July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kamati za Bunge kuanza Jan 13

Spread the love

KAMATI za Kudumu za Bunge la Jamhuri, zinatarajiwa kuanza Jumatatu ya tarehe 13 – 24 Januari, 2020 jijini Dodoma, kabla ya Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge uliopangwa kuanza tarehe 28 Januari 2020. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli za kamati, wabunge wanapaswa kuwasili jijini Dodoma Jumapili 12 Januari 2020, kwa ajili ya kuanza kwa vikao vya kamati. 

Aidha, shughuli zote za kamati zimepangwa kwa kuzingatia Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari 2016.

Kwa mujibu wa taarifa ya Bunge, shughuli zitakazotekelezwa na kamati hizo ni pamoja na kupokea na kujadili taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu, na bajeti ya serikali kupitia wizara na taasisi zake.

Shughuli hii itatekelezwa na kamati za kisekta na bajeti, kushughulikia hoja mbalimbali za ukaguzi kama zilivyoripotiwa katika taarifa ya hesabu zilizokaguliwa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2018.

“Jukumu hili litatekelezwa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC),” imeeleza taarifa ya kitengo cha mawasiliano na uhusiano wa kimataifa, Ofisi ya Bunge.

Taarifa hiyo imeeleza Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) itafanya ziara za ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma katika baadhi ya miradi ya maendeleo.

Pia kamati hiyo itapokea taarifa kuhusu namna hisa za serikali zinavyosimamiwa katika mashirika na taasisi mbalimbali, ambazo serikali ina hisa pungufu ya asilimia 50.

“Shughuli hii itatekelezwa na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma. Uchambuzi wa sheria ndogo zilizowasilishwa mezani wakati wa mkutano wa kumi na saba wa Bunge, shughuli hii itatekelezwa na Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo,” taarifa hiyo ilieleza.

Mbali na hayo, kutakuwa na kuandaa taarifa ya kamati kuhusu shughuli zilizotekelezwa katika kipindi cha kuanzia Januari 2019 hadi Januari 2020. Shughuli hiyo  itatekelezwa na kamati zote.

Pia taarifa imeeleza, ratiba za shughuli za Kamati za Bunge, pamoja na maeneo ambayo kamati hizo zitafanya ziara zinapatikana katika tovuti ya Bunge.

error: Content is protected !!