January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kambaya ambana mbavu Jecha

Spread the love

BAADA ya kuonekana hajui utaratibu wa sheria, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha amebanwa na CUF aoneshe fomu ambayo Maalim Seif Shariff Hamad alijaza kuingia kugombea uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi,anaandika Jabir Idrisa

Hoja hiyo imetolewa leo hii na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano na Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdul Kambaya katika taarifa kwa vyombo vya habari ikihusu tamko la Jecha kuwa anamtambua Maalim Seif kuwa mgombea katika uchaguzi huo.

Katika taarifa aliyoitoa jana kupitia kanda iliyorushwa na Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), kuzungumzia ushiriki wa vyama katika uchaguzi aliouitisha kwa shinikizo la Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichomuamuru kuufuta kibabe uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba, 2015, Jecha amesema wagombea wote wanatambuliwa kwa kuwa waliotangaza kujitoa hawakufuata utaratibu wa kisheria.

Jecha amesema utaratibu huo unataka mgombea anayejitoa awasilishe hati ya kiapo iliyoidhinishwa na Mahakama na kwamba kwa kuwa hakuna hata mgombea mmoja aliyetimiza sharti hilo, Tume inatambua wagombea wote wanashiriki uchaguzi.

Tume haikubadilisha karatasi ya kura ya urais wala wagombea uwakilishi na udiwani, japokuwa CUF ilitangaza mapema hata kabla ya tarehe ya uchaguzi wa marudio kutajwa, kuwa haitashiriki uchaguzi huo kwa kuwa si halali bali uchaguzi halali ni ule wa Oktoba mwaka jana uliofutwa kwa lengo la kukandamiza haki ya wananchi kukichagua CUF.

Kufuatia msimamo wa Jecha, Abdul Kambaya amesema Jecha kulazimisha CUF kuendelea kuwa na wagombea kwenye uchaguzi huo, ni sawa na kumlazimisha mwaname kutoa talaka kwa mwanamke ambaye hakumuoa.

“CUF haishtushwi na utaratibu wa mtu anayejitekenya kisha akacheka mwenyewe,” amesema Kambaya akimlenga Jecha kuwa tangu alipoufuta uchaguzi mkuu hapo tarehe 28 Oktoba, bila ya kushirikisha makamishna wa Tume, amekuwa akijitekenya na kucheka mwenyewe.

Ndipo Kambaya akasema kama Jecha anajua sheria, basi aoneshe fomu ambayo Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar anayepigania haki yake ya ushindi wa urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika, alijaza akiomba kuteuliwa na Tume ya Uchaguzi kugombea katika uchaguzi wa marudio.

“Tungestahiki kufanya anachotaka Jecha kama anaweza kutuonesha fomu aliyoijaza Maalim Seif ili kugombea uchaguzi wa marudio wa Machi 20, 2016 ili hoja yake ya kumtaka akajitoe mahakamani kwa kula kiapo iwe na mashiko.

“Hawezi (Jecha, kuonesha fomu hiyo) kwa kuwa Maalim Seif alijaza fomu za uteuzi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, 2015, uchaguzi halali ambao Jecha aliufuta kwa kutumwa na chama chao CCM,” amesema Kambaya.

Amesema kwa kuwa uchaguzi wenyewe anaoupigia chapuo Jecha ili kuridhisha matakwa ya waliomtuma kuvunja sheria, hauko kisheria, ni kujitekenya kudai kuwa anawatambua wagombea kwa kuwa hawakujaza fomu ya kiapo cha mahakamani kujitoa uchaguzi huo.

Jecha amekuwa akihaha kufanikisha uchaguzi wa marudio kwa kulazimisha vyama vyote vishiriki, sambamba na jitihada za CCM kupenyeza fedha kwa viongozi wa vyama visivyo na ufuasi watofautiane na kuwezesha kuunga mkono uchaguzi huo. Vyama kumi vimetangaza kutoshiriki lakini jana Jecha alitangaza kuwa wagombea saba wa urais, wakiwemo waliofukuzwa vyama, waliripoti na kupatiwa ulinzi wa askari polisi.

error: Content is protected !!