July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kamani aja na usimamizi rasilimali, kukuza uwekezaji

Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dr. Titus Kamani akitangaza nia ya kuwania Urais

Spread the love

DAKTA Titus Kamani-Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, ametangaza nia ya kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuomba uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili agombee urais Oktoba mwaka huu, huku akiahidi kusimamia vyema rasilimali na kukuza uwekezaji. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Dk. Kamani ambaye pia ni Mbunge wa Busega mkoani Simiyu, ametangaza nia hiyo leo katika mkutano wa ndani uliofanyika kwenye ukumbi wa grand hall jijini Mwanza na kuhusisha makada mbalimbali wa CCM kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kaskazini.

Amesema kuwa ataendeleza kazi za viongozi waliotangulia, hivyo kipaumbele chake ni kuhakisha kusimamia uchumi wa taifa.

Dk. Kamani ameahidi kuwa endapo akipata ridhaa ya kuwa Rais, atahakikisha anaweka mazingira rafiki ya wawekezaji kutoka nje, kuimarisha huduma ya maji vijijini na miundombinu ya barabara.

Ametaja vipaumbele vingine kuwa ni kuimarisha mshikamano wa uongozi unaowashirikisha wananchi katika matumizi ya rasilimali za nchi, kujenga huduma ya maji vijijini na kuimalisha umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kuimalisha mawasiliano ya kisiasa, jamii na kiuchumi.

Kwa mujibu wa mtangaza nia huyo, endapo vitu hivyo vitasimamiwa na kulindwa, vitawezesha taifa kupiga hatua kimaendeleo na kukuza uchumi wa taifa ambao unaonekana kuyumba hivi sasa.

Kilimo na Mifugo 

Dk. Kamani amesema asilimia 80 ya Watanzania walio wengi wanategemea kilimo na kwamba hiyo ni moja ya mipango yake mikubwa ambayo ataingia nayo Ikulu kuhakikisha inawekwa mipango mizuri kwa wakulima.

“Kama tutashindwa kuwekeza katika kilimo hatutafanikiwa na hata kama tutakuwa na gesi, hivyo ni lazima tukawawezesha wakulima kwa kuwatafutia njia nzuri ya kufanya shughuli zao.

“Nikipata nafasi hiyo, ni dhumuni langu kuona hata Mkuu wa Wilaya anasimamia, hiyo ni pamoja na kwenda shambani kukagua mazao ya wakulima na kiasi wanachovuna,” amesema Kamani.

Katika Mifugo, amesema Tanzania ni nchi ya tatu barani Afrika kwa kuwa na mifugo wengi, lakini imekuwa na tatizo kubwa la malisho na kwamba ni wajibu wake akiingia Ikulu atahakikisha malisho yanaboreshwa.

Pia, kuhakikisha idadi ya viwanda vya kusindika ngozi na nyama vinaongezeka ili kuongeza ajira kwa vijana ambao hawana kazi, pamoja na kutafuta maeneo yamayofaa katika kufanyia kazi hiyo. 

Usimamizi mbovu wa rasilimali

Kwa mujibu wa Dk. Kamani, usimamizi mbovu uliopo serikalini, umekuwa ukichangia kushuka kwa uchumi hivyo, akiwa Rais atahakikisha anaisimamia kikamilifu kwa manufaa ya taifa.

Amesema mara nyingi Watanzania wamekuwa wakilalama juu ya viongozi wa ngazi ya juu kushindwa kuchukua maamuzi magumu katika mambo ya rushwa, kitendo ambacho kinatakiwa kuimarishwa.

Hata hivyo, amesema endapo akiwa Rais, atahakikisha anajenga uwezo kwa watumishi na viongozi kuchukua maamuzi magumu pindi kunapogundulika kumefanyika ubadhilifu.

Pia amesema atahakikisha anasimamia urasmu uliopo serikalini unazibitiwa kwa nguvu zote jambo ambalo litaweza kuliletea taifa maendeleo na kukuza uchumi kwa kila mtanzania.

Rushwa na kodi

Dk. Kamani amesema, akiwa rais, tatizo la rushwa linakomeshwa pamoja na kusimamia ulipaji wa kodi kwa wafanyabiashara wakubwa na wadogo.

Amesema atasimamia watu wanaoshindwa kulipa kodi, kudhibiti kodi sumbufu kwa wafanyabiashara na kutilia mkazo vita vya rushwa kwa watumishi wa umma na viongozi serikalini.

“Endapo utashindwa kudhibiti vitu hivyo, utasababisha nchi kuyumba kimaendeleo, hivyo basi kila mamlaka inapaswa kushiriki katika kupambana na vitendo vya rushwa.

“Kama kiongozi ni lazima nisimamie udokozi wa nguvu za wananchi unaofanywa na watumishi wasiokuwa waaminifu kwa watanzania wenzao, pamoja na kuboresha mazingira kwa wafanyakazi,”amesema.

Wasifu 

Dk. Titus Kamani alizaliwa mwaka 1955 katika kijiji cha Mkula Wilaya ya Busega mkoani Simiyu (zamani Wilaya ya Magu- Mwanza), akiwa mtoto wa tano kuzaliwa katika familia ya watoto 10. 

Alianza safari ya elimu ya msingi mwaka 1965 hadi 1968 na kuendelea na katika shule ya msingi Bwiru na kuhitimu mwaka 1971.

Alihitimu elimu ya sekondari mwaka 1979 na kupata alama za kumwezesha kuendelea na masomo ambapo mwaka 1981, Dk. Kamani alihitimu masomo ya kidato cha tano na sita.

Kwa mujibu wa sheria, kipindi hicho alijiunga na kuhitumu Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kambi ya Bulombora mkoani Kigoma kati ya mwaka 1981 na 1982.

Kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu, Dk. Kamani alifanya kazi kama Afisa Mifugo msaidizi katika Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha kati ya mwaka 1982 na 1984, hiyo ilikuwa ni kwa mjibu wa Azimio la Musoma lililowataka vijana wa kiume kufanya kazi kwa miaka miwili kabla ya kujiunga na chuo.

Baada ya hapo, Dk. Kamani, alijiunga na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine mkoani Morogoro mwaka 1984 na kufanikiwa kuhitimu mwaka 1987 na kutunukiwa shahada ya wa mifugo.

Dk.Kamani amekuwa kada wa 10 wa CCM kutangaza nia ya kutaka kugombea urais tangu chama kilipofungua milango. Wengine waliokwaishatangaza nia ni Makongoro Nyerere, Luhaga Mpina, Prof. Sospeter Muhongo, Edward Lowasa, Mwigulu Nchemba, Steven Wasira, Prof. Mark Mwandosya na Balozi Ali Karume.

error: Content is protected !!