Tuesday , 16 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kambi Maalim Seif waiangukia mahakama
Habari za SiasaTangulizi

Kambi Maalim Seif waiangukia mahakama

Spread the love

WABUNGE wa Chama cha Wananchi (CUF), wamelalamikia hatua ya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, kuchelewa kutoa maamuzi kwenye mashauri kadhaa yaliyofunguliwa na watu mbalimbali juu ya “mustakabali” wa baadaye wa chama hicho. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Mnadhimu wa wabunge hao, Ally Salehe, amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, kuchelewa kutolewa maamuzi kwenye mashauri hayo, kumesababisha athari kubwa ndani ya chama hicho.

Kuna kesi imeahirishwa kutolewa hukumu kwa zaidi ya mara tatu. Jambo hili limeliathiri sana chama chetu, ikiwa ni pamoja na kushindwa kufanya uamuzi wa kiungozi,” ameeleza.

Salehe ambaye ni mbunge wa Malindi Unguja amesema, “siyo lengo letu, na wala hatukusudii, kuingilia taratibu za mahakama; na au kutoa shinikizo la aina yoyote lile kwa mahakama. Isipokuwa kwa kweli, tumepata mashaka makubwa namna shauri hili lilivyoahirishwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu.”

Anasema, “mashaka yetu yanatokana na sababu zilizoelezwa mahakamani siku ya hukumu, kwamba maamuzi hayatatolewa kwa sababu Jaji amepangiwa majukumu mengine.

“Hofu zaidi ikaja pale ilipoonekana kuwa tarehe 17 Machi 2019 aliyoitaja pale katika ukumbi wa Mahakama ambayo ni siku ya Jumapili.”

Katika shauri hilo, bodi ya wadhamini ya CUF inaomba mahakama kumtangaza Prof. Lipumba kuwa siyo mwenyekiti wa chama hicho; kuondoka kwenye ofisi za Buguruni na kurejesha mali zote za chama ambazo anazimiliki kinyume cha sheria.

CUF kimetumbukizwa kwenye mgogoro mkubwa wa uongozi na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francies Mutungi, kufuatia hatua yake ya kumrejesha madarakani, kinyume na sheria, aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba.

Prof. Lipumba alijiuzulu uenyekiti wa chama hicho kwa hiari, kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu –  tarehe 6 Agosti 2015 – kwa maelezo kuwa amekosa ushirikiano na viongozi wenzake.

Aliwaambia waandishi wa habari wakati huo, kwa namna chama kinavyokwenda, nafsi yake inamsuta kuendelea kuwa kiongozi.

Akatangaza kung’atuka na kudai kuwa atabakia kuwa mwanachama muaminifu wa CUF na iwapo chama chake kitaridhia, anaweza kuwa mshauri wake.

Prof. Lipumba alishikilia uamuzi wake wa kujiuzulu licha ya kuombwa kutofanya hivyo na viongozi wenzake wa juu akiwemo Maalim Seif Shariff Hamad.

Baadaye alirejea kwenye nafasi hiyo kwa msaada wa Jaji Mutungi, akidai kuwa ametengua maamuzi yake.

Mbele ya waandishi wa habari, mbunge huyo amesema, Prof. Lipumba, ni kikwazo katika mkakati wa chama hicho wa kujisuka upya kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye uchaguzi mkuu wa mwakani.

Anasema, namna kesi ilivyoahirishwa na tarehe iliyopangwa, imeibua zaidi maswali miongoni mwao na kwamba, mazingira hayo yanawasukuma kuwa na hisia mbaya.

Wabunge hao wameiomba Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kuhitimisha shauri Na. 23/2016 linalohoji uhalali wa uenyekiti wa Prof. Lipumba ili chama hicho kipumue.

“Maswali yamekuwa mengi miongoni mwetu na kwa kweli huwezi kuepuka hisia mbaya kwa wanachama na viongozi wetu kutokana na kauli alizozitoa Profesa Lipumba alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari siku moja kabla ya hukumu, na hicho kilichotokea,” amesema.

Pia wabunge hao wamemuomba Jaji Mkuu wa Tanzania, Ibrahim Juma na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Ferdnand Wambali, kufuatilia kwa karibu shauri hilo kwa kuwa uamuzi wake utawezesha kuifanya CUF itimize wajibu wake wa kikatiba na kisiasa katika siasa za ushindani za Tanzania.

“Chama kimekosa kuwa na Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti toka mwaka 2015, tunahitaji kufanya chaguzi za ndani kujaza nafasi hizi na nyingine,” amesema Saleh.

Aidha, Saleh ametaja athari ilizopata chama CUF tangu mgogoro wa kiuongozi wa chama hicho uanze kuwa, ni pamoja na kupoteza rasilimali fedha katika kugharamia mashauri yaliyoko Mahakama Kuu, baadhi ya wabunge wake kuondolewa bungeni na madiwani kuvuliwa uanachama.

“Madhara na athari ya mgogoro huu uliopandikizwa ni kubwa sana kwetu kama wawakilishi wa wananchi na kwa chama kwa ujumla. Nikitaja machache ni kupoteza wabunge, madiwani na wenyeviti wa mitaa hata katika maeneo ambayo kichama tuko imara.

“Viongozi wa chama kuondolewa kwenye nafasi zao. Kuibwa kwa fedha za ruzuku zaidi ya Shilingi 1.5 bilioni na uharibifu wa mali za chama zikiwemo magari, majengo na chama kushindwa kuendesha shughuli zake kwa utulivu,” amesema Saleh.

Ameeleza kuwa, mgogoro huo unavuruga mipango ya chama hicho na hata kushindwa kujiandaa kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2020.

Mahakama hiyo ilipanga kusoma hukumu katika shauri lililofunguliwa na Bodi ya Wadhamini ya chama hicho kupinga Prof. Lipumba, kuwa mwenyekiti wake tarehe 22 Februari 2019.

Hata hivyo, Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Sharmillah Sarwatt, aliwaambia viongozi, wafuasi na wanachama wa chama hicho, waliofurika kwenye ukumbi wa wazi Na. 1 (Open Court Room One), kuwa hukumu hiyo sasa itasomwa tarehe 17 Machi 2019.

Alisema, sababu za kusogezwa mbele kwa uamuzi huo, unatokana na Jaji Dk. Benhajj kupangiwa majukumu mengine nje ya ofisi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia amfariji mjane wa Musa Abdulrahman

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan leo Jumanne amempa pole Mwanakheri Mussa...

Habari za Siasa

Nape: Wanasiasa, wanahabari, wafanyabiashara mteteeni Samia

Spread the loveWaziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,...

Habari za Siasa

CAG: TAWA imegawa vibali vya uwindaji bila idhini ya waziri

Spread the loveRIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali...

Habari za Siasa

TAMISEMI yatenga bil. 17.79 kwa ajili uchaguzi serikali za mitaa

Spread the loveWIZARA Ofisi ya Rais-TAMISEMI, imetenga fedha kiasi cha Sh. 17.79...

error: Content is protected !!