SERIKALI ya Tanzania imetakiwa kufanya tathimini dhidi ya changamoto ya kupanda kwa bei ya mahitaji muhimu ikiwemo vyakula, ili iweze kuchukua hatua za haraka kuidhibiti. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Wito huo umetolewa leo Jumatano, tarehe 1 Februari 2023 na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, wakati ikiwasilisha bungeni taarifa yake ya shughuli ilizotekeleza kuanzia Februari 2022 hadi Februari 2023.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, David Kihenzile, amesema Serikali inatakiwa kuweka mikakati ya muda mrefu ili kuzuia hali hiyo.
“Kutokana na changamoto ya kupanda kwa bei ya mahitaji muhimu ikiwemo Mafuta, Mchele na Sukari, ni Rai ya Kamati kwamba Serikali itathimini hali hiyo na ichukue hatua za haraka sambamba na kuweka mikakati ya muda mrefu ili kuzuia hali hiyo,” amesema Kihenzile akisoma taarifa hiyo.
Wito wa kamati hiyo imekuja ikiwa imepita siku moja tangu baadhi ya wabunge kuitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti kudhibiti changamoto ya mfumuko wa bei za vyakula, ili kuwasaidia wananchi masikini ambao hawana kipato cha kutosha kumudu mfumuko huo.
Hata hivyo, Serikali imetoa taarifa bungeni ya kwamba jitihada ilizochukua katika kutoa ruzuku kwenye mafuta, mbolea na maeneo mengine, itasaidia kuondoa mfumuko huo katika msimu ujao wa mavuno.
Kwa kuwa katika msimu wa 2022/23, wakulima wamefanya shughuli za uzalishaji kwa gharama nafuu baada ya Serikali kuweka ruzuku.
Leave a comment