Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kamati Kuu CCM yamaliza kazi, wagombea ubunge kusuka au kunyoa kesho
Habari za SiasaTangulizi

Kamati Kuu CCM yamaliza kazi, wagombea ubunge kusuka au kunyoa kesho

Spread the love

JOTO la wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliojitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania ubunge wa majimbo na wale wa Viti Maalum, linazidi kupanda, kufuatia Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, kumaliza kazi yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Taarifa kutoka ndani ya kikao cha CC kilichomaliza muda mfupi uliyopita mjini Dodoma zinasema, tayari chombo hicho kimepeleka mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu (NEC), juu ya wanachama wanaopaswa kuteuliwa kuwania nafasi hizo.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole, mkutano wa NEC umepanga kufanya kesho Alhamisi, tarehe 20 Agosti 2020 jijini Dodoma.

Kikao cha CC kilichofanyika Ikulu ya Chamwino, kwa siku mbili mfululizo – jana Jumanne na leo Jumatano – chini ya uenyekiti wa Rais John Pombe Magufuli, kilipitia faili la wagombea takribani 1300, kutoka Bara na Visiwani.

Katika kinyang’anyiro hiki, wanachama takribani 11,000 wa CCM, walijitosa kuwania nafasi za ubunge wa majimbo na viti maalum.

“Lengo la kikao hiki, ni kupitia ‘mafaili’ ya wagombea ubunge yaliyoandaliwa na vikao ngazi ya majimbo, wilaya na mikoa, kabla ya kupeleka mandekezo yetu kwa NEC, ambayo ndiyo itakayofanya uteuzi wa mwisho, kesho Alhamisi,” ameeleza mmoja wa wajumbe wa CC ambaye hakupenda kutajwa jina.

Amesema, “pamoja na kwamba NEC inaweza kubadilisha orodha ya wagombea kwa kuchomoa baadhi ya waliopendekezwa na Kamati Kuu, lakini kwa jinsi kazi ilivyofanyika kiuweledi, hatutarajii kuwapo kwa mabadiliko makubwa.”

Mtoa taarifa huyo, hakupenda kuingia kwa undani kuzungumzia suala hilo, badala yake akataka mwandishi kusubiri hadi kesho ambako kutatolewa orodha kamili ya wanachama waliopitishwa kuwania nafasi hizo.

Kabla ya majina hayo kupelekwa CC, Sekretarieti ya Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati ya Usalama na Maadili, zilifanya kazi kubwa ya kuyachakata na kuyafanyia upembuzi wa moja baada ya jingine.

Hii inazidisha presha kwa wagombea zaidi ya zaidi ya 10,000 waliojitosa kuwania ubunge kwenye majimbo 264 ya uchaguzi na kushiriki kura za maoni.

Katika kura hizo za maoni, karibu nusu ya wabunge wa sasa wa majimboo na viti maalum walishindwa kutetea nafasi zao.

Miongoni mwa walioangukia pua kwenye hatua hiyo, ni pamoja na aliyekuwa mbunge wa Babati Vijijini, Jitu Soni; aliyekuwa mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto; aliyekuwa mbunge wa Kyera, Dk. Harrison Mwakyembe; aliyekuwa mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul; aliyekuwa mbunge wa Serengeti, Chacha Marwa Ryoba; aliyekuwa mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba na aliyekuwa mbunge wa Nkenge, Balozi Diodorus Kamala.

Wengine, ni aliyekuwa mbunge wa Mufindi Kusini, Medard Kigola; aliyekuwa mbunge wa Ileje, Janeth Mbene; aliyekuwa mbunge wa Mwanga, Prof. Jumanne Maghembe; aliyekuwa mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe na aliyekuwa mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga.

Katika orodha hiyo ya walioanguka, yumo pia aliyekuwa mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nswanzugwako; aliyekuwa mbunge wa Mvomero, Selemani Sadiq Murad; aliyekuwa mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali; aliyekuwa mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga na aliyekuwa mbunge wa Bagamoyo, Dk. Shukuru Kawambwa.

Wengine, ni Albert Obama, aliyekuwa mbunge wa Buhigwe, mkoani Kigoma; Godfrey Mgimwa, aliyekuwa mbunge wa Kalenga, mkoani Iringa, Abdallah Mtolea, aliyekuwa mbunge wa Temeke; Zuberi Kuchauka, aliyekuwa mbunge wa Liwale, mkoani Lindi, Maulid Mtulia, aliyekuwa mbunge wa Kinondoni na David Silinde, aliyekuwa mbunge wa Momba, mkoani Songwe.

Hata hivyo, Polepole amewahi kukaririwa mara kadhaa akisema, kushinda au kuongoza katika kura za maoni, siyo kigezo kitakachotumika kufanyia uteuzi, huku akigusika wale wote waliojihusisha na vitendo vya rushwa wajiandae “kufundishwa adabu.”

Alisema, chama chake, kitahakikisha wagombea wote waliotuhumiwa kutoa rushwa katika zoezi la kura za maoni, wanaenguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Alisema, “wale ambao hawakutoa rushwa, walifuata katiba na kanuni za chama, wawe na amani; wale waliovunja utaratibu na wavurugaji, tutawafundisha adabu kipindi hiki.”

Aliongeza, “intelejensia ya chama imejipanga vizuri zaidi, katika kushughulikia suala hili. Hawa ni watu hatari sana, kwa maana ya kusimamia utaratibu. Kwa hiyo, hawa wenzetu wametuwekea utaratibu mzuri sana.

Kauli hiyo, ndiyo inayosubiriwa na wadau mbalimbali wa siasa kuona wale waliojihusisha na vitendo vya rushwa watakatwa kama alivyoahidi mwanasiasa huyo, kwamba wana taarifa za kila aliyefanya udanganyifu.

Hali hiyo imeanza kujitokeza kwa walioteuliwa kugombea udiwani ambapo baadhi ya waliokuwa wameongoza kwenye kura za maoni wamekatwa na kuteuliwa wengine ikiwemo walioshika nafasi ya tatu, pili au ya nne.

Kitendo hicho kimeshuhudiwa baadhi ya maeno kama Dodoma kukiibuka vurugu kwa wale ambao walioongoza, lakini majina yao yakakatwa.

Huenda hali kama hiyo inaweza kujitokeza kwa wale ambao majina yao yatakatwa.

Willium Ngereja (katikati)

Tofauti na uchaguzi uliopita mwaka 2015, waliokatwa walihamia vyama vya upinzani ambako walipewa fursa ya kugombea na kutoa ushindani mkali na wengine walishinda.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, watakaokatwa CCM wana nafasi ndogo sana ya kupenya, kwa kuwa zitakuwa zimebaki siku nne kufungwa kwa pazia la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Tume ya uchaguzi imetangaza, tarehe 25 Agosti 2020, kuwa ndio siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu.

Vyama vingi vya siasa kama CUF, Chadema, ACT-Wazalendo na NCCR-Mageuzi, kwa sehemu kubwa wamekwisha kufanya uteuzi wa wagombea wao wa ubunge na hivyo kuwapa wakati mgumu wale watakaokatwa kuendeleza ndoto zao za kuwania nafasi hizo katika uchaguzi wa mwaka huu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!