June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kamati za maafa zakumbushwa wajibu wao

Mji wa Bukoba, mkoani Kagera

Spread the love

KAMATI za kuratibu maafa katika ngazi ya Serikali za Mitaa zimetakiwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu ya menejimenti ya maafa ili kuweza kujenga jamii yenye uwezo wa kuzuia na kukabili maafa yanayotokea katika maeneo yao. Anaandika Mwandishi Maalum … (endelea).

Akifungua mafunzo ya waratibu wa maafa mkoani Kagera, Juni 24 mwaka huu, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa waKagera, Fikira Kisimba ameeleza kuwa, nguvu ya uwezo wa jamii kuweza kukabili maafa itapatikana iwapo kamati za kuratibu maafa katika ngazi za serikali za mitaa zitawajibika wakati wote kwa kutokuwa zinasubiri uratibu wa maafa yanapotokea.

“Tunazo kamati za maafa kuanzia ngazi za vijiji, vitongoji, kata, wilaya hadi mkoani lakini kamati hizi zinasikika sana wakati maafa yanapotokea hali ambayo si nzuri katika hatua za menejimenti ya maafa, kwani tunaposema menejimenti ya maafa tunazingatia, kuzuia, kukabili  maafa na kurejesha hali ya awali baada ya maafa kutokea” alisema Kisimba.

Kisimba ameongeza kuwa, Mkoa wa Kagera umekuwa ukikumbwa na maafa ya upepo mkali ambapo alibainisha kuwa Wilaya ya Muleba imewahi kupatwa na maafa hayo pamoja na maafa ya Kimbunga katika Kisiwa cha Goziba.

Na akwamba, wilayani Misenyi magonjwa ya mlipuko yamekuwa yakijitokeza hivyo kamati husika zikiwajibika athari za maafa haya zinapunguzika.

Awali akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi (Mipango na Utafiti), Idara ya Uratibu maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Naima Mrisho alizitaka kamati za  serikali za  mitaa  na vijiji mkoani humo kuhusisha maafa na mipango yao ya maendeleo, ili kuhakikisha jamii inakuwa na uwezo wa kupunguza athari za maafa hayo.

“Ili kamati za maafa ziweze kuwajibika ipasavyo hatunabudi Mipango ya Maendeleo katika Serikali za Mitaa ihusishe maafa ili jamii iwe na uwezo wa kukabiliana na maafa wakati janga linapotokea na wakati wa kurejesha hali,” amesisitiza.

error: Content is protected !!