is protected !!