October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kamatakamata; Lijuakali, Kiwanga wawindwa

Spread the love

PETER Lijuakali, Mbunge wa Kilombero na Susan Kiwanga, Mbunge wa Jimbo la Mlimba yote ya mkoani Morogoro wanawindwa na Jeshi la Polisi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Jeshi la Polisi mkoani humo limeeleza kuwa, linawasaka wabunge hao ili kuwafungulia mashtaka baada ya awali mahakama ya mkoa huo kuwaacha huru kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashitaka yao.

Wabunge hao pamoja na wanachama 13 wa chama hicho walishitakiwa kwa kufanya uhalifu kwa kuchoma moto Shule ya Sekondari ya Kijiji cha Sosi, wilayani Malinyi jambo ambalo upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha.

Hata hivyo, siku chache baada ya kuachwa huru, jeshi hilo lilianza kukamata upya wanachama hao ambapo saba kati ya 13 tayari wamekamatwa huku wengine wakiendelea kusakwa.

Wilbroad Mutafungwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro amesema kuwa, tayari wana ushahidi wa kutosha na kwamba, wabunge hao ni miongoni mwa wanaotafutwa ili kwenda kujibu mashtaka.

Hayo yanaendelea wakati ambao chama hicho kinaendelea kuuguliwa maumivu kutokana na mwenyikiti wake Taifa-Freeman Mbowe na Ester Matiko, Mbunge wa Tarime Mjini kuendelea kusota mahabusu kwa kunyimwa dhamana.

Katika kesi yao ya msingi, Mbowe Matiko na wengine saba wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka 2018 maeneo ya Dar es Salaam.

Wengine ni Mbunge wa Peter Msigwa, Iringa mjini; John Mnyika, Mbunge wa Kibamba na Katibu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji.

Pia wamo Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda; Mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu ambao wote walikuwepo mahakamani.

error: Content is protected !!